Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huduma za dharura zapunguza vifo hospitalini kwa asilimia 31 Tanzania

Muktasari:

  • Kiwango cha vifo kimeshuka kutoka 116 hadi 81 kwa kila wagonjwa 10,000 waliolazwa. Mafanikio hayo yamechangiwa na mafunzo kwa wahudumu wa afya, upatikanaji wa vifaa muhimu na kuboreshwa kwa huduma za wagonjwa mahututi.

Dar es Salaam. Tanzania imeandika mafanikio katika sekta ya afya baada ya kurekodi kupungua kwa asilimia 31 ya vifo vya wagonjwa waliolazwa hospitalini.

Hatua hiyo imekuja kutoka na utekelezaji wa mpango wa Huduma Muhimu za Dharura na Wagonjwa Mahututi (Essential Emergency and Critical Care - EECC) katika vituo 79 vya afya na hospitali kwenye mikoa mitano ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Kigoma, Katavi, Songwe, Mtwara na Zanzibar.

Kulingana na taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), matokeo hayo yanaifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zinazoonesha ushahidi wa mafanikio ya matumizi ya EECC.

Mpango huo, unaofadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), unalenga kuboresha huduma za msingi kwa wagonjwa walio katika hali mahututi kwa kutumia mbinu zinazoweza kutekelezwa hata katika mazingira yenye rasilimali chache.

Kwa mujibu wa matokeo ya utekelezaji wa programu hiyo kwa kipindi cha mwaka 2024 hadi 2025, kiwango cha vifo vya wagonjwa waliolazwa hospitalini kilishuka kutoka vifo 116 hadi 81 kwa kila wagonjwa 10,000 waliolazwa.

Aidha, utoaji wa huduma muhimu kwa wagonjwa mahututi umeongezeka kwa kiwango kikubwa, huku utekelezaji wa viwango vya EECC ukipanda kutoka asilimia 27 hadi asilimia 75 katika vituo vilivyoshiriki.

Mafanikio hayo yamechangiwa na uwekezaji katika kuwajengea uwezo wahudumu wa afya, kuimarisha mifumo ya usimamizi wa huduma na kuhakikisha vifaa muhimu vya kuhudumia wagonjwa mahututi vinapatikana katika vituo vya kutolea huduma.

Katika utekelezaji wake, zaidi ya wahudumu 1,000 wa afya pamoja na viongozi zaidi ya 200 wa mifumo ya afya walipatiwa mafunzo ya EECC, huku vifaa vya kitaalamu, miongozo ya kazi na nyenzo za kusaidia utoaji wa huduma vikisambazwa katika vituo vilivyoshiriki.

Mpango huo ulijikita katika kuboresha uwezo wa wahudumu wa afya kutambua mapema wagonjwa walio katika hali mbaya na kuwapatia huduma za haraka kabla hali zao hazijawa mbaya zaidi.

Pia ulijumuisha uteuzi wa waratibu wa EECC katika kila kituo cha afya, kuimarisha upatikanaji wa vifaa na dawa muhimu, pamoja na kuweka mfumo wa ufuatiliaji wa matokeo na mrejesho wa utekelezaji.

Tathmini ya programu hiyo inaonesha kuwa maarifa ya wahudumu wa afya kuhusu huduma za dharura na wagonjwa mahututi yaliongezeka kutoka asilimia 31 hadi asilimia 67.

Mpango wa EECC uliongozwa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na MUHAS, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), pamoja na Global Affairs Canada.

Wadau wa afya wanaamini kuwa kuendelezwa kwa mpango huo kutasaidia kuboresha ubora wa huduma za afya nchini, kuongeza uwezo wa wahudumu wa afya na kuendelea kupunguza vifo vinavyoweza kuzuilika katika hospitali na vituo vya kutolea huduma.

Mtaalamu wa afya ya binadamu, Dk Ernest Winchislaus, amesema hatua hiyo ni kubwa zaidi katika sekta ya afya.

“Wakati programu nyingi za afya zimekuwa zikijikita katika kuanzisha teknolojia za kisasa au kupanua huduma za kibingwa, EECC imeonesha kuwa kuimarisha huduma za msingi za dharura na wagonjwa mahututi kunaweza kuokoa maisha ya watu wengi kwa kiwango kikubwa,” amesema.

Amesema kupungua kwa asilimia 31 ya vifo vya wagonjwa waliolazwa hospitalini, kutoka vifo 116 hadi 81 kwa kila wagonjwa 10,000 waliolazwa, si takwimu za kawaida.

Amesema takwimu hizo zinawakilisha maelfu ya wagonjwa walionusurika kutokana na wahudumu wa afya kutambua mapema hali zao kuwa mbaya, kuanza matibabu ya kuokoa maisha kwa wakati na kutoa huduma muhimu kwa ufanisi.

Aidha, amesema ongezeko la utekelezaji wa EECC kutoka asilimia 27 hadi asilimia 75, pamoja na kuongezeka kwa uelewa wa wahudumu wa afya kutoka asilimia 31 hadi asilimia 67, linaonesha kuwa kuwekeza kwa watu kupitia mafunzo ni muhimu sawa na kuwekeza katika miundombinu na vifaa tiba.

“Moja ya nguvu kubwa ya EECC ni kwamba imebadili mtazamo wa utoaji huduma kutoka kuzingatia ugonjwa pekee hadi kumweka mgonjwa katika kitovu cha huduma kulingana na ukubwa wa hali yake. Wagonjwa mahututi hupatikana katika kila idara ya hospitali, ikiwemo wodini za magonjwa ya ndani, uzazi, watoto, upasuaji na idara za dharura,” amesema.

Hata hivyo, amesema kuwa katika nchi nyingi zenye kipato cha chini na cha kati, ikiwemo Tanzania, wagonjwa hao mara nyingi hutibiwa katika wodi za kawaida badala ya vyumba maalumu vya uangalizi maalumu (ICU).

“Mafanikio yanayotia moyo zaidi ni kwamba baadhi ya hospitali na vituo vya afya vinavyotekeleza EECC vimeanza kutumia fedha zao za ndani kuendeleza mafunzo na kupanua utekelezaji wa programu hiyo,” amesema.

Dk Ernest amesema huo ni ushahidi kwamba EECC imeanza kujengeka kama sehemu ya mfumo wa kawaida wa utoaji huduma za afya badala ya kuwa mradi unaotegemea ufadhili wa nje.

Mara nyingi, miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo hupata mafanikio ya muda mfupi, lakini hupoteza nguvu ufadhili unapokoma.

Akizungumzia matokeo ya utekelezaji wa mpango huo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Dk Jonathan Budenu, amesema umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya wajawazito na kupunguza idadi ya wagonjwa wanaohitaji rufaa.

"Kumekuwa na upungufu mkubwa wa vifo vya akina mama tangu utekelezaji wa EECC ulipoanza. Pia, idadi ya wagonjwa wanaopelekwa rufaa imepungua kwa kiwango kikubwa. Kwa sasa tumerekodi kifo kimoja tu cha mama katika hospitali ya wilaya, huku halmashauri nzima ya wilaya ikiwa haijarekodi kifo chochote cha mama. Hili halijawahi kutokea katika historia ya eneo hili," amesema Dk Budenu.