Fanya mazoezi mchanganyiko upate utimamu zaidi wa mwili
Muktasari:
- Uchanganyaji wa mazoezi mepesi na mengine husababisha kuwa na matokeo makubwa zaidi kwa utimamu wa mwili kutokana na viungo vingi zaidi vya mwili kufanya kazi sana.
Kila kijana wa kileo angependa zaidi kupata utimamu wa mwili kwa kufanya mazoezi, ili pia awe na mwonekano wa kimazoezi ikiwamo kujazia kiukakamavu.
Inawezekana ni kawaida kila mara kufanya mazoezi mepesi ikiwamo yale ya kutembea, kukimbia kasi ya wastani, kuruka kamba, kuogolea na kucheza dansi ya aerobiki ili kujenga utimamu wa Afya ya mwili.
Mazoezi mepesi ni muhimu kwa afya ya mwili kwani ndiyo yanayowezesha kutukinga na unene ambao ni moja ya tatizo linaloweza kuhatarisha kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo magonjwa ya moyo, shinikizo la juu la damu, kisukari na kiharusi.
Kuchanganya mazoezi haya na mazoezi mengine ikiwamo yale ya unyanyanyuaji wa vitu vizito vya wastani, mazoezi ya vituo vya michezo, mazoezi ya viungo na usingaji wa mwili (massage) huwa matokeo mazuri katika utimamu wa mwili.
Ufanyaji wa mazoezi haya katika programu ya mazoezi mepesi ni kama vile umeweka chumvi katika chakula ili kunogesha zaidi na kuleta ladha ambayo itakufanya kuwa na hamu ya kula zaidi.
Uchanganyaji wa mazoezi mepesi na mengine husababisha kuwa na matokeo makubwa zaidi kwa utimamu wa mwili kutokana na viungo vingi zaidi vya mwili kufanya kazi sana.
Ukiacha faida nyingi za kufanya mazoezi mepesi lakini kuchanganya na zoezi hasa baada ya mazoezi mepesi husababisha misuli ya mwili kupata kazi ya ziada hivyo kuifanya kujengeka na kuimarika zaidi.
Mfano mzuri ni endapo unafanya mazoezi ya kukimbia sana mara kwa mara baada ya zoezi hili utakapochanganya na zoezi kama la viungo vya mwili au kufanya usingaji(massage) mwili hupata faida ya misuli ya mwili kupata utulivu kwa kuondokana na uchovu unaoleta maumivu.
Vile vile unyanyuaji wa vitu vyenye uzito wa wastani mara baada ya kufanya mazoezi mepesi huchangia misuli ya mwili katika maeneo ya mikono, tumboni, kifuani, mgongoni kuimarika zaidi na kujengeka.
Kuchanganya mazoezi mepesi na mazoezi haya ya ziada humfanya mwanamichezo hapata hamasa zaidi, kwani hujiona kuwa anafanya kitu kipya hivyo kufanya kwa ari zaidi.
Ni kawaida kwa wafanya mazoezi mepesi katika maeneo ya wazi kuwa na vikwazo mbalimbali ikiwamo hali ya hewa ya mvua au upepo mkali wenye vumbi na msogamano wa magari katika njia za dharula ambazo wafanya mazoezi hutumia kutembea na kukimbilia.
Hivyo mazoezi ya ziada ya unyanyuaji vitu vizito au ya viungo huweza kuwa mbadala kutokana na mazoezi haya yanaweza kufanyika ndani katika eneo dogo.
Zoezi la ziada kama massage linaweza kumfanya aliyefanya mazoezi mepesi kuhisi burudani kutokana na aina hii ya zoezi la viungo kusaidia kuinyoosha misuli na kuipa wepesi mpya.
Vile vile kuifanya mishipa ya damu kutanuka zaidi hivyo damu nyingi kwenda katika misuli hiyo na hatimaye kuondokana na tatizo la misuli kubana linaloweza kujitokeza wakati au baada ya mazoezi mepesi.
Kwa upande wa mazoezi ya ziada ya viungo yenyewe huweza kusaidia viungo vya mwili kuwa na wepesi hivyo kuwa na utayari wa kufanya kazi kwa ufanisi wakati wa mazoezi mepesi.
Jambo hili pia ni moja ya njia za kusaidia kuepukana na majeraha ya michezo kwani kufanya mazoezi ya viungo vya mwili kabla ya kuanza mazoezi mepesi hupasha moto na pamoja na kuipa wepesi kiutendaji.
Pia kufanya zoezi hili kwa mtindo wa kasi na mpaka kushuka na kuwa taratibu mara baada ya mazoezi huweza kuipoza misuli ambayo imetoka kufanya kazi ngumu hivyo kuifanya kurudi katika hali nzuri.
Kadiri unavyoyafanya mazoezi haya pamoja na mazoezi mepesi husaidia kuboresha utimamu wa mwili zaidi, hivyo kupata matokeo chanya ya kiafya.
Mazoezi Mchanganyiko yanawafaa zaidi vijana wanaopenda kuwa na mwonekana wa mwili mkakamavu na mwepesi.