Vifaa vyatolewa kusaidia watoto wachanga kupumua
Muktasari:
- Tafiti za Wizara ya Afya na Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) zinaonesha kuwa vifo vya kukosa hewa vinachangia kati ya asilimia 25–30 ya vifo vya watoto wachanga nchini, huku takwimu za TDHS zikionesha watoto 32 hufariki kwa kila vizazi hai 1,000.
Dar es Salaam. Mradi wa Breathing for Baby (BfB), unaolenga kuokoa maisha ya watoto wachanga wanaozaliwa na changamoto za kupumua, umekabidhi vifaa vya huduma ya watoto wachanga vyenye thamani ya zaidi ya Sh164 milioni kwa hospitali za mkoa wa Dar es Salaam.
Takwimu za Tanzania Demographic and Health Survey (TDHS 2022) zinaonesha kuwa vifo vya watoto wachanga bado ni 32 kwa kila vizazi hai 1,000.
Mradi huo, unaosimamiwa na Chuo Kikuu cha Afya Kishiriki Muhimbili (MUHAS), umekabidhi msaada huo leo Jumanne, Septemba 9, 2025, kwa ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni jitihada za kuboresha uhai wa watoto wachanga na ubora wa huduma za afya ya uzazi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano, Mtafiti Mkuu wa Mradi wa BfB, Profesa Nahya Masoud, amesema vifaa hivyo vitasambazwa kwenye wodi za watoto wachanga, vyumba vya kujifungulia, vyumba vya upasuaji, na hata magari ya wagonjwa.
“Mchango huu wa vifaa ni zaidi ya msaada wa kifaa pekee, ni hatua ya kubadilisha namna huduma za watoto wachanga zinavyotolewa.
“Kuanzia utambuzi wa mapema wa matatizo ya kiafya hadi msaada wa upumuaji kwa watoto wenye shida ya kupumua, vifaa hivi vitasaidia kuokoa maisha na kuimarisha mfumo mzima wa huduma za watoto wachanga,” amesema Profesa Nahya.
Amevitaja vifaa vilivyokabidhiwa kuwa ni pamoja na mashine 50 za kupimia kiwango cha oksijeni kwenye damu na mapigo ya moyo, mifumo 27 ya VAYU bCPAP, ambayo ni vifaa vya usaidizi wa upumuaji kwa watoto wachanga walioko hatarini; mashine 12 za kunyonya uchafu zinazotumika kutoa majimaji, damu au ute kwenye njia ya hewa na sehemu nyingine za mwili.
Vifaa vingine ni toroli 8 za kufufulia wagonjwa (resuscitation trolleys) zikiwa na vifaa muhimu kwa ajili ya huduma ya dharura ya uokoaji uha, kifaa cha kupima kiwango cha sukari kwenye damu, kikiwa na vipimo vyake; na vipimajoto vya kidijitali vinavyopima kiwango cha joto la mwili kwa usahihi.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdul Rajab Mhinte, amesema vifaa hivyo vinatumika kusaidia watoto wachanga wanaozaliwa na changamoto za kupumua na wanahitaji msaada.
Amesema hatua hiyo ni endelevu ya jitihada za Serikali ya Tanzania za kuboresha afya za wananchi, hasa watoto, ambapo jitihada za awali zilikuwa kuboresha afya ya kinamama.
“Jitihada hii sasa inakwenda kuwapa matumaini Watanzania, hasa kinamama na wenza wao, kwamba watoto wao watakaozaliwa watakuwa na afya njema. Inawatoa fofu wale ambao watoto wao watapata shida ya kupumua. Kwa hakika, kwa vifaa hivi afya za watoto zinakwenda kuimarika zaidi,” amesema.
Aidha, Profesa Nahya amesema mradi huo unalenga kuchunguza changamoto za muktadha wa utekelezaji, kupima ubora wa huduma zinazotolewa, kupanua upatikanaji wa tiba ya Continuous Positive Airway Pressure (CPAP), pamoja na kusaidia mafunzo na usimamizi wa wahudumu wa afya.
Amesema pia mradi unahakikisha uendelevu kwa kusisitiza matumizi sahihi, matengenezo ya mara kwa mara, na uwajibikaji wa vifaa.
Baadhi ya maofisa wa afya wa Mkoa wa Dar es Salaam wamekaribisha msaada huo na kuuelezea kama nyongeza kubwa katika juhudi za kupunguza vifo vya watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika.
Vifo vinavyotokana na matatizo ya kupumua na changamoto nyingine za kiafya kwa watoto wachanga bado ni miongoni mwa visababishi vikuu vya vifo nchini hivyo, msaada huu unatarajiwa kubadili hali hiyo.