Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Zanzibar yaipiku Dar kutua watalii

Muktasari:

  • ‘Mgeni njoo, mwenyeji apone’ msemo huu unatosha kueleza ongezeko la idadi ya abiria wa kimataifa, wakiwemo watalii, walioingia nchini kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume (AAKIA) uliopo Zanzibar ukilinganisha ule wa Dar es Salaam (JNIA) na viwanja vingine nchini.

Dar es Salaam. ‘Mgeni njoo, mwenyeji apone’ msemo huu unatosha kueleza ongezeko la idadi ya abiria wa kimataifa, wakiwemo watalii, walioingia nchini kupitia Uwanja wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume (AAKIA) uliopo Zanzibar ukilinganisha ule wa Dar es Salaam (JNIA) na viwanja vingine nchini.

Hali hiyo inaelezwa na wachambuzi wa masuala ya anga na uchumi kuwa imetokana na janga la Uviko 19, ambalo limeongeza wageni kwenye uwanja huo.

Ripoti ya takwimu za kitaifa (Tanzania in figures 2021) inayotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaonyesha kuwa uwanja huo kwa miaka mitatu (2017 hadi 2019) AAKIA ilikuwa inapokea baada ya mlipuko wa Uviko-19 ulioathiri dunia nzima kuanzia mwaka 2019, mambo yamebadilika.

Uwanja huo miaka ya 2020 na 2021 uliongoza kwa idadi ya abiria wa kimataifa waliotua na kuipiku JNIA.

Katika kipindi hicho, Jamhuri ya Muungano na Zanzibar ziliweka mikakati mbalimbali kujikinga na maambukizi ya Uviko-19 baada ya kuwepo maambukizi kadhaa nchini, lakini Tanzania visiwani ilinufaika na hali hiyo.

Uwanja ndege wa AAKIA mwaka 2021 ulipokea wageni wa kimataifa 732,000 ukifuatiwa na JNIA uliopokea wageni 604,000 wa kimataifa, ikiwa ni tofauti ya wageni 128,000.

Uwanja unaofuatia kuingiza wageni wengi ni wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ulioshika nafasi ya tatu kwa kupokea wageni wa kimataifa 150,000 huku viwanja vingine nchini kwa ujumla wake vikipokea wageni wa kimataifa 4,000 kwa kipindi cha mwaka huo.

“Wakati ule wa Uviko-19 watalii wengi Tanzania walikuwa Zanzibar, kwa hiyo ndege kutoka mataifa mbalimbali zilienda kuwachukua raia wake, hii inaweza kuwa imesaidia kuongeza idadi ya watalii Zanzibar baada ya janga hilo kuisha,” alisema Juma Fimbo ambaye ni mtaalamu wa masuala ya usafiri wa anga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Masoko ya Utalii Zanzibar, Mohamed Mansoor alisema takwimu hizo zinaonyesha jinsi utalii wa Zanzibar ulivyokua kutokana na ndege nyingi kubwa kuutambua uwanja huo, ambao hivi sasa unapokea ndege nyingi.

“Kuongezeka kwa wageni wa kimataifa Zanzibar ni ishara kuwa shughuli za utalii zimeongezeka na pia ndege kubwa kutoka maeneo mbalimbali ya dunia zinaweza kutua AAKIA tofauti na ilivyokuwa awali,” alisema Mansoor.

“Tunadhani wageni wengi waliokuja Zanzibar kupitia uwanja huu wa ndege (AAKIA) watakuwa ni watalii kwa sababu karibia asilimia 30 ya Pato la Taifa la Zanzibar linachangiwa na shughuli hizo,” aliongeza waziri huyo.

Takwimu hizi zinabainisha kuwa karibia nusu ya abiria wa kimataifa (asilimia 48.8) walioingia nchini mwaka 2021 kupitia usafiri wa anga walishukia Zanzibar kwenye uwanja wa AAKIA.

Katika mwaka 2020, abiria wa kimatifa waliowasili katika viwanja vya ndege nchini walikuwa 943,000, idadi ambayo iliongezeka hadi milioni 1.5 mwaka 2021.

Kutokana na ongezeko hilo la wageni, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ya kuweka miundombinu na huduma kwa wageni hao.

Miezi minne iliyopita, Waziri wa Utalii na Malikale wa Zanzibar, Simai Mohammed Said alifanya mazungumzo na Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Hussain Ahmad Al Homaid kwa ajili ya kudumisha usafiri wa anga baina ya nchi hizo, hasa wakati wa Kombe la Dunia litakalofanyika November nchini Qatar ili kusaidia kuongeza utalii nchini.

“Tumezungumza kuhusu njia za kuwapata baadhi ya watalii ili wabaki Tanzania wakati na baada ya Kombe la Dunia kuanza, ili waweze kutazama mechi Doha na kurejea Tanzania kama makazi yao makuu wakati wote wa mashindano,” alisema Simai.