Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanasayansi wabaini sababu usonji kukumba zaidi wavulana

Muktasari:

  • Kemikali zisizoharibika ‘PFHxA’ zilizotajwa kuwa chanzo, hupatikana kwenye bidhaa nyingi za kila siku kama chupa za plastiki, nguo na hata maji ya kunywa, ambazo pia zinahusishwa na saratani, ugumba na kasoro za kuzaliwa.

Dar es Salaam. Wanasayansi wamebaini sababu ya kwa nini wavulana wana uwezekano mkubwa zaidi wa kuwa na usonji na tatizo la kutotulia ‘ADHD’ kuliko wasichana, huku kemikali iitwayo PFHxA ikihusishwa.

Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la European Journal of Neuroscience, umeonyesha wavulana wana uwezekano mara tatu zaidi wa kugundulika na tatizo la usonji na kutotulia, ukilinganisha na wasichana.

Kati ya asilimia 22.5 ya watoto wenye usonji nchini Marekani asilimia 14.5 ni wavulana, asilimia 5.8 ya wenye usonji Uingereza asilimia 3.5 ni wavulana, Ujerumani asilimia 8.4 kati yao 6.5 ni wavulana na Canada ni asilimia 11.1 kati yao asilimia nane ni wavulana.

Hata hivyo, nchini Tanzania tafiti zinaonyesha kati ya watoto 10 wenye changamoto ya usonji, wanane ni wavulana.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Rochester wamependekeza wavulana huenda wakawa na mwitikio mkubwa zaidi kwa msongo wa mazingira kama vile kemikali hatari zisizoharibika (forever chemicals) wakati ubongo wao unapoendelea kukua.

Wamesema kemikali hizo huvuruga mawasiliano ya ubongo na kusababisha mabadiliko ya kitabia ya muda mrefu kwa wavulana, kama vile wasiwasi, kushindwa kutulia na ugumu wa kufuata maagizo.

Kemikali hizo hupatikana kwenye bidhaa nyingi za kila siku kama chupa za plastiki, nguo na hata maji ya kunywa, ambazo huchukua maelfu ya miaka kuharibika ambazo pia zinahusishwa na saratani, ugumba na kasoro za kuzaliwa.

Akizungumzia utafiti huo, Daktari bingwa mbobezi na mtafiti wa magonjwa ya watoto, Profesa Karim Manji amesema kwa tafiti zilizofanyika nchini Tanzania, watoto wa kiume wameathirika zaidi na usonji kati ya watoto 10 wanane ni wavulana na wawili wasichana.

Amesema bado haijulikani sababu, ila kuna uwezekano miundo ya neva zao na viini vya homoni zinaweza kuchangia, huku akitaja kurithi kutoka kwa baba kwenda kwa mtoto.

“Utaona baba ana dalili za usonji ni mkimya, asiyependa kuchangamana na watu, mkorofi sana, hawasiliani na watu wengi wanasema ndivyo alivyo kumbe ni usonji.”

Kwa mujibu wa Profesa Manji, anataja kinamama kuzaa kwa upasuaji huchangia changamoto hiyo.

“Wengi walio na usonji asilimia 90 wamezaliwa kwa njia ya upasuaji. Anayezaliwa kwa njia ya kawaida anapita kwenye maji yanayompa msisimko wa ubongo unakua vizuri, hiyo tunadhani inachangia, bado inahitaji utafiti zaidi, huenda wa kiume wana neva zinazoweza kunyonya zile kemikali zikaathiri haraka au ni kurithi kutoka kwa baba,” amesema.


Utafiti

Katika utafiti huu wa sasa, wanasayansi wamebainisha kemikali mahususi iitwayo PFHxA, inayotumika katika vifungashio vya chakula vya karatasi na vitambaa visivyopata doa kwa urahisi.

Watafiti wanasema inaweza kusababisha tabia za wasiwasi zinazohusiana na usonji, lakini cha kushangaza, athari hizo zilionekana zaidi kwa wavulana.

Waliendesha utafiti kwa kuwapa panya wachanga kemikali hiyo kupitia mama yao. Mama panya alipewa chakula cha funza kilichochanganywa na PFHxA wakati wa ujauzito na kipindi cha kunyonyesha.

Kwa kumpa kemikali hiyo kwa njia hii, ilihakikisha kuwa watoto wa panya walipata kemikali hiyo wakati wa ujauzito kupitia damu ya mama na baada ya kuzaliwa kupitia maziwa yake.

Wanasayansi waligundua kuwa watoto wa kiume wa panya walionyesha mabadiliko ya kutisha ya kimaendeleo kama vile kupungua kwa kiwango cha shughuli, kuongezeka kwa wasiwasi na matatizo ya kumbukumbu.

La kushangaza ni kuwa hawakuona mabadiliko kama hayo kwa watoto wa kike wa panya.

Hata baada ya miaka panya hao kufikishwa kwenye kemikali hiyo kwa mara ya kwanza, bado walionyesha mifumo ya tabia inayohusishwa na matatizo hayo, hali inayopendekeza kuwa kemikali zisizoharibika unaweza kuwa na athari za muda mrefu kwenye ubongo.

Mwandishi mkuu wa utafiti huo na mtaalamu wa tiba ya mazingira, Profesa Elizabeth Plunk ameeleza kuwa matokeo hayo kuwa ya kutisha.

"Ingawa athari hizi zilikuwa ndogo, kugundua athari za kitabia kwa wanaume pekee kunafanana na hali nyingi za matatizo ya ukuaji wa neva ambayo huathiri zaidi wavulana," amesema Profesa Plunk na kuongeza;

"Kuelewa athari za PFHxA kwenye ubongo unaokua ni muhimu sana, tunapopendekeza kanuni za kudhibiti kemikali hii."

Watafiti wanatarajia huu kuwa mwanzo wa tafiti nyingi zaidi kuchunguza madhara ya kemikali ya PFHxA, hasa kwenye maeneo ya ubongo yanayohusika na harakati, kumbukumbu na hisia.

Lakini wataalamu wameonya kuwa hii inaweza kuwa ni kwa sababu wavulana hurejelewa zaidi kwa uchunguzi kutokana na dalili zao kuwa dhahiri zaidi, si kwa sababu ya tabia za kurithi.

Hata hivyo wanabainisha kuwa wasichana wenye usonji, wanaweza kuficha baadhi ya dalili kwa kuiga tabia na michezo ya watoto wengine.