Umuhimu wa chanjo dhidi ya saratani shingo ya kizazi
Muktasari:
Lakini, nina imani kubwa kwamba tunaanza kupiga hatua katika kuyakabili maradahi haya baada ya kukamilisha mpango mkakati wa utoaji wa chanjo ya HPV (Human Pappilloma Virus) ili kuwakinga wasichana dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi ambayo inaanzia kwenye mlango wa uzazi na kusambaa sehemu nyingine za mwili.
Kwa muda mrefu sasa nimekuwa nikiziangalia mbinu zinazotumika kupambana na saratani na kubaini bado tunakabiliwa na changamoto nyingi.
Lakini, nina imani kubwa kwamba tunaanza kupiga hatua katika kuyakabili maradahi haya baada ya kukamilisha mpango mkakati wa utoaji wa chanjo ya HPV (Human Pappilloma Virus) ili kuwakinga wasichana dhidi ya saratani ya shingo ya uzazi ambayo inaanzia kwenye mlango wa uzazi na kusambaa sehemu nyingine za mwili.
Saratani hii inashika nafasi ya pili miongoni mwa zinazogharimu zaidi maisha ya wanawake duniani kote. Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa takriban vifo 500,000 vya wanawake hutokea kila mwaka kutokana na saratani hii hasa nchi za Afrika ikiwamo Tanzania.
Kwa mpango huu, naamini utasaidia kupunguza na ikiwezekana kumaliza kabisa vifo vitokanavyo na saratani ya shingo ya kizazi.
Saratani ya shingo ya uzazi inasababishwa na vihatarishi vingi kama vile kujihusha na ngono isiyo salama katika umri mdogo, kuwa na washirika wengi wa tendo la ndoa, magonjwa mengine ya zinaa ikiwemo gonorea, kaswende, hata Virusi vya Ukimwi, ulevi na matumizi ya tumbaku.
Sababu nyigine ni upungufu wa vitamin na maambukizi ya virusi vinavyosababisha saratani hii; human pappilomavirus (HPV).
Kumbuka, saratani huwa haiambukizwi ila virusi hivi huweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Vikiambukizwa kwa mwanamke husababisha saratani hii lakini kwa mwanaume huweza kusababisha saratani ya koo.
Chanjo hii iliyozinduliwa hivi karibuni, ikitolewa kwa umakini na usahihi kwa wasichana wenye umri kati ya miaka tisa hadi 14 itawakinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya HPV vinavyosababisha saratani ya shingo ya uzazi.
Wasichana wenye umri huu ndio walengwa wakubwa wa chanjo hii kuliko makundi mengine kutokana na utendaji kazi wake. Chanjo hii hufanya kazi ikiwa msichana bado hajaanza kushiriki tendo la ndoa.
Kwa mwanamke ambaye ameshawahi kushiriki tendo la ndoa hata mara moja tu, chanjo haitaweza kumsaidia na ndio maana wanawake si walengewa. Wasichana ambao bado hawajabalehe hata wameobalehe lakini hawajaanza kushiri tendo la ndoa itawasaidia kuwakinga dhidi ya virusi vya HPV na saratani ya shingo ya uzazi wakikua.
Aidha, kumekuwa na habari za upotoshaji zinazosambaa miongoni mwa watu kuwa chanjo hii ina madhara ya kiafya kwa mtoto wa kike na hali hii imesababisha hofu kwa wazazi na walezi kwa kuhofia usalama wa wao.
Habari hizi ni upotoshaji na zinapaswa kupuuzwa. Chanjo hii haina madhara yoyote kiafya sana sana itamnufaisha mtoto wa kike hapo baadae na inatolewa kwa umakini mkubwa na wataalamu wenye mafunzo ya kutosha.
Aidha chanjo hii ni nadra kusababisha maumivu sehemu ilipochomwa au kusababisha uchovu na kizunguzungu. Hali hizi huwatokea wasichana wachache na hupotea ndani ya muda mfupi baada ya kuchomwa.
Mpango huu unadhamiria kuwafikia mamilioni ya watoto wa kike nchini na niwaombe wazazi na walezi wajitokeze kuwapa chanjo wasichana wao kwa sababu itawasaidia kuwakinga dhidi ya vifo vya saratani hapo baadaye.