Zaidi ya wanamitindo 30 kushiriki maonesho ya mavazi

Muktasari:

  • Zaidi ya wanamitindo 30 na wabunifu 15 wachanga wakiwemo walemavu wanatarajiwa kushiriki maonesho ya mavazi yanayojulikana kama Start Tailoring Business (STB) kwa lengo la kukuza na kuboresha kazi zao.


Dar es Salaam. Zaidi ya wanamitindo 30 na wabunifu 15 wachanga wakiwemo walemavu wanatarajiwa kushiriki maonesho ya mavazi yanayojulikana kama Start Tailoring Business (STB) kwa lengo la kukuza na kuboresha kazi zao.

Akizungumza na Mwananchi jijini Dar es Salaam leo Alhamisi Novemba 25, 2021 muandaaji wa maonyesho hayo, Augustar Masaki amesema maonesho yanatarajiwa kufanyika Novemba 27, mwaka huu katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa, Dar es Salaam.

"Nimekuwa na darasa kwa vijana wanaopenda kuwa wabunifu. Mwaka huu tumepata wenye ulemavu ambao tutashiriki nao katika jukwaa hilo la mavazi," amesema Masaki.

Amesema mavazi yatakayoonyeshwa yametengenezwa na wanamitindo hao wahitimu ambao pia watatunukiwa vyeti na zawadi kwa watakaofanya vizuri zaidi.

Jukwaa hilo litahudhuliwa na wanamitindo mbalimbali huku wasanii wote wakikaribishwa kushiriki.