Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ziara ya Russia haitaathiri mahusiano yetu na nchi nyingine

Muktasari:

  • Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kikazi nchini Russia kati ya Juni 3 hadi Juni 5 iliyolenga kujenga mahusiano ya kidiplomasia na ushirikiano kibiashara.

Dar es Salaam. Serikali imesema ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Russia haitaathiri uhusiano wa kidiplomasia wala ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na mataifa mengine duniani.

Imeeleza kuwa Tanzania inaendelea kusimamia msimamo wake wa kuendeleza diplomasia ya wazi na ya masilahi mapana ya kitaifa.

Rais Samia Suluhu Hassan alifanya ziara ya kitaifa nchini Russia kati ya Juni 3 hadi Juni 5, 2026 kwa mwaliko wa Rais wa Russia, Vladimir Putin iliyolenga kujenga mahusiano ya kidiplomasia na ushirikiano kibiashara.

Ziara hiyo kwa mkuu wa nchi imemfanya Rais Samia kuwa wa pili kutoka Tanzania kuitembelea nchi hiyo, tangu alivyofanya hivyo Rais wa kwanza, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere miaka takribani 50 iliyopita.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumapili Juni 6, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati akijibu swali la mwandishi wa habari juu ya uwepo wa wasiwasi wa ziara hiyo inavyoweza kuathiri mahusiano na nchi nyingine ambazo zimeiwekea Russia vikwazo.

Profesa Kitila amesema kuna tofauti kubwa kati ya uhusiano wa kidiplomasia na masuala ya vikwazo yanayotolewa na baadhi ya nchi.

Amesema hadi sasa hakuna nchi yoyote iliyovunja uhusiano wa kidiplomasia na Russia ikiwa ni pamoja na Marekani, Ulaya na Ujerumani licha ya kuwepo kwa vikwazo vya kiuchumi vinavyolenga sekta au taasisi maalumu.

Amefafanua vikwazo vya kiuchumi si sawa na kuvunjika kwa uhusiano wa kidiplomasia, akibainisha kuwa nchi zinaweza kuendelea na mawasiliano ya kisiasa na kidiplomasia hata kama kuna hatua za kiuchumi zilizowekwa kwa sekta au watu binafsi.

Profesa Kitila amesema msimamo wake wa muda mrefu ni kuunga mkono utatuzi wa migogoro duniani kwa njia ya amani na mazungumzo badala ya matumizi ya nguvu za kijeshi.

Profesa Kitila amesema Tanzania inaamini kuwa migogoro yote inapaswa kuanzia na kumalizika mezani kupitia mazungumzo kwa kuzingatia misingi ya amani ya kimataifa na mfumo wa Umoja wa Mataifa.

“Tunataka migogoro yote itatuliwe kwa njia ya amani. Dunia inapaswa kurudi kwenye utaratibu wa kimataifa unaozingatia matakwa ya Umoja wa Mataifa,” amesema.

Amesema Tanzania itaendelea kuendesha sera yake ya mambo ya nje kwa kuzingatia masilahi ya kiuchumi na kitaifa, bila kujifungamanisha upande mmoja wa mgogoro wa kimataifa.

Amesema katika mazingira ya sasa ya migogoro ya kisiasa, nchi nyingi zinaendelea kushirikiana na pande tofauti ikiwa ni pamoja na mataifa yenye migogoro ya kisiasa kwa kuzingatia uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi.

Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na washirika wake wote wa jadi na wapya ikiwa ni pamoja na mataifa ya Magharibi, Asia na Mashariki ya Kati huku ikisisitiza kuwa ushirikiano huo unaendelea kukua katika sekta za uwekezaji, miundombinu na biashara.

“Tanzania itaendelea kushiriki katika diplomasia ya kimataifa kwa uwazi huku ikilinda uhuru wake wa maamuzi na masilahi yake ya kiuchumi,” amesema Profesa Kitila na kuongeza

“Tunakwenda kuzungumza na kila mtu. Hii ni dunia ya ushirikiano mpana lakini tutaongozwa na masilahi ya Tanzania.”