Zijue sababu matokeo ya awali uchaguzi Kenya kutofautiana

Muktasari:

Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika jana, Jumanne Agosti 9, yameanza kutolewa na vyombo vya habari mbalimbali huku yakionyesha tofauti kutoka chombo kimoja hadi kingine.

Dar es Salaam. Matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Kenya uliofanyika jana, Jumanne Agosti 9, yameanza kutolewa na vyombo vya habari mbalimbali huku yakionyesha tofauti kutoka chombo kimoja hadi kingine.

Matokeo hayo ya awali yanaonyesha mchuano mkali kati ya mgombea wa Kenya Kwanza na Naibu Rais, William Ruto na mpinzani wake Raila Odinga wa Azimio la Umoja.

Kwa sasa Wakenya wanasubiri Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kutangaza matokeo ya jumla.

Wakati IEBC ikisubiriwa kutangaza matokeo ya jumla, vyombo vya habari vimeendelea kutoa matokeo ya awali kutoka katika vituo mbalimbali vya kupigia kura.

Kwa mujibu wa tovuti ya Daily Nation ya Kenya imeeleza sababu za vyombo vya habari kutoa matokeo tofauti.

Imesema kuwa hatua ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuruhusu vyombo vya habari kufanya majumuisho ya matokeo ya Uchaguzi huo, vyombo hivyo vimeanzisha vituo vyao vya kufanya majumuisho ya kura.

Ingawa wote wanapata data kutoka kwa tume ya uchaguzi, takwimu zinatofautiana katika vyombo vya habari kutokana na baadhi ya mambo ikiwamo kasi ya kuchakata data na idadi ya wafanyakazi wanaofanya kazi hiyo.

Pia katika kuchukua matokeo hayo, hakuna mpangalio maalumu au wa kufanana wa kupakua matokeo hayo na kila anayefanya hesabu hizo anaanza na idadi fulani ya fomu ambazo anaweza kuzijumlisha na kisha kutoa matokeo ya awali.

Hata hivyo, matokeo hayo yanatokana na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) kwa kuwa tume hiyo imeziweka fomu za matokeo namba 34A na 34B katika tovuti yake.

“Kumbuka matokeo yanayotangazwa katika vituo vya kupigia kura ni ya mwisho na ndiyo yapo kwenye tovuti. Matokeo ya tovuti ya umma ndiyo tume itategemea wakati wa kujumlisha kura katika kituo cha kitaifa cha kuhesabia kura,” Daily Nation imemnukuu Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati.

Kwa mujibu wa kituo cha kuhesabia kura cha Nation Media Group, hadi kufikia saa 7:50 mchana, matokeo ya awali yalionyesha kuwa Naibu Rais William Ruto alikuwa akiongoza katika kura kwa kura 3,445,516 (51.44%) dhidi ya Raila Odinga wa Muungano wa Azimio la Umoja One wa Kenya aliyepata kura 3,209,400 (47.91%).

Mgombea urais wa chama cha Roots alikuwa na kura 28,529, huku David Mwaure Waihiga wa Chama cha Agano akiwa na kura 14,936.

Kwa mujibu wa Daily Nation matokeo hayo ya awali yanahusisha jumla ya vituo 21,714 kati ya 46,229 vilivyohesabiwa na timu ya NMG, ambayo ni jumla ya kura 6,698,381.

Hata hivyo pamoja na kila chombo cha habari kutoa matokeo yake lakini mwishowe matokeo hayatatofautiana kwa kuwa wamechukua sehemu moja.

 IEBC itaanza kutangaza matokeo hayo baada ya kukamilisha ukusanyaji wa fomu na taratibu zinazotakiwa