Fahamu msongo unavyochangia magonjwa yasiyoambukiza
Dar es Salaam. Msongo wa mawazo ‘stress’ ni hali ya shinikizo la kiakili au la kihisia linalotokana na mahitaji yanayofikiriwa.
Hali hii huleta mfadhaiko wa akili anaoupata mtu kutokana na shida, tabu, dhiki, matatizo au changamoto zinazomkabili katika maisha ya kila siku.
Katika jamii nyingi, hasa za Kiafrika tumekuwa na mitazamo tofauti kwa mtu mwenye msongo wa mawazo, kati ya mitazamo hiyo, asilimia kubwa huja na hitimisho lisilothibitika kitabibu kuwa madhara ya hali hiyo ni pamoja na kupungua uzito na kukonda.
Msongo hutokea pale unapoona uwezo, maarifa au ujuzi wako umefikia mwisho na hauendani na jambo lililopo mbele yako.
Ijapokuwa unapokuwa na hali hii haina maana ni tatizo, kuna msongo unaokusaidia kuchochea na kuboresha utendaji wako wa kazi.
Lakini hali hii inapozidi, husababisha kupata wasiwasi na hatimaye sonona, unapofikia hatua hii ndipo tatizo hilo huanza kuleta matokea hasi katika mwili.
Baadhi ya matokeo hasi yatokanayo na msongo na sonona ni pamoja na uchochezi wa magonjwa yasiyoambukiza kama vile moyo, changamoto ya afya ya akili, sukari, shinikizo la damu, saratani na kiharusi.
Tafiti mbalimbali, ikiwemo ile ya mwaka 2005 kutoka Pubmade Central iliyosimamiwa na National Center for Biotecnology Information (NCBI) ya nchini Marekani, ilithibitisha kuwa kutokana na matokeo mengi hasi ya msongo, asilimia kubwa huwapata wale waliopitia hali ngumu ya kimaisha, talaka, kufiwa na wazazi au watoto, kuongezeka uzito kupita kiasi na kukosa ajira.
Utafiti uliothibitisha haya ni ule uliofanyika nchini Denmark ambao wagonjwa 13,006 nchini humo, walilazwa kwa mara ya kwanza na kuthibitika kuwa wanaopata magonjwa yasiyoambukiza na kujiua ni wale wenye msongo uliopita kiasi, ambao huchochea magonjwa mbalimbali mwilini.
Pia, uchunguzi mwingine ni ule wa meta ambao uligundua asilimia 24 ya wagonjwa wa saratani, hugunduliwa kwa watu wenye sonona ambapo utengenezwaji wa seli za saratani (abnormal cells) ambayo hugeuka saratani, huanza pale unapokuwa na msongo unaotokana na sababu mbalimbali za kimaisha.
Aidha kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu takribani milioni 350 duniani wameathiriwa na tatizo la magonjwa yasiyoambukiza, ambayo chanzo hasa ni msongo wa mawazo.
Vilevile asilimia 75 ya watu wanaokabiliwa na tatizo hili katika nchi zinazoendelea hawapati matibabu, tatizo hili pia linatajwa kuwa chanzo namba moja duniani kwa vifo vya vijana wenye umri kati ya miaka 19 hadi 29.
Utafiti mwingine uliothibitisha kuwa msongo ni chanzo cha magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza ni ule wa Wizara ya Afya, ulioeleza namna msongo unavyochochea na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza.
Kupitia chapisho hilo, magonjwa kama kisukari huchochewa zaidi na hasira, kutozingatia mlo, kuudhika haraka, kitu ambacho husababisha kupanda au kushuka kwa sukari. Yote haya chanzo chake ni msongo na sonona, kusahau pia huingia kwenye magonjwa yasiyoambukiza yanayohusisha afya ya akili.
Msongo pia huchochea unywaji wa pombe, utumiaji wa tumbaku na dawa za kulevya, matumizi ya vitu hivi husababisha magonjwa ya ini, figo, saratani ya mapafu lakini pia uraibu wa dawa za kulevya, yote haya ni magonjwa yasiyoambukiza ambayo sehemu ya chanzo chake ni msongo wa mawazo.
Aidha, mtaalamu wa afya, Dk John Magesa kutoka kituo cha Azania Polyclinic anasema mtu mwenye msongo aina yake ya maisha hubadilika kwa kiasi fulani, hasa upande wa vyakula ambapo kwa namna moja au nyingine huwa chanzo hasa cha magonjwa.
“Wengi tunapokuwa na msongo tunakula chakula chochote kile bila kuzingatia mlo unaotakiwa, aina hiyo ya ulaji wengi tunajikuta tunakula vyakula vilevile ili kushiba. Madhara ya hili ni mtu kuchochea sukari na baadhi ya viungo katika mwili kushindwa kufanya kazi kama inavyotakiwa na kusababisha magonjwa yasiyoambukiza,” anasema Magesa.
Anasema msongo huchochea kutanua mishipa ya moyo au kubana mishipa ya moyo na kushindwa kufanya kazi yake inavyotakiwa, hivyo kusababisha kupata magonjwa ya moyo.
Ameongeza kuwa shinikizo la damu mara nyingi hutokea baada ya chembechembe nyekundu za damu kushindwa kufanya kazi, kazi kubwa ya chembe hizo ni kubeba hewa safi inayopatikana kupitia mzunguko mzuri wa damu kwenye mapafu na moyo.
“Unapokuwa na shinikizo la damu, insulini inashindwa kufanya kazi yake ya kuweka uwiano mzuri wa sukari inayoingia mwilini, hivyo sukari hiyo huingia kwa kiasi kikubwa bila kuchujwa na kuweka uwiano unaotakiwa kuingia mwilini na kusababisha kisukari,” anasema.
Mwanasaikolojia Happy Haule anasema ‘stress’ zinaweza kumfanya mtu anenepe kwa sababu ya kuvurugwa kwa mfumo mzima wa mwili na akili, ambapo mtu hujaribu kujitafutia furaha kupitia kula vyakula bila kujali vina faida au madhara kwa afya yake.
“Mwili kuongezeka au kupungua itategemeana na aina ya mapokeo ya tatizo husika yatakayo sababisha kupata hamu ya kula kupita kiasi au kukosa kabisa hamu na hatimaye kupata vidonda vya tumbo.
“Kuongezeka au kupungua kwa namna moja au nyingine huchochea kisukari, matumizi ya dawa za kulevya kutafuta ahueni ya msongo na mwishowe husababisha uraibu wa dawa za kulevya,” anasema Kalungu.
Anasema mwili wa binadamu huwa una mifumo ya kujitetea ijulikanayo kama (Defensive Mechanism), ambapo mifumo hii hufanya kazi kwa kushirikiana na ubongo na huweza kumuathiri mtu kulingana na mapokeo ya kifikra aliyonayo kuhusu tukio au jambo fulani na ili “stress” iwepo lazima kuwepo na kichocheo au chanzo.
“Ubongo huwa una kemikali mbalimbali ambazo huufanya mfumo wa akili kuitikia katika matukio fulani, ambapo mwitikio huu ukiwa endelevu, unaweza kumfanya mtu apate mabadiliko fulani ya kimwili au kiakili kama asipotafuta ufumbuzi mapema,” anaeleza.
Anaendelea kufafanua kuwa mabadiliko ya kemikali na vichocheo mbalimbali mwilini unaosababishwa na msongo wa mawazo husababisha uzalishaji wa protini na kuchochea baadhi ya magonjwa.
Ameongezea kuwa, moja ya sababu zinazochangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa afya na kusababisha vifo vingi ni msongo wa mawazo, ambao mwishowe huibua na kuchochea ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza.
“Msongo wa mawazo una athari nyingi, kama kusababisha mtu kujiingiza kwenye ulevi uliopindukia, kuvurugika kwa homoni katika mwili, macho kupunguza uwezo wa kuona, baadaye husababisha kifo,” anasema.
Aidha, shirika hilo limeonya kuhusu ongezeko la watu wenye unene uliopitiliza, huku wakitaja hiyo kama sababu kuu ya kuwapo kwa watu wengi wenye maradhi ya moyo, kisukari na ini.
Naye, Mtaalamu wa Lishe kutoka Shirika la World Vision, Dk Daudi Gambo anasema katika kipindi ambacho mtu anakuwa na msongo mkubwa wa mawazo, mwili hutumia kiasi kikubwa cha sukari, hasa katika ubongo kutokana na nguvu kubwa inayotumika katika kufikiria mambo yanayomsibu.
“Hivyo mtu kuhitaji kwa kiwango kikubwa vyakula vyenye ladha nzuri mdomoni na vyenye wingi wa sukari, chumvi pamoja na mafuta kama vile chipsi, soda au bia ambapo matumizi ya muda mrefu ya vyakula hivyo yanaweza kusababisha unene kupindukia na kupata baadhi ya magonjwa yasiyoambukiza,” anasema.
Anaeleza vilevile mtu anaweza kukonda kutokana na kutokula chakula kama inavyohitajika, ikumbukwe katika kipindi hicho mwili wa binadamu huhitaji kwa kiasi kikubwa vyakula vinavyoongeza nguvu na sukari.
“Asilimia kubwa ya watu wakipata msongo wa mawazo hushindwa kula na wengine hujifungia ndani bila kufanya shughuli yoyote na kipindi hicho mwili huhitaji kwa kiasi kikubwa vyakula vinavyoongeza nguvu pamoja na sukari, hivyo kutokula husababisha mwili kupungua na kutozingatia mlo unaotakiwa kutokana na hali yake ya kiafya huchochea maradhi hayo,” anasema Dk Gambo.