Yaliyojificha uwekezaji wa Hayati Dk Magufuli Chato yawekwa vitabuni

Muktasari:

  • Waandishi nguli wa habari nchini Tanzania wamezindua kitabu 'I am the State' (Mimi ni Dola) chenye kuonyesha maendeleo ya miradi ya uwekezaji yaliyofanyika wilayani Chato mkoani Geita na ukiukwaji wa sheria uliofanyika ndani ya utawala wa hayati Rais Dk John Magufuli wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.

Dar es Salaam. Ikiwa ni miaka miwili tangu aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk John Magufuli kupoteza maisha Machi 17, 2021 akiwa madarakani, waandishi wakongwe wanne wamezindua kitabu kinachoonyesha sura ya kiongozi huyo na uwekezaji mkubwa alioupeleka wilayani Chato.

Absalom Kibanda, Ansbert Ngurumo, Neville Meena na Jesse Kwayu ndio waandishi walioandika kitabu hicho chenye jina 'I am the State' ikiwa na maana Mimi ndio Dola.

Kitabu hicho linaonyesha hali ilivyo sasa wilayani Chato alipozaliwa kiongozi huyo mkuu wa nchi baada ya miradi mikubwa ya maendeleo kuelekezwa huko kwa matakwa yake.

Miongoni mwa mambo yaliyoangaziwa katika kitabu hicho ni wanyama waliopelekwa Chato enzi ya utawala wa Rais Dk Magufuli, ujenzi wa kiwanja cha ndege, uboreshaji mkubwa wa miundombinu, wananchi kukimbilia kununua viwanja, ujenzi wa masoko na miradi mingineyo.

Pia kitabu hicho kimeangazia fedha zilizopelekwa wilayani huko zitarejeshwaje, mpango wa wilaya hiyo kuandaliwa kuwa mkoa uko uliishia wapi.

Kabla ya uzinduzi wa kitabu hicho Ansbert Ngurumo amesema jina la kitabu limetokana na hofu iliyoshuhudiwa baada ya utawala wa hayati Dk Magufuli tangu mwaka 2015-2021 kuelekeza miradi mingi eneo alikozaliwa bila kuwepo mtu aliyehoji.

Amesema kilichofanyika ndani ya utawala wa Dk Magufuli ilikuwa ni historia ya kipekee kwani awamu zote za viongozi waliopita hapa nchini hakukuwa na kiongozi aliyefanya uwekezaji mkubwa eneo alilotoka.

Mbali na uwekezaji walioutaja kuwa na dalili zote za ubinafsi alioufanya kiongozi huyo, amesema upo ukandamizaji mkubwa alioufanya kwenye jamii na kutoa kauli zenye vitisho kuonyesha hakuna aliye juu yake.

"Kama mnafikiri mpo huru kiasi hicho watch it,"Kauli hayati Dk Magufuli enzi ya uhai wake ambaye imeleta tafsiri kwenye kitabu hicho namna ambavyo uongozi wake haukutetereshwa na kitu chochote.

Akizindua kitabu hicho Askofu wa Jimbo la Karagwe mkoani Kagera, Dk Benson Bagonza amesema uandishi wa kitabu hicho uwe chachu kwa viongozi wastaafu na walio madarakani kuandikiwa vitabu kulingana na mazuri na mabaya yao.

Amesema kitabu cha I am the State kinaonyesha namna fedha za umma zilivyotumika nje ya bajeti ya bajeti ya serikali.

"Mambo yaliyotajwa katika kitabu hiki yalitendeka nchi ikiwa gizani na watu walinyamazishwa na haya yaliyoandikwa ni sehemu ndogo ya yaliyotendeka nchi ikiwa gizani"amesema.