Zitto: Tusirejee demokrasia ya kupewa, tuimarishe mashauriano kwanza

Kiongozi wa ACT–Wazalendo, Zitto Kabwe

Muktasari:

  • Licha ya Tanzania kusifika kuwa ni miongoni mwa mataifa yenye utulivu na demokrasia, wadau wanataka yafanyike maboresho katika Katiba iboreshwe ili hali iwe bora zaidi.

Na Zitto Kabwe

Kabla ya Julai mosi, 2022 nilitenga muda kusoma rekodi kuhusu harakati wakati wa kuanzishwa kwa siasa za ushindani nchini Tanzania. Kwa bahati nzuri, kitu hicho kimekuwa ni muhimu kwamba tangu Januari 2021, nimeanza kuandika kitabu kuhusu historia ya siasa za sasa na ushiriki wangu.

Ushiriki umenisukuma kufanya utafiti mkubwa ambao umeishia kwa kuandika makala hii leo.

Lazima niseme na kuwatahadharisha mwanzoni kuwa majumuisho yangu ni tata kidogo. Nilijenga hoja katika hilo kwamba demokrasia ya Tanzania ni ya kupewa na dola na si matokeo ya shinikizo kubwa na tishio kutoka kwa wananchi. Ni katika ahadi hii ndio nategemea kujenga hoja yangu. Baada ya miaka 25 ya siasa za vyama vingi, Serikali inaonekana kuipokonya demokrasia bila kujali ongezeko la ukomavu uliodhihirishwa na Bunge changamfu la wakati fulani ambalo najivunia kuwa sehemu yake.

Hofu yangu kubwa ni uendelevu wa demokrasia hii nayoiona ina mapungufu na ya mpito.

Hata hivyo, kitu kizuri ni kuwepo na fursa ya kusonga mbele kuelekea Bunge changamfu zaidi. Tunapoadhimisha miaka 30 ya vyama vingi nchini, ni wakati wa kuangalia kilichofanyika na kujadili kusahihisha makosa yaliyopita na hivyo kuimarisha demokrasia.

Niwe muungwana kukubali kuwa kulikuwa na harakati chache za kudai vyama vingi na kumaliza mfumo wa kidikteta wa chama kimoja. Nikiwa kijana wakati huo, nilisoma kuhusu watu waliojitoa muhanga kwa ajili ya demokrasia.

James Mapalala, Seif Sharrif Hamad, Shaaban Khamis Mloo, Mabere Nyaucho Marando, Prince Mahinja Bagenda, Chief Abdallah Fundikira, Christopher Kasanga Tumbo, Mashaka Nindi Chimoto, Hamad Rashid Mohamed na Chiku Aflah Abwao ni baadhi ya watu ambao walikuwa mstari wa mbele kudai demokrasia ya vyama vingi.

Kulikuwa na vijana pia katika harakati hizo walioweka rehani elimu yao kwa ajili ya demokrasia. Hao ni James Francis Mbatia, Antony Komu, Msafiri Mtemelwa, Ismail Jussa na wengine wengi. Kulikuwa na wanawake wa kariba tofauti za maisha, lakini ambaye alijitokeza zaidi alikuwa Mama Chiku Abwao. Baadaye yakaja majina kama Mary Kabigi, Fatma Maghimbi, Teddy Kasela-Bantu, Edith Munuo na wengine. Baadhi yao, kwa kupitia kamati ya kitaifa iliyoitwa National Committee for Construction and Reform, au NCCR kwa Tanzania Bara, na KAMAHURU visiwani Zanzibar, waliongoza madai hayo ya demokrasia. Hata hivyo, madai haya yalichukuliwa na CCM na baadaye na serikali na kutugawia aina ya demokrasia iliyoitaka. Haikutokana na majadiliano, wala msukumo wa madai. Ilikuwa demokrasia ya kupewa. Na hii inaweza kuwa dhambi ya asili!

Mwalimu Julius Nyerere, rais na muasisi wa taifa la Tanzania, alikuwa chombo muhimu katika demokrasia hii. Jukumu alilofanya kuiongoza nchi kurudi katika vyama vingi imeandikwa vizuri, na machapisho ya vitabu kuhusu viongozi wa zamani bado yanatolewa. Ushahidi kuhusu uamuzi wa CCM na serikali kutugawia ‘demokrasia’ uko katika kitabu cha Rais Mkapa.

“Mageuzi mengine makubwa ambayo Mwalimu aliongoza, ambayo yalitekelezwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, yalikuwa ni mabadiliko kutoka mfumo wa chama kimoja kwenda wa vyama vingi,” anaandika Mkapa. “Nakumbuka wengi wetu ndani ya chama hawakufurahia hilo, lakini alitushawishi. Alishaona fedheha ya mabadiliko katika nchi zilizounda Sovieti, na tuligundua kuwa katika kiwango kidogo kulikuwa na ulazima wa nchi yetu kutoka katika mfumo wa chama kimoja kwenda vingi. Wakati wa mjadala ndani ya chama kuhusu suala hili, Mwalimu alisema itakuwa ni makosa kutokubaliana na mabadiliko haya. Ni lazima tubadilike sisi au hatutakuwa na uwezo wowote wa kudhibiti mabadiliko hayo. Tutafagiliwa na wimbi hili.” Hii inamaanisha hofu ya kubadilishwa na haja ya kudhibiti mabadiliko, ndiyo ilikuwa lengo la juhudi za Nyerere.

Naye Rais Mwinyi anaelezea mjadala ndani ya chama na upinzani imara ambao uliainishwa na hoja ya ‘ongoza mabadiliko au badilishwa’. CCM iliitisha mkutano maalumu na waziri mkuu wa wakati huo, John Malecela alishauri wajumbe akisema “ni bora kucheza soka kwenye uwanja ambako kanuni zinajulikana, kuliko kucheza chini ya meza gizani”.

Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo, Mkapa aliaandaa wasilisho kikao cha halmashauri kuu iliyokutana Februari, 1990, baadaye kuundwa kwa Tume ya Nyalali mwezi huo. Hilo lilifuatiwa na mkutano baina ya Rais Mwinyi na mkuu wa itikadi wa CCM, Kingunge Ngombale-Mwiru kujadili ripoti ya Nyalali na baadaye mkutano mkuu. Hadi hapo, mambo yalishaandaliwa kwa ajili ya mgawo wa demokrasia.

Kuanzia Aprili 28 hadi Mei 8

Kuanzia uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995 hadi mwaka 2015, demokrasia katika uchaguzi ilikua kutokana na ongezeko la wabunge wa upinzani na matokeo ya uchaguzi wa rais. Kwa wastani, upinzani ulikuwa ukishinda hadi asilimia 40 ya kura. Demokrasia yetu ilikuwa inakomaa, taratibu lakini kwa uhakika.

Lakini mwaka 2015, mambo yaliharibika. Baada ya uchaguzi uliokuwa na ushindani na ambao nusura CCM ipoteze urais, kiongozi mpya wa chama hicho aliamua ‘kuipokonya demokrasia’. Kwa miaka mitano hadi mwaka 2021 nchi iliingia kwenye mchakato wa kuwa ya chama dola, ingawa si kisheria.

Mwanasayansi ya siasa, Michaela Collord anaelezea hali hii kwa kifupi: Kwanza, kulikuwa na juhudi za wazi za kuminya upinzani kujiendesha na kujitangaza. Juni 2016, baada ya miezi kadhaa ambayo shughuli za wabunge wa upinzani zilibanwa ndani ya Bunge, watu 22 walishtakiwa kwa tuhuma za kumtukana rais na magazeti kadhaa yalifungiwa na polisi ikapiga marufuku mikutano ya hadhara hadi mwaka 2020.

Rais John Magufuli, ambaye ndio kwanza alikuwa amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa CCM, alisema “hatuwezi kuruhusu watu kuingiza siasa katika kila kitu, kila siku,” na baadaye kuongeza “ni wakati gani watu watafanya kazi na kujenga taifa?” Hatua hii ilikwamisha vyama vya upinzani kujijenga.

Wakati huo, Msajili wa Vyama vya Siasa akakuza mgawanyiko ndani ya moja ya vyama vikubwa vya upinzani, CUF, akitambua na kupitisha fedha za Serikali katika kikundi kidogo, huku akikataa kuutambua upande ulioongozwa na katibu mkuu, Seif Sharif Hamad.

Hatua hii ilisababisha kundi la Hamad kujiondoa mwaka 2019, na kujiunga na ACT-Wazalendo, chama ninachokiongoza. CUF ikabakia kuonekana kama chama kinachoungwa mkono na dola.

Serikali ya Awamu ya Tano ilitumia jitihada hizi na mikakati mingine kudidimiza upinzani. Hiki kilikuwa kipindi cha ongezeko la vitisho, ukatili dhidi ya viongozi wa upinzani na wafuasi wao. Katika kipindi hiki mnadhimu mkuu wa upinzani, Tundu Lissu, alinusurika kuuawa na “watu wasiojulikana”. Nilikamatwa mara 16 katika kipindi cha miaka mitano na kushtakiwa kwa uchochezi na mahakama ya wilaya miezi michache kabla ya uchaguzi. Viongozi wengine wengi wa upinzani na wabunge walipatikana na hatia ya makosa ambayo yalionekana ya kubambika, kwa mfano Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Halima Mdee (Kawe), Esther Bulaya (Bunda) na Freeman Mbowe wa Hai.

CCM ikahamasisha wimbi la madiwani na wabunge wa kujiondoa na kujiunga nacho, vitendo vilivyosababisha uchaguzi mdogo huku CCM ikiwateua waliohama upinzani kugombea na wakashinda kirahisi chaguzi zenye tuhuma za ukiukwaji taratibu.

Katika kutumia sheria kimabavu, CCM ambao ni wengi bungeni, walipitisha mabadiliko ya Sheria ya Vyama vya Uchaguzi Januari, 2020, yaliyompa mamlaka zaidi Msajili, huku upinzani ukionya kuwa yangerejesha chama kimoja. Katika mabadiliko hayo, sheria ilirahisisha kufuta vyama na pia kumpa Msajili mamlaka ya kumvua mtu uanachama na hivyo kumuondoa madarakani. Mwishoni, katika hatua ambayo ililenga uchaguzi wa mwaka 2020, CCM ilishinda uenyekiti wa vijiji 12,000 na serikali 4,000 za mitaa kwa asilimia 99 katika uchaguzi uliofanyika Novemba 2019. Tanzania ya Novemba mwaka 2020 ilifanana na Tanzania ya Aprili mwaka 1992 wakati Bunge liliporejesha mfumo wa vyama vingi.

Kwa kuwa ilikuwa ni demokrasia ya kupewa, na si matokeo ya madai, mgawaji aliipokonya bila ya kikwazo cha wananchi. Baadhi ya watu watasema kulikuwa na kutokubali, ndio, lakini watu wachache walipambana kuilinda demokrasia na wengi wakasalimu amri kwa mfumo. Baadhi ya watu walioijenga demokrasia, wakaamua kushirikiana na dola kudidimiza walichokijenga.

Sasa tuko kipindi cha kuanzia mwaka 1992 hadi 1995, inaonekana kama vyama ndio kwanza vimeanzishwa na vinaanza kujipanga. Nilivutiwa na maoni ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoandika hivi karibuni katika kuadhimisha miaka 30 ya vyama vingi, alipoahidi mabadiliko ya kisiasa na kiuchaguzi. Haya na mabadiliko ya Katiba ni muhimu wakati wa kuelekea kujenga upya demokrasia yetu. Falsafa yake ya uongozi ya R4 (Reconciliation, Resilience, Reforms and Rebuilding) au kwa Kiswahili Maridhiano, Ustahimilifu, Mabadiliko na Ujenzi Mpya. imetupa matumaini.

Hata hivyo, kuna hatari ya kurejea katika demokrasia ya kupewa. Nashauri kwamba inatakiwa iwe demokrasia ya mashauriano kwa kuwa tunaweza tusiwe nguvu ya kutosha ya kupata demokrasia inayotokana na madai.