Njia za kukabiliana na tatizo la kusahau

Maisha ni kupanda na kushuka kunakoweza kumsababishia mtu kuwa katika mtanziko wa mawazo yanayoweza kusababisha kusahau baadhi ya mambo.

Hali hiyo katika maisha ni ya kawaida, lakini inapojirudia mara kwa mara na kusababisha watu walio karibu yako kukereka na tabia hiyo, wataalamu wa afya wanasema ni dalili ya ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu.

Hali hiyo ni tofauti na anayoisema Justine Zablon (26), anayesimulia siku moja alihaha kuutafuta ufungua ambao aliushika mkononi.

“Nafikiri hili ni tatizo, kuna siku nilizunguka kuutafuta ufunguo wa nyumbani kwangu ambao niliushika mkononi, nilitumia kama sekunde 60 kuutafuta, lakini nilipotulia nilishangaa nimeudondosha chini…kwangu niliona tatizo, japo hali hiyo haikunirudia tena,” anaeleza.

Anna Christopher, mkazi wa Tabata anasema baba yake mwenye umri wa miaka 64 anasumbuliwa na tatizo hilo aliloeleza tayari wamempeleka hospitali kwa matibabu.

“Baba yangu anaweza kukuambia jambo akasahau alikuambia nini, unamkumbusha jambo linakuwa kama hamjawahi kuzungumza. Hii kwenye familia inatutatiza ndio maana tulikaa na kumpeleka hospitali. Ni tatizo la mara kwa mara kwake,” anasema.

Tatizo la kusahau linafafanuliwa na Daktari Bingwa wa Ubongo na Mishipa ya fahamu wa Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Alpha Kinghomella anayesema ni mara chache ugonjwa huo kuwapata vijana, akiwataja wenye umri mkubwa zaidi kusumbuliwa na tatizo hilo.

“Ni mara chache kuwakuta watu wenye umri chini ya miaka 50 wana tatizo la kumbukumbu. Linakuwepo, lakini si hali ya kuwekwa katika viwango vya ugonjwa, ndio maana sheria za kazi zimeweka utaratibu mtu anapofikia miaka 55 hadi 60 astaafu kwa maana kwamba uwezo wake wa kupambanua mambo unapungua kutokana na seli zinazotumika kukumbuka kupungua,” anaeleza.

Dk Kinghomella anaeleza kadiri umri wa mtu unavyokwenda ndivyo uwezo wa ubongo wake kufanya mambo unavyopungua.

Anasema ubongo hufanya mawasiliano kutokana na mabadiliko ya kemikali ndani ya kiungo hicho, hivyo kadiri mtu anavyokuwa mzee uzalishaji wa kemikali hizo hupungua, jambo ambalo huenda kuathiri uwezo wa mtu kuwa na kumbukumbu.

Mambo anayotaja kuwaweka vijana kwenye tatizo la kupoteza kumbukumbu ni unywaji wa pombe kupitiliza, matumizi ya dawa za kulevya kupitiliza pamoja na ugonjwa unaokwenda kuathiri uzalishaji wa kemikali zinazohusika na kumbukumbu kwenye ubongo.

Kupata ajali nako kunatajwa na Dk Kinghomella kuwa chanzo cha moja kwa moja mtu kupoteza kumbukumbu, hasa mgonjwa anapopata tatizo kwenye ubongo, hali inayomsababisha kupoteza kumbukumbu.

“Mtu anapopata ajali, jambo la kwanza hupata mshtuko na ubongo kupoteza mawasiliano, sasa mgonjwa huyu anapotoka katika hali hiyo kurejea kwenye hali ya kawaida kuna mabadiliko mengi yanatokea.

“Mabadiliko hayo yanaweza kusababisha athari kwenye ubongo na seli zikapotea au kukosa damu na kufa, hiyo inakuwa chanzo cha kumbukumbu ya mtu kutokuwa sawa,” anaeleza.

Kwa upande wake, Dk Peter Kyombya anasema kupoteza kumbukumbu zipo sababu nyingi, mojawapo ni kutokana na msongo wa mawazo na kutokuzingatia lishe bora.

“Ulaji wa lishe bora unaweza kukusaidia kukukinga na magonjwa hayo pamoja na mazoezi. Pia ni muhimu kuepuka unywaji wa pombe kupitiliza,” anaeleza.

Dk Daniel Magomele anasema ubongo wa mbele ndio unaohusika na utunzaji wa kumbukumbu, hivyo jambo lolote lenye kuathiri eneo hilo kunaweza kuathiri kumbukumbu ya mtu (mfumo wa maisha wa kila siku wa mtu) hatua ambayo kitaalamu ndio hushauri mtu kutafuta matibabu.

“Dalili za ugonjwa huu ni mtu kuuliza maswali ambayo tayari ameshauliza, kuchanganya maneno mfano unasema kitanda kumbe unamaanisha meza, kuchelewa kukamilisha shughuli ambazo umeshazoea,” anaeleza.


...Anachosema msaikolojia

Mtaalamu wa saikolojia, Ramadhani Masenga anasema mbali na kusahau mara kwa mara kuwa ni tatizo, anaongeza kuwa wakati mwingine binadamu wanakuwa na tabia ya kusahau vitu vidogo vidogo kutokana na tabia iliyojengeka kwamba wanapofanya vitu vikubwa vinatambulika na vinawapatia sifa mapema.

“Kutaka kukimbia kufika haraka tunapotaka hivyo tunajikuta tunakazania vitu vikubwa na kusahau vitu vidogo, jambo lingine ni ile kutaka kusifika kwenye jamii, mfano unaweza kuzungumza na mtu mipango yake, lakini akakutajia mipango mikubwa ambayo akiitaja utamuona mtu wa tofauti. Hali ile inampa nguvu na faraja.

“Jambo ambalo hatujui vitu vidogo ndio vinatengeneza vitu vikubwa, hivyo tunakimbia kufanya vitu vikubwa bila kujua thamani ya vitu vidogo,” anaeleza.

Dk Kinghomella anasema tatizo la kusahau linatibika, lakini kupitia visababishi vyake na kama imechangiwa na ulevi kupindukia, suluhu yake ni kuacha ulevi.

Kama changamoto hiyo imetokana na umri anasema, hauwezi kurudishwa nyuma, lakini kwa watu wa karibu na mtu mwenye changamoto hiyo lazima wamsaidie kufahamu kwanza anasumbuliwa na tatizo hilo.

“Mtu akishaeleweshwa ana shida ndio unaweza kumpeleka kwa mtaalamu wa masuala ya fahamu, jambo la pili kuna namna ya kuufanya ubongo ukarejesha ile mifumo ya taarifa iliyopo, mfano kumpa mgonjwa dawa, jambo lingine ni kumfanyisha mazoezi tiba ili kurejesha ubongo kwenye hali ya kawaida,” anaeleza.

Ili kumsaidia mgonjwa wa aina hiyo, Dk Kinghomella anasema ni lazima jamii iepukane na unyanyapaa.

Jambo analoshauri daktari huyo kuepukana na changamoto hiyo ni kuufanyisha ubongo kazi, hasa kusoma vitabu, kucheza michezo mbalimbali yenye kuchangamsha ubongo, jambo ambalo anaeleza husaidia kuchelewesha tatizo la watu kusahau.

“Ukisoma vitabu vya hadithi au chochote kile husaidia ubongo. Kuna baadhi ya vitu kama ubongo hauvifanyii kazi muda mrefu vinapotea, michezo kama karata, drafti ni nzuri, na wale wenye umri mkubwa kusoma vitabu ni nzuri kwa sababu unaufanya ubongo kuwa imara.

“Kwa wale ambao wameanza kupata tatizo la kusahau ni muhimu waanze kufanya shughuli zenye kuchangamsha ubongo,” anasema.


Takwimu za WHO

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza idadi ya watu wanaoishi na ugonjwa wa shida ya akili na kupoteza kumbukumbu na uwezo wa kufikiri inakadiriwa kuwa watu milioni 55.

Kati ya watu hao asilimia 8.1 ni wanawake na asilimia 5.4 ni wanaume wenye umri zaidi ya miaka 65. Idadi hiyo inakadiriwa kufikia watu milioni 78 mwaka 2030 na milioni 139 ifikapo mwaka 2050.

Kulingana na WHO, kila mwaka zinaripotiwa kesi milioni 10, huku asilimia 60 ya matatizo hayo yakitokea kwenye mataifa yanayoendelea.

Pia inasema ugonjwa huo wa kusahau na kushindwa kufikiria ambao watu wengi huita ni kichaa ni moja ya changamoto kuu za kiafya katika kizazi cha sasa na ni sababu ya saba ya vifo duniani huku utafiti wa ugonjwa huo ukichukua asilimia 1.5 pekee ya tafiti zote za kiafya.

Oktoba mwaka jan, WHO ilitoa mwongozo kwa kuwalenga watunda sera, wafadhili, jumuiya za watafiti wa magonja ya shida ya akili ili kuwezesha utafiti kuwa fanisi zaidi, wenye usawa na pale utakapofanyika kuleta matokeo.

Mwongozo huo umetoa maeneo manne muhimu ya kufanyia utafiti ikiwa ni pamoja na kuangalia uzoefu wa tafiti nyingine za magonjwa ya kuambukiza unaonesha nini, maendeleo ya sayansi na teknolojia bila kusahau akili bandia.