Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mambo 10 ambayo mwanamke hapaswi kumficha daktari

Mambo ambayo yanamfanya mgonjwa kutokuwa muwazi kwa daktari ni aibu, wasiwasi, kutojiamini, hisia za kuonekana mzembe, fikra za kuonekana si mwaminifu, kudharaulika, kuonekana mzembe na mjinga.Tabia ya wagonjwa wa namna hiyo haiwasaidii bali inawaharibia.

Muktasari:

Daktari anapokosa ushirikiano mzuri kwa mgonjwa huweza kutoa tiba ambayo haina tija na pengine huhatarisha zaidi afya za mhusika

Kwa kawaida, mgonjwa anatakiwa kumwambia daktari ukweli kuhusu matatizo yake yote ya kiafya ili aweze kusaidiwa kupata tiba sahihi. Daktari naye kwa upande wake, hana budi kuwa mkweli kwa mgonjwa, japokuwa kuna wakati madaktari hujikuta katika wakati mgumu kuwaambia wagonjwa wao mambo ambayo wanahisi kuwa yatawasababishia hofu, kihoro, huzuni, kukata tamaa na kupoteza matumaini.

Najua ni jambo lisilopendeza daktari akigundua kuwa mgonjwa wake amemficha ukweli au amemdanganya kwa kusema uongo hasa pale anapomuuliza kuhusu habari muhimu zinazohusu taarifa nyeti za maisha binafsi. Lakini pia mgonjwa hupoteza imani kwa daktari akibaini kuwa amemdanganya hata kama ni kwa sababu nzuri.

Hii inaonyesha kuwa, uhusiano kati ya daktari na mgonjwa utakuwa na manufaa iwapo utajengwa katika msingi wa maadili ya ukweli na uwazi daima. Daktari anaweza kuzuia habari mbaya kwa mgonjwa bila kumwambia uongo. Pia, mgonjwa anaweza kumwambia daktari ukweli wa mambo yake ya siri kwa lugha nyepesi isiyosababisha aibu.

Jambo la msingi katika uhusiano wa tiba ni kujenga mazingira ya kuaminiana na kutunza siri kuhusu habari njema zinazopatikana katika mazingira ya tiba. Kabla ya kutafuta daktari wa kukutibu, lazima ujiulize swali hili: “Je! ninamwamini daktari huyu?”

Kumdanganya daktari au kumficha siri kwa namna yoyote ile, kunaweza kuleta madhara zaidi katika afya ya mgonjwa kuliko madhara kwa upande wa mtoa tiba.

Ukweli ni kwamba, uzoefu wa kazi, mara nyingi madaktari hubaini uongo wa wagonjwa na wakati mwingine jambo hilo huwakatisha tamaa na kuwavunja moyo wa kutoa msaada stahiki.

Madaktari wengi wanapobaini uongo wa wagonjwa, hujisikia vibaya kwani huona kuwa, wao si muhimu kwa mgonjwa husika.

Uongo wa mgonjwa usipobainika, unaweza kumfanya daktari kutoa matibabu yasiyo na msaada au yanayohatarisha afya ya mgonjwa. Madaktari hushindwa kutambua matatizo ya wagonjwa na kutoa tiba sahihi na salama, pale wanapopewa taarifa zisizo sahihi.

Baadhi ya tafiti zinabainisha kuwa, idadi ya wagonjwa wanaowadanganya madaktari kuhusu afya zao au kuzuia baadhi ya taarifa muhimu ni kubwa kufikia kiasi cha mgonjwa mmoja kati ya wanne. Hii ni sawa na asilimia 25 ya wagonjwa wanaoenda hospitalini kila siku.

Utafiti uliofanywa na WebMD mwaka 2004, ulibaini kuwa asilimia 38 ya wagonjwa wanawadanganya madaktari au hawasemi ukweli kuhusu utekelezaji wa maagizo wanayopewa hospitalini.

Hii hujitokeza zaidi kwa magonjwa yanayosababisha unyanyapaa, mapenzi ya jinsi moja, idadi kubwa ya wapenzi, utoaji wa mimba, uvutaji wa sigara, matumizi ya pombe, dawa za kulevya, matumizi ya ugoro pamoja na kuchanganya dawa za asili na zile za hospitalini.

Mara nyingi hali hii hutokea kama mgonjwa atahisi kuwa daktari au mhudumu wa afya atamhukumu kimaadili. Pia wagonjwa wengine hupenda kuwafurahisha madaktari ili wasichukie kwa kufikiri kuwa wagonjwa hawafuati kwa makusudi maelekezo sahihi ya tiba wanayopewa.

Wagonjwa pia, hujikuta wakiwaambia madaktari uongo kwa kupunguza uzito, kujifanyisha au kuongeza chumvi kwenye matatizo yao ya kiafya.

Lengo huwa ni kuvuta usikivu wa madaktari kwa matazamio ya kupata huduma bora zaidi. Wagonjwa wengine pia huwa na matazamio ya kuandikiwa vipimo au dawa fulani na anapomshauriwa au kupewa vipimo na dawa tafauti, mgonjwa anaweza kumwambia daktari kuwa dawa hiyo inamsababishia matatizo wakati si kweli.

Jambo jingine linalowaingiza wagonjwa katika tabia hii ni kutaka kuandikiwa cheti cha kupumzika kazi (sick sheet) au kupata upendeleo wa kupata chakula kizuri. Hii hutokea hasa kwa wanafunzi wa shule za sekondari na vyuo.

Wanawake wanaongoza

Miongoni mwa wagonjwa wengi ambao hujikuta katika wakati mgumu kuwaambia madaktari ukweli ni wanawake. Wanawake wengi wenye matatizo ya siri wamekuwa wakiwaficha madaktari wao.

Jambo ambalo kila mwanamke anapaswa kulifahamu ni kwamba, yapo mambo ambayo anaweza kuona kama tatizo la kawaida au lisilohusiana na ugonjwa wake na akalifanya kuwa siri, lakini kumbe ni dalili muhimu ambayo ingemsaidia daktari kugundua tatizo kubwa la kiafya linalomsumbua au lililoko njiani kumuathiri.

Yapo mambo mengi, lakini hapa nayataja kumi. Hayo ni mwanamke anapohisi maumivu wakati wa kujamiiana, kuota nywele nyingi mwilini au ndevu, kukosa hamu ya tendo la ndoa, maji yenye harufu mbaya kutoka ukeni, kuwa mjamzito, hamu ya tendo la ndoa kupita kiasi, uvimbe njia ya haja kubwa, kuota kinyama kwenye njia ya haja kubwa, tabia ya kufanya mapenzi kinyume cha maumbile na kutumia vipodozi haramu.

Mengine ni mwanamke kuficha kuwa anatumia njia za kupanga uzazi au  ana ujauzito, jambo ambalo linaweza kumfanya daktari kumwandikia dawa ambayo inaweza kumuathiri au kulingana na hali halisi iliyopo.

Mwanamke anaweza akawa ameathirika kwa vipodozi lakini humficha daktari akiamini atampatia dawa ambayo itamtibu. Hali hii inaweza kumfanya asipone haraka kwa kutopata dawa mwafaka au akaathirika zaidi kutokana na kuendelea kuvitumia vipodozi vyenye sumu.

Wapo wanawake ambao pia hushindwa kuwaeleza madaktari ukweli kuhusu mzunguko wao wa hedhi na kiasi cha damu wanachopata kila wanapoingia kwenye mazingira hayo kila mwezi. Hii ni njia mojawapo inayoweza kuonyesha ishara au dalili fulani ambayo ni muhimu kwa daktari kurahisisha uchunguzi wa matatizo yanayomkabili mwanamke.

Anapohisi maumivu wakati wa kujamiiana, inaweza kuwa dalili ya matatizo makubwa kama vile Uambukizo katika Mfuko wa Uzazi (PID), uvimbe tumboni (Fibroid), kugandamana kwa via vya uzazi (pelvic adhesions) au kuota kwa misuli ya mfuko wa kizazi sehemu zingine za mwili (Endometriosis). Mambo hayo yanaweza kusababisha mimba kutunga nje ya kizazi au mwanamke asipate ujauzito.

Mwanamke kuwa na nywele nyingi mwilini, kuota ndevu nyingi au kuwa na ukavu wakati wa tendo la ndoa inaweza kuwa ni dalili ya tatizo la kukosekana kwa ulinganifu wa vichocheo vya jinsi mwilini.

Kinachoweza kuchochea pia matatizo haya ni uvimbe katika tezi za mayai. Mara nyingi matatizo ya tezi za mayai ya mwanamke husababisha ugumba.

Kuota kinyama kupitia njia ya haja kubwa inaweza ikawa ni dalili za saratani au bawasiri. Mwanamke akiwa na tatizo hilo hana budi kumweleza daktari ili hatua mwafaka zichukuliwe na kukuepusha na madhila ya maradhi hayo. Ukumbuke magonjwa kama haya yanapocheleweshwa kupatiwa tiba haraka, yanaweza kuwa sugu na yatakayochukua muda mrefu wa tiba kiasi cha kumkatisha tamaa mgonjwa.

Harufu mbaya ya majimaji katika sehemu za siri, inaweza kuwa dalili ya uambukizo wa bakteria au hatua za awali za saratani ya shingo ya kizazi. Kwa sababu hiyo ni vizuri kumweleza daktari kwa uwazi jambo hili ili utibiwe badala ya kufanya siri kwa kujipulizia pafyumu zenye manukato makali na kujisafisha mara kwa mara kwa kutumia sabuni zenye kemikali.

Jambo la msingi ni kuhakikisha kuwa unakuwa muwazi na mkweli kwa daktari wako ili aweze kukupa huduma unayostahili kupata.

Kama humwamini daktari fulani, kiasi cha kushindwa kumwambia siri zinazohusiana na matibabu yako, una haki ya kutafuta daktari unayemwamini. Unapaswa kujisikia salama na huru ili kupata huduma bora za matibabu. Huduma bora ni haki ya msingi kwa kila mwanamke au mgonjwa yeyote.