Hizi hapa faida kujifungulia kwenye maji

Muktasari:
- Huondoa hatari ya kuchanika uke na upumuaji kwa mtoto, husaidia homoni za uchungu kwenda haraka bila kupitia mateso ya muda mrefu, kuondokana na uzito uliozidi kwa mtoto hii ni katika kusaidia afya ya mama na mtoto.
Shinganya. Mwanzilishi wa huduma ya kujifungulia kwenye maji Taifa, mkunga mtaalamu Agnes Ndunguru ameeleza faida ambazo humsaidia mama anayejifungua kwenye maji pamoja na mtoto, wakati huduma hii inapotimiza miaka mitatu tangu kuanzishwa nchini.

Akizungumza leo Jumatatu Mei 05, 2025 mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha katika maadhimisho ya siku ya wakunga duniani yaliyofanyika katika viwanja vya zimamoto vilivyopo halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga mkoani humo.

"Mimi ni mwanzilishi wa huduma ya kujifungulia kwenye maji nchini Tanzania, ambapo huduma hii husaidia kuondoa hatari ya kuchanika uke, kuondoa hatari za upumuaji kwa mtoto, husaidia homoni za uchungu kwenda haraka bila kupitia mateso ya muda mrefu, kuondokana na uzito uliozidi kwa mtoto (Obesity)," amesema Agnes.
Naye Rais wa Chama cha wakunga Tanzania, Dk Beatrice Milike amesema kuwa chama kilianzishwa Novemba 1992 na kina matawi 42 nchini pamoja za wanachama 5,000, kundi lililo mstari wa mbele katika kutoa huduma.
"Wakunga wako mstari wa mbele kutoa huduma kwa asilimia 90 ya huduma zote, kundi hili linapunguza vifo kwa asilimia 87, endapo watumishi watapewa mbinu bora na tumekuwa tukitoa mafunzo mbalimbali kwa wakunga kuongeza weledi," amesema Dk Beatrice.

Mganga mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Yudas Ndungile amesema kuwa Serikali katika kipindi cha miaka minne imefanya mambo makubwa yanayoonekana kwenye sekta ya afya mkoani humo.
"Hospitali mpya nne zimejengwa na mbili zilizokuwa na muda mrefu zimefanyiwa marekebisho, vituo vya afya 18 vimejengwa na kutoa huduma za upasuaji, uboreshaji wa vyumba vya wagonjwa, kuna magari ya wagonjwa 18 yaliyoongezwa pamoja na watumishi 920 wapya walioajiriwa," amesema Dk Ndungile.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha ametoa shukurani kwa Serikali kwa kuboresha sekta ya afya mkoani humo na kutoa takwimu za ongezeko la wakina mama wanaojifungulia katika vituo vya afya.

Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA) Daktari mkunga Beatrice Mwilike akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wakunga duniani.
"Katika kipindi cha mwaka 2015/2016 kulikuwa na asilimia 66 ya kinamama wanaojifungulia katika vituo vya afya rasmi, kuna ongezeko hadi asilimia 85 kwa mwaka 2025," amesema Macha.