Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vipodozi hatari vyashamiri katika mitandao ya kijamii

Biashara ya vipodozi hatari vinavyochubua mwili na ambavyo hutengenezwa bila kufuata kanuni na mwongozo wa kitaalamu, imeshamiri katika mitandao ya kijamii na vinawapatia wauzaji mamilioni ya fedha.

Vipodozi hivyo, ambavyo ni mchanganyiko wa mafuta tofauti ya losheni, huwekwa katika makopo ambayo yana picha za wasichana warembo, lakini si rahisi kupatikana madukani.

Pengine ni katika kuikwepa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) ambayo imepiga marufuku vipodozi vinavyobainika kuwa na viambata sumu ambavyo ni hatari kwa mtumiaji, biashara hiyo imeshika kasi kwenye mitandao ya kijamii, huku walengwa wakubwa wakiwa ni wanawake.

Katika matangazo ambayo hutolewa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu vipodozi hivyo, wanawake huelezwa kuwa wakivitumia watakuwa na mwonekano mzuri wa ngozi kwa muda mfupi hata kama wameungua na mionzi ya jua.

Wafanyabiashara hao wanadai vipodozi hivyo pia huondoa mabaka mwilini, kutakatisha ngozi na kuwa mweupe wa wastani, wa kati au kama mzungu kutegemeana na utashi wa mtuamiaji.

Pia, vipodozi hivyo vinaelezwa kuondoa sugu kwenye viwiko vya mkono na miguu pamoja na weusi kwenye makwapa.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika maduka mbalimbali ya vipodozi ya jumla na rejareja eneo la Kariakoo, unaonyesha kuwa bei ya vipodozi hivyo ambavyo vyenye ujazo wa mililita 250 huuzwa kati ya Sh30,000 na Sh50,000, lakini haviuzwi kwenye maduka hayo.

Mmoja wa wauzaji wa vipodozi hivyo, Christina Peter anasema wao huwa wanauza bidhaa zilizosajiliwa na TFDA na siyo ambavyo havijasajiliwa na havijulikani.

Baada ya muuzaji kutajiwa moja ya krimu hizo kama anauza alionekana kuvijua.

“Krimu hiyo haipo hapa dukani. Si unasema vile vinavyotangazwa Instagram? Hapa hatuuzi. TFDA hawavitaki hivyo, kwanza havijasajiliwa, labda uwapigie simu watakuletea ulipo,” alisema.

Mfanyabiashara mwingine mwenye duka la vifaa vya ofisini na shuleni (stationery), aliyejitambulisha kwa jina moja la Fadhili, anasema huwa anashiriki kwa aina tofauti katika biashara hiyo; anapokea oda ya kuchapisha lebo za vipodozi hivyo.

“Unaona kama hii,” anasema Fadhil akionyesha karatasi yenye chapa ya moja ya vipodozi hiyo.

“Tumetengeneza. (Inaonekana) Inatoka Uingereza lakini ni hapa hapa nchini. Mimi ndiyo nimetengeneza kisha inabandikwa kwenye kopo.”

Akizungumzia vipodozi hivyo, ofisa uhusiano wa TFDA, Gaudensia Simwanza alisema baadhi havijasajiliwa na wahusika hawana vibali vya kuvitangaza.

Simwanza anasema changamoto iliyopo kwenye mtandao wa Instagram ni watu kutangaza vipodozi bila kuweka anuani zao kamili.

“Hata kama ukifuatilia anwani yake hupati, unakuta ameweka namba ya simu. Sasa ukipiga mtu (aliyepokea) anakwambia upo wapi nichukue pikipiki nikuletee,” anasema.

“Lakini tunashirikiana na wenzetu wa kitengo cha makosa ya mtandao katika kuhakikisha tunazisimamia. Wale ambao wanatangaza tunawapata ili wapate vibali na kuangalia kama vinafaa kwa matumizi. Pia, tumekuwa tukitoa elimu kwa wananchi kuhusu bidhaa wanazonunua kwamba lazima wajue kama zimesajiliwa na wanunue katika maeneo ambayo hata kama akipata matatizo iwe rahisi kurudi kwenye duka ili tufuatilie.”

Simwanza anasema kabla ya kuanza kutumia kipodozi chochote, watu lazima waangalie kama kina kiambata sumu na viwe vinauzwa kwenye maeneo yanayojulikana.

Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya wateja wa vipodozi hivyo wanadai kuwa kuna tofauti kati ya vipodozi vinavyotengenezwa kienyeji nyumbani na vile vya viwandani ambavyo vilipigwa marufuku.

“Awali, nilikuwa natumia vile vya kununua kwenye maduka lakini ngozi yangu ilikuwa haing’ai. Lakini tangu nianze kutumia vinavyouzwa Instagram (ambavyo havijasajiliwa) ngozi imekuwa nzuri, tatizo bei yake kubwa,” anasema Fransisca Mohammed.

Wataalamu wa afya wazungumza

Mfamasia kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (Moi ), Heri Wagi anasema bidhaa mbalimbali za vipodozi zinazotangazwa kwenye mitandao ya kijamii, nyingi ubora wake haujathibitishwa na TFDA.

Mtaalamu huyo wa dawa anasema vipodozi huwa na kemikali (viambata) zinazoleta athari katika mwili wa binadamu hasa vinapotengenezwa bila kufuata viwango sahihi vya kemikali husika.

“Vipodozi ni mchanganyo wa uwiano rafiki kwa ngozi na mwili ya binadamu na baadhi ya viambata (kemikali) huwa na kazi tofauti kulingana na uwiano wake,” anasema Wagi.

Mfamasia huyo, ambaye pia ni mwanachama wa Famasi Jamii, alitoa mfano wa kiambata aina ya hydroquinone maarufu kwa ajili ya kufanya ngozi iwe angavu akisema inazidi kiwango cha asilimia moja na hivyo huathiri afya ya ngozi.

“Uandaaji wa vipodozi unapaswa uzingatie utaalamu, mwongozo na kanuni zilizowekwa na TFDA ili kuepuka athari kwenye ngozi na mwili kwa ujumla,” anasema.

Kuhusu vipodozi hivyo kubadilisha rangi ya ngozi haraka, alisema ni kutokana na mchanganyiko wake kuwa katika uwiano wa juu, hivyo watu wengi wamekuwa wakivikimbilia na kuviona vizuri.

“Baadhi ya vipodozi hivi vinavyotumika usoni (na mwilini) ili kung’arisha ngozi (kuchubua), vimegundulika kuwa na viambata sumu kama madini aina mercury (zebaki), lead, pamoja na kemikali ya hydroquinone na glutathione,” anasema Wagi.

Mtaalamu huyo anasema vipodozi hivyo huzuia uzalishwaji wa melanin unaohusika kutunza rangi ya asili kwa mtu, hivyo kusababisha ngozi kuanza kuonekana nyeupe hata kama lengo lilikuwa ni kuondoa chunusi.

Dk Abubakari Hassan, ambaye ni mtaalamu wa mionzi na tiba kutoka taasisi ya saratani ya Ocean Road, anasema kemikali zilizopo kwenye vipodozi hivyo hupenya kwenye vinyweleo na kuingia mwilini kisha kuharibu figo, ini, ubongo na sehemu nyingine za mwili.

“Mfano mercury is very toxic metal (zebaki ni sumu kali). Na mara nyingi inaweza kusababisha saratani na maradhi mengine inapowekwa kwenye vipodozi,” anasema.

Madhara yake

Wagi ambaye ni mfamasia anashauri watumiaji wa vipodozi hivyo vinavyoelezwa kuwa vinatoa matokeo mazuri haraka, watambue kuwa madhara yake ni makubwa zaidi kuliko faida.

Anataja madhara yatokanayo na vipodozi hivyo kuwa ni ugonjwa wa saratani, kuungua ngozi na kuhisi maumivu.

“Tafiti zilizofanyika zimeonyesha baadhi ya sabuni na vipodozi vingine vinavyotengenezwa kwa njia zisizo rasmi kuwa huwa na kiasi kikubwa cha madini ya mercury na lead ambayo huweza kusababisha saratani,” anasema mtaalamu huyo.

Pia, anasema ngozi huchubuka kirahisi hasa mtumiaji akipata ajali, hivyo kusababisha kidonda kupona kwa shida.

“Kemikali hizo huondoa mvuto wa kiasili wa ngozi ambao kimsingi hauwezi ukarejeshwa tena,” anasema Wagi.

Anasema madhara mengine ni kushindwa kuhimili jua au joto, hivyo mtu kupata maumivu kutokana na upungufu wa melanin ambayo kazi yake huwa ni kuchuja mionzi hatarishi (ultraviolet radiations). Pia husababisha ngozi kuwasha mara kwa mara na kupoteza mvuto.

“Mzio wa ngozi (allergic reactions) ni madhara mengine makubwa yanayoweza kutokea,” anasema Wagi.

Mfumo wa hewa pia huweza kuathiriwa na baadhi ya kemikali hizo, na hata kusababisha saratani ya mapafu.