Zanzibar, Taasisi ya UAE wasaini mikataba kujenga miradi

Muktasari:

  • Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Mfuko wa Misaada wa Sheikh Zayed bin Sultan al Nahyan kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wametiliana saini mikataba ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kisiwani humo.

  

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Mfuko wa Misaada wa Sheikh Zayed bin Sultan al Nahyan kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) wametiliana saini mikataba ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kisiwani humo.

Utiaji wa saini mikataba hiyo ya miradi mitatu katika nyanja za elimu, afya na ustawi wa jamii, umefanyika leo Jumatatu Juni 27, 2022 kati ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Juma Maliki Akili na Katibu wa mfuko huo, Hamad Kudus al Amri na kushudiwa na Rais Hussein Mwinyi Ikulu ya Zanzibar.

Akizungumza baada ya kutia saini, Rais Mwinyi amepongeza hatua ya mfuko huo katika ushirikiano na nia yao ya kukuza maendelo ya taifa hilo.

“Hivi sasa Serikali imejikita katika utekelezaji wa miradi hususani ya afya, elimu na maendeleo ya jamii hivyo wanapotokea marafiki na taasisi kuunga mkono, hatuna budi kushukuru,” amesema Rais Mwinyi

Naye Katibu wa mfuko huo, Hamad bin Kudus al Amri amesema uhusiano kati ya UAE, Zanzibar na Tanzania kwa ujumla una historia kubwa na watazidi kushirikiana.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Dk Saada Mkuya amesema hatua hiyo ya kusaini mikataba ya ujenzi wa shule mbili za Mwembeladu na Mtopepo, hospitali na kituo cha kisasa cha wazee ni kuchochea zaidi ushirikiano baina ya nchi hizo.

“Maeneo haya Rais umekuwa ukiyapa kipaumbele hapa Zanzibar na kwasababu yanaendana na ilani ya CCM ya 2020/2025, Mpango wa Maendeleo wa mwaka 2050 na Mpango wa Maendeleo Muda wa kati Zadec,” amesema