Njia za kupata ngozi mwororo ‘glow’ kiafya

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya watu wakihangaika kuwa na ngozi nzuri zenye kuvutia kupitia vipodozi mbalimbali, wataalamu wa afya wametoa dondoo kadhaa za kufuata ili kuwa na ngozi mwororo, wanawake huita ‘kuglow’.
Ili kuwa na ngozi yenye mvuto, ni muhimu kuzingatia usafi wa mwili mzima, lishe, unywaji wa maji ya kutosha, mazoezi, kupata usingizi wa kutosha pamoja na kujiepusha na msongo wa mawazo.
Dondoo hizo zinatajwa, ilhali wengine hutumia bidhaa mbalimbali, ikiwemo vipodozi vya asili au vile vinavyozalishwa viwandani, vidonge au ‘drip’ ambazo hudai zinasaidia kuwa na ngozi nzuri.
Wengine huenda mbali hata kufikia uamuzi wa kufanya upasuaji rekebishi ili tu waweze kuwa na mwonekano wa kuvutia.
Baadhi ya vipodozi hivyo, huifanya ngozi kuwa na rangi moja kati ya sehemu ya mwili wa binadamu ambayo baadhi yao, hasa wanawake hutumia fedha katika kuifanya iwe na muonekano wa kuvutia.
Fatuma Hamduni, mkazi wa Kimara jijini Dar es Salaam anasema kwa mwezi mmoja ana utaratibu wa kutenga zaidi ya Sh150,000 kwa ajili ya kuhudumia ngozi yake.
“Gharama hiyo ni kwa ajili ya kufanya huduma maalumu kwa ajili ya ngozi ya uso pamoja na kusingwa mwili, ambayo hunigharimu zaidi ya Sh80,000.”
Kwa upande wake, Saraphina Lampard anasema kutokana na kipato chake huwa anatenga Sh50,000 kwa ajili ya kununua bidhaa kwa ajili ya kutunza ngozi yake.
Hata hivyo baadhi yao pamoja na kutumia kiasi kikubwa cha fedha bado hawafanikiwi kupata kile wanachokitarajia au matokeo yake kuwa ya muda mfupi.
Mambo ya kuzingatia
Hata hivyo, wataalamu wa afya wanataja dondoo muhimu za kufuata ili kuwa na ngozi nzuri yenye afya.
Akibainisha mambo hayo, Daktari wa ngozi kutoka hospitali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Tumpale Luhanga anasema mtu anapofanya usafi wa ngozi ya uso pamoja na mwili mzima inasaidia kuondoa uchafu uliopo juu ya ngozi.
“Ni muhimu kujitahidi kuoga mwili mzima angalau mara mbili kwa siku, yaani asubuhi na jioni kwa kutumia maji ya uvuguvugu na sabuni,” anasema.
Pia anaongeza kuwa ni muhimu kuzingatia kutumia ‘dodoki’ laini ili kuepusha ngozi kupata michubuko.
Anaongeza kuwa pamoja na usafi wa mwili, vilevile ni muhimu kuzingatia usafi wa nguo unazovaa, mataulo ya kujikaushia maji pamoja na mashuka ambayo mtu analalia.
Anasema kutokuzingatia usafi kunaweza kusababisha mtu kupata changamoto mbalimbali za ngozi, ikiwemo ukurutu.
Jambo jingine muhimu lililotajwa na Dk Luhanga ni kupata muda wa kutosha wa kulala na kupumzika, ni muhimu pia katika kuimarisha afya ya ngozi, kwani hujijenga pale mtu anapokuwa amepumzika.
“Kutopata muda wa kutosha kulala kunaweza kusababisha ngozi kukosa nuru, kuwa na mikunjo pamoja na kufanya ngozi kuzeeka mapema,” anasema.
Anasema kitaalamu inashauriwa mtu kupata muda wa kulala angalau saa sita hadi nane kwa mtu mzima.
Msongo wa mawazo
Pamoja na madhara mengine ya kiafya yanayosababishwa na mtu kuwa na msongo wa mawazo, ikiwemo kuleta athari katika mifumo mbalimbali ya afya ya binadamu, lakini pia ina athari kwa upande wa ngozi.
Akizungumza na Mwananchi, Mtaalamu wa masuala ya chakula na lishe na Meneja mradi wa Afya ya Mama na Mtoto kutoka Shirika la World Vision, Dk Daud Gambo anasema ili kuwa na ngozi nzuri na yenye afya, ni vyema kuzingatia ulaji wa matunda, hasa yale yenye wingi wa vitamin C.
Anataja matunda hayo ni kama vile machungwa, limao, pensheni, nanasi, parachichi na mengineyo yenye asili hiyo, kwani pamoja na kazi yake ya kuusaidia mwili kupambana dhidi ya mashambulizi na sumu za vyakula, pia katika ngozi husaidia kuondoa uvimbe na mikunjo, hivyo kuilinda ngozi yako kutozeeka mapema.
“Pia ni muhimu kwa afya ya ngozi yako sababu inasaida kutengeneza collagen, aina ya protini inayotengeneza ngozi,” anasema.
Pamoja na ulaji wa matunda, Dk Gambo anasisitiza ulaji wa mboga za majani za kutosha kwa siku, kwani zinasifika kwa kuwa na wingi wa Vitamin A katika ngozi, zinahusika katika kusaidia ngozi kuzalisha seli mpya na kuondoa zile zilizokufa, hivyo kupunguza ukavu kwa kutunza ngozi, kuifanya kung’ara na kuvutia.
“Vyakula vingine vyenye wingi wa vitamin A ni pamoja na viazi vitamu, pilipili hoho, broccoli na nyinginezo,” anasema.
Kwa mujibu wa tovuti ya ‘Times of India’, vyakula vingine ambavyo vinashauriwa kwa ustawi wa ngozi yako ni pamoja na mayai, maziwa, samaki, manjano, zabibu huku pia ikiorodhesha vitu vya kuepuka kula au kunywa kwa wingi kwa ustawi wa ngozi yako.
Vitu hivyo ni pamoja na unywaji wa pombe kupindukia, kahawa kuzidi kiwango, pamoja na utumiaji wa sukari, mafuta na chumvi kwa wingi.
Dk Gambo anaongeza kuwa pamoja na kuzingatia lishe, pia ni muhimu kuzingatia unywaji wa maji ya kutosha.
Anasema unywaji wa maji kwa wingi huifanya ngozi kuwa yenye unyevu, laini na yenye kuvutia.
"Maji yanasaidia sana katika kuimarisha afya ya ngozi, hivyo ni muhimu kuzingatia unywaji wa maji kama inavyoshauriwa na wataalamu,” anasema.
Anasema mtu asipokunywa maji ya kutosha husababisha kupata ukavu wa ngozi, hivyo kupunguza mvuto wake.
Anaongeza kuwa inashauriwa kwa mtu mzima kunywa angalau glasi nane za maji kila siku.
Mazoezi
Daktari wa binadamu, Dk Shita Samwel anasema mazoezi yanasaidia mishipa ya damu kupeleka damu kwa wingi katika ngozi, hivyo kuleta lishe katika seli zilizopo katika ngozi na wakati huohuo kitendo cha kutoka jasho husaidia kuondoa takamwili.
Anasema mazoezi mepesi ndiyo ambayo kwa kiasi kikubwa yanachoma mafuta yaliyorundikana maeneo mbalimbali mwilini, ikiwamo chini ya ngozi kama utayafanya kwa muda wa dakika 30 na zaidi kwa siku tano za wiki.
Anafafanua kuwa wakati wa mazoezi viungo vya mwili, ikiwamo misuli hufanya kazi, wakati wa mazoezi ndipo misuli hiyo huvunjavunja sukari ambayo moja ya zao ni joto.
“Joto la ndani linapopanda na kuwa juu, mwili hujibu mapigo ili kuhakikisha kuna joto la wastani, hivyo huupoza mwili na kulinda joto kwa kuruhusu jasho kutoka pamoja na joto.
“Kipindi hiki ndicho ambacho jasho lenye taka mwili hutoka pamoja na joto ili kuupoza mwili, wakati wa kufanya hivi ndipo ngozi kusafishwa…
“Kitendo hiki huwa na faida, kwani hata yale mafuta yanayorundikana chini ya ngozi pamoja na taka nyingine, huondolewa kwa kiwango kikubwa, kipitia vitundu vilivyopo juu ya ngozi,” anasema.
Vilevile anasema mazoezi haya wakati jasho linapotoka huweza kuondoa na vitu vingine ambavyo ni sumu na hata kuua vijidudu vinavyoweza kudhuru ngozi.
Dk Shita anathibitisha kuwa mazoezi hasaidia kuondoa makunyanzi kutokana na tishu za juu ya ngozi kujinyoosha na kutulia huifanya ngozi kuwa imara. Ndio maana wafanya mazoezi wazee huendelea kuonekana vijana.
Anasema husaidia kushusha kichochezi kijulikanacho kama ‘cortisol’ ambacho kinamsababishia mtu kuwa katika hali ya msongo au shinikizo.
“Kiwango chake kuwa juu huchochea kujitokeza kwa chunusi au vipele juu ya ngozi na pia kuharibu nyuzi nyuzi za tishu kuvunjika vunjika, hivyo kuleta makunyanzi,” anasema.
Anasema ndiyo maana wenye shinikizo la akili au msongo wa mawazo, mfano walioumizwa kihisia hutokwa na vipele vingi juu ya ngozi, kwa sababu ya kupanda kwa kichochezi hicho.
Dk Shita anasema kadiri unavyofanya mazoezi, ndivyo pia misuli hutuna na kuimarika, hatimaye ngozi iliyoifunika huvutana na kuonekana ng’aavu isiyo tepetepe.
“Wakati wa mazoezi moyo ukiwa unasukuma damu, ngozi hunufaika kwa kupata kiasi kingi cha damu, hivyo huboreka zaidi, kwani mafuta asili ya ngozi hutengenezwa na kuifanya ngozi kuwa ng’aavu,” anasema.
Tafiti zinaonyesha kuwa mazoezi yanaweza kuisaidia ngozi kujikarabati kwa haraka zaidi, jambo ambalo linaupa uwezo wa kudhibiti saratani ya ngozi kabla ya kupiga hatua.
Hakikisha mazoezi yaendane na lishe bora, ikiwamo protini, mbogamboga na matunda na maji ya kutosha.
Homoni
Licha ya kufanya vitu kadha wa kadha kulinda ngozi isiharibike, kuna sababu za kimaumbile, ikiwamo mabadiliko ya homoni ambayo huifanya ngozi kubadilika na wakati mwingine kupata chunusi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya homoni na kisukari Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Dk Salama Ali anasema homoni ina nafasi kubwa katika kufanya ngozi ya mtu kuwa yenye mvuto, hivyo inapotokea changamoto, huweza kuleta mabadiliko katika ngozi.
"Mfano kwa wanawake homoni za estrogen, progesterone zina nafasi katika kufanya ngozi ya mwanamke kuwa nzuri, inapotokea mabadiliko huweza kusababisha ukavu katika ngozi pamoja na vipele na chunusi," anasema.
Anasema kwa mtu mwenye dalili za kuvurugika kwa homoni, kwanza hufanyiwa vipimo na matibabu yake hufanyika kulingana na majibu ya vipimo.
Mtaalamu wa masuala ya urembo, Isha Mtawa, anashauri pamoja na mambo hayo ni muhimu kumuona mtaalamu wa ngozi kabla ya kuanza kutumia kipodozi cha aina fulani, ili kupata ushauri wa kitaalamu.
“Ni muhimu kuwa na tabia ya kunawa uso mara kwa mara, kuepuka tabia ya kulala na vipodozi vya makeup, pamoja na kujiepusha na ulaji wa vyakula vyenye mafuta na sukari kwa wingi,” anasema Isha.