Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi ya mbinu za Halima alivyopona Kifua Kikuu sugu

Halima Mikidadi akizungumza na mwandishi wa makala hii, Herieth Makwetta.

Wengi tukisikia ugonjwa wa kifua kikuu huwa tunaogopa. Wazo linalomjia kichwani mtu anayekutana na mgonjwa mara nyingi ni hofu ya kuambukizwa.

Lakini umewahi kumfikiria mtu unayekutana naye katika shughuli zako za kila siku kama ofisini, sokoni, kwenye msongamano, vyombo vya usafiri na hata magulio?

Vimelea vya kifua kikuu husababishwa na bakteria ‘Mycobacterium tuberculosis’ ambavyo husambazwa kwenye hewa na muathirika anapokohoa, kupiga chafya, kutema mate, kucheka au kuzungumza.

Hata hivyo, sayansi inaeleza watu wengi wamewahi kupata vimelea vya ugonjwa huu, lakini hawakuugua kutokana na uimara wa kinga zao.

Halima Mikidadi (39), aliyekuwa akiuza samaki alipata kifua kikuu mwaka 2021 bila kufahamu aliyemwambukiza.

Akiwa katani Magugu wilayani Babati, anasema kwenye biashara alikutana na watu mbalimbali na nyakati nyingine alisafiri kufuata samaki.

Akizungumza na Mwananchi Machi mwaka huu, ikiwa ni miezi mitatu tangu alipopona ugonjwa huo, anaeleza namna alivyopitia changamoto za dawa kushindwa kufanya kazi, kukaa chumba cha wagonjwa mahututi, unyanyapaa na kuachwa na mumewe.

Kabla ya kuugua alikuwa katika ndoa yenye furaha yeye, mumewe na watoto wao wanne, lakini mambo yaligeuka alipoanza kuugua na kubainika kuwa ana kifua kikuu.

“Nilianza kuumwa kawaida nikawa naendelea na biashara zangu, changamoto kubwa nikawa naona mwili unachoka sana, nashindwa kula, mwili unaniuma lakini pia nakohoa sana, nilijitibu lakini ugonjwa ukaendelea,” anasimulia.

Halima anasema dawa za hapa na pale hazikumsaidia, hali yake ilizidi kuwa mbaya. Akipitia nyakati hizo anasema alikuwa bega kwa bega na mume wake.

Alipoanza kushindwa kufanya kazi,  mumewe alimpeleka hospitali ya Mrara wilayani Babati kwa ajili ya vipimo zaidi.

“Nikapelekwa hospitalini kupimwa, hapa maradhi hayakuonekana nikaambiwa nikapimwe mkoani, nikaenda. Hapo ndipo nilipobainika nina Kifua Kikuu sugu, wakanipa dawa nikaanza kumeza bila kupata matokeo yoyote,” anasema.

Anasema wakati anaendelea na matibabu, hali ya unyanyapaa ilianza kujitokeza kwa mumewe, hivyo alilazimika kurudi nyumbani kwa wazazi wake. “Dawa nilizokuwa nameza zilinikataa, nikazidi kuumwa na hali ikawa mbaya zaidi. Mwili ukajaa (kuvimba), miguu ikawa minene ndiyo hapo wakaanza kunipima tena.

“Ilifikia hatua mpaka wakanitoa maji kwenye mapafu, wakanipeleka Moshi, Kibong’oto (Hospitali ya kutibu kifua kikuu sugu) nikalazwa na nikaendelea na matibabu kwa miezi saba ndipo nikaruhusiwa,” anasimulia.

Halima anasema aliruhusiwa kurudi mkoani Manyara alikoendelea kuchukua dawa na wakati huo alikuwa amepata nafuu kidogo.

Anasema aliendelea kutumia dawa kwa miezi 18 akamaliza dozi na kurejea katika maisha ya kawaida.

Licha ya kupona, anasema hawezi kufanya shughuli ngumu bali kazi za kawaida pekee.

Kuna nyakati katika ugonjwa huo alipoteza fahamu, “Sikumbuki namna nilipata matibabu, ninakumbuka niliambiwa nina TB sugu,” anasema.

Anapoulizwa iwapo anakumbuka ni lini na wapi alipata maambukizi au iwapo alikuwa na mtu anayekaribiana naye mwenye maambukizi, Halima anasema hakumbuki na hakuna aliyemshuku.

“Sikumbuki ni namna gani niliambukizwa, ninafanya biashara ya kuuza samaki, hivyo kwa kutembea mtaani ninakutana na watu mbalimbali.

“Nilikuwa na mume, nilipoanza kuugua alinihudumia na aliposikia nina Kifua Kikuu sugu alianza kunitenga,” anasema na kuongeza kuwa watoto aliwaacha kwa mumewe na mpaka sasa hawana mawasiliano yoyote.


Kifua Kikuu sugu

Miongo kadhaa nyuma, ugonjwa wa Kifua Kikuu ulimhusisha mgonjwa ambaye tayari ameshaugua, ametibiwa na kutokana na ufuatiliaji hafifu wa dawa, zilijenga usugu na baadaye mgonjwa akapata Kifua Kikuu sugu.

Hali kwa sasa ni tofauti. Halima hakuwahi kuugua, lakini maambukizi ya kwanza akapata Kifua Kikuu sugu.

Kukiwa na ongezeko la kila mwaka la wagonjwa wa Kifua Kikuu nchini, Wizara ya Afya inasema inaanza kupata wagonjwa wengi wapya wa Kifua Kikuu sugu. Kwa mujibu wa takwimu za wizara hiyo, katika miaka mitano kuanzia 2015 kumekuwa na ongezeko la wagonjwa na baadhi wamebainika kuwa na aina hiyo ya TB.

Mwaka 2015 wagonjwa wapya waliogundulika walikuwa 62,000, mwaka 2016 (65,908), mwaka 2017 (69,623), mwaka 2018 (75,845) na mwaka 2019 walikuwa 82,000.

Tatizo hilo limesababisha ugonjwa huo kuwa tishio zaidi kwa kuwa mgonjwa ambaye hajaanza dawa husambaza vimelea kwa urahisi zaidi.

Hali hiyo imetajwa kuwa tishio kwa uchumi wa nchi, ikizingatiwa Serikali kwa taarifa ya mwaka jana ilitumia Sh11 bilioni kununua dawa na Sh4.6 bilioni kwa ajili ya kununua vifaa tiba kupambana na Kifua Kikuu kila mwaka kwa kutoa matibabu bure.

Mratibu wa mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na ukoma kutoka Wizara ya Afya, Dk Allan Tarimo alisema mkoa unaoongoza ni Dar es Salaam ambao una asilimia 20 ya wagonjwa wapya.

Mikoa mingine ni Mbeya, Arusha, Geita na Manyara, huku akiitaja mikoa yenye wagonjwa wachache zaidi kuwa Kigoma, Katavi, Songwe. Pia, Unguja na Pemba.

Dk Tarimo alisema uwezekano wa kupata Kifua Kikuu kutoka kwa mtu unayeishi au kufanya kazi naye ni mkubwa kuliko kutoka kwa mgeni.

Anasema aliyeanza kutumia dawa angalau kwa wiki mbili haambukizi.


Dalili za Kifua Kikuu

Dalili za kifua kikuu kuwa ni kukohoa, wakati mwingine kukiwa na makohozi au damu, kusikia baridi, uchovu, homa, kukonda kwa mwili, kukosa hamu ya kula na kutoa jasho jingi isivyo kawaida, hasa usiku.

“Ugonjwa huu huathiri hasa mapafu, lakini kinaweza kuathiri vilevile sehemu nyingine za mwili na dalili zinaweza kubadilika. Bila kupata tiba huweza kusambaa kwenye sehemu nyingine za mwili kupitia mfumo wa damu.

“Ikishambulia mifupa inaweza kuleta maumivu ya uti wa mgongo na kuharibu maungio ya mifupa, ikishambulia ubongo husababisha meningitis, ikienda kwenye maini na figo huweza kusababisha damu ndani ya mkojo na ikishambulia moyo inaweza kuathiri uwezo wa moyo wa kusukuma damu na kusababisha ‘cardiac tamponade’ ambayo inaweza kuua,” alisema Dk Tarimo.

Anasema makundi yaliyo hatarini kuugua Kifua Kikuu ni wenye VVU, watoto chini ya miaka mitano, wenye utapiamlo na tatizo la lishe; magonjwa sugu ikiwemo saratani, kisukari, wanafunzi wa shule za bweni, wachimbaji migodini na magerezani.

Imeandikwa kwa udhamini wa Bill & Melinda Gates Foundation