Zitto kupigania ujenzi barabara kuunganisha Kigoma-Katavi

Muktasari:

  • Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ameendelea ziara ya kichama katika Mkoa wa Kigoma na kuahidi kuishinikiza Serikali kujenga barabara ya Simbo-Rukoma-Kalya-Mpanda kwa kiwango cha lami ili kuondoa adha ya usaifiri kwa wananchi.

Uvinza. Kiongozi wa chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe ametangaza kampeni maalumu kuishinikiza Serikali kujenga barabara ya Simbo-Rukoma-Kalya-Mpanda kwa kiwango cha lami, ili ipitike kipindi chote cha mwaka.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Rukoma Wilaya ya Uvinza jana Jumatano, Novemba 22, 2023, Zitto amesema pamoja na kuwaondolea wananchi adha ya usafiri wakati wa masika, barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 234 pia ni muhimu kiuchumi kwa sababu inaunganisha mikoa ya Kigoma na Katavi.

“Barabara ya Simbo-Rukoma-Kalya inapita katika vijiji vinavyopakana na nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa njia ya maji kupitia Ziwa Tanganyika, hivyo ni moja ya barabara ya kimkakati kiusalama inayotakiwa kupitika kipindi chote cha mwaka,’’ amesema Zitto.

Kutokana na upungufu wa kibajeti, mwanasiasa huyo ameshauri barabara hiyo kujengwa kwa mfumo wa EPC+F inayotoa fursa kwa mkandarasi kukubaliana na Serikali kujenga barabara kwa fedha zake, halafu Serikali inamlipa kidogo kidogo kwa muda mrefu kulingana na bajeti kila mwaka wa fedha.

“Mwaka 2022, Serikali imetangaza zabuni maalumu ya ujenzi wa barabara nane tofauti kwa mfumo wa EPC+F; Kigoma tunataka barabara ya Simbo-Kalya-Mpanda nayo iingizwe kwenye mpango huo kutokana na umuhimu wake kimkakati, kiulinzi na kuunganisha mikoa ya Kigoma na Katavi,’’ amesema.

Amesema kutokana na ubovu wa barabara, wananchi wanaosafiri kwa basi kutoka mjini Kigoma kwenda Kijiji cha Kalya wilayani Uvinza hulipa nauli ya Sh20,000 kwa safari moja, bei inayokaribiana na nauli ya Sh19,000 kwa mabasi ya kawaida au Sh26,000 kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma umbali wa kilomita 451 kwa mujibu wa bei elekezi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra).

“Yaani wananchi wa Uvinza wanalipa nauli kubwa kutoka kijiji kimoja kwenda kingine kuliko wanaosafiri kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma kupitia mikoa ya Pwani na Morogoro. Hii haikubaliki,’’ amesema Zitto.

Awali, Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Petro Ndolezi amesema kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara ya Simbo-Rukoma-Kalya, wananchi wanalazimika kununua bidhaa na huduma kwa bei juu kulinganisha na maeneo mengine yanayofikika kirahisi.

“Soda yenye ujazo wa mililita 350 inauzwa Sh1,200 kulinganisha na bei ya Sh600 Kigoma mjini, Uvinza na maeneo mengine yanayofikika kirahisi,’’ amesema Ndolezi.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Hadija Ramadhani, mkazi wa Kijiji cha Rukoma akitaja vifaa vya ujenzi kuwa miongoni mwa bidhaa zinazouzwa ghali kijijini hapo kulinganisha na maeneo mengine.

“Hapa Rukoma, mfuko mmoja wa saruji unauzwa kati ya Sh28,000 hadi Sh30,000 kulinganisha bei ya Sh18,500 hadi Sh24,000 kwenye maeneo mengine,’’ amesema Hadija.

Akizungumzia kilio cha wananchi kuhusu barabara ya Simbo-Rukoma-Kalya kupitika kwa shida wakati wa masika, Meneja wa Wakala wa Barabara Mkoa wa Kigoma, Narcis Choma amesema ofisi yake inafanya kila linalowezekana kuhakikisha barabara hiyo inapitika kipindi chote cha mwaka kwa kufanya ukarabati wa mara kwa mara katika maeneo korofi.

“Hii ni barabara ya changarawe na tunajitahidi kufanya ukarabati kila wakati kulingana na uwezo wa kibajeti, ili ipitike kipindi chote cha mwaka,’’ amesema Choma.

Kuhusu ujenzi wa kiwango cha lami, meneja huyo amesema: “Kwa sasa barabara ya Simbo-Kalya haiku kwenye mpango wa kujengwa kwa lami mwaka huu wala mwaka kesho…ninachoahidi ni kwamba kwa uwezo wetu wote Tanroads tutahakikisha inapitika iwe masika au jua.’’

Katika hatua nyingine, kiongozi huyo wa chama cha upinzani amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu migogoro ya ardhi na misako ya mara kwa mara unaofanywa na maofisa uhamiaji kwa madai ya kusaka wahamiaji haramu ambapo ameahidi kufuatilia ufumbuzi kutoka taasisi na mamlaka husika.

Amesema wananchi wa Kigoma wana haki ya kuishi kwa amani wakifaidi matunda ya Utanzania wao kama wanavyofaidi wenzao wa maeneo na mikoa mingine nchini inayopakana na nchi jirani za Kenya, Uganda, Zambia, Msumbiji na Malawi.