Zingatia haya kwa lishe bora ya mtoto

Dar es Salaam. Lishe bora kwa watoto ni kitu muhimu kinachopaswa kuzingatiwa na jamii ili kuwa na watoto wenye afya na makuzi bora.

Hii ni kwasababu lishe husaidia mwili kukua vyema, kujengeka na kuimarisha kinga ya mwili kupambana na magonjwa.

Mtaalamu wa Lishe Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji anaeleza namna sahihi ya kumlisha mtoto akisisitiza umuhimu wa kutumia siku 1,000 ambazo ni kipindi muhimu cha ukuaji na maendeleo ya mtoto ambacho ubongo hukua kwa kasi.

“Hizi ni siku kuanzia ujauzito hadi mtoto anapofikisha miaka miwili, kipindi ambacho mtoto bado anatengenezwa, kuanzia miezi sita hadi miaka miwili mtoto anapoanza kula chakula wakati ambao mahitaji yake ya virutubisho mwilini yanahitajika kwa kiasi kikubwa hasa protini, nishati lishe, vitamin na madini.

“Hivyo ni muhimu sana kumpatia mtoto vyakula kama nyama, samaki, mayai, maziwa, vyakula vya nafaka kama mahindi, mchele bila kusahau matunda na mboga za majani kwa kuvitengeneza kwa njia ambayo itakuwa rahisi kwa mtoto kumeza,” anasema.

Baada ya miaka miwili hadi mitano, Husna anasema hicho ni kipindi mtoto anaanza kujitambua na kujihusisha sana na mazingira kwa michezo ya mwili na akili pia.

Anasema hivyo kiwango cha nishati, protini na madini bado vitaendelea kuhitajika mwilini hivyo ni muhimu wazazi kuendelea kuandaa vyakula kwa kuzingatia makundi yote.

Baadhi ya wazazi wanakiri kuzingatia lishe bora kwa watoto wao kama asemavyo Aisha Jamali mama wa watoto watatu lakini mtoto wake wa miaka mitatu anampatia juisi zilizoongezwa sukari.

“Hizi juisi za kutengeneza nampa na hata zile za kopo za kununua pia nampatia kwasababu hakuna shida, niliwahi kukatazwa kumpa vyakula vya mafuta ila mara chache huwa nampa sio kila siku,” anasema.

Mkazi wa Arusha, Rose Kisioki anasema mtoto wake wa miaka minne humpatia vyakula vyenye mafuta japo humfanyisha mazoezi kila mara.


Nini kiepukwe

Husna anashauri si salama kumpa mtoto vyakula vilivyoandaliwa tayari (fastfood) ambayo huwa na kiwango kidogo cha virutubishi.

“Mlishe chakula kiasi kidogo mara kwa mara, pia mazingira kumlishia mtoto yawe rafiki kwa yeye kula na kukifurahia chakula,” anasisitiza.

Akisisitiza suala la lishe kwa mtoto, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe Wizara ya Afya, Neema Joshua anasema vinywaji vilivyoongezwa sukari haviruhusiwi kupewa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na vijana balehe chini ya miaka 19 kwasbabu za kiafya.

“Sio vinywaji vya viwandani peke yake hata vinywaji vilivyotengezwa na kuongezwa sukari mtoto hapaswi kupewa, kama mtoto ni mdogo apewe tunda ale, tunda libondwe aweze kula baada ya kufikisha miezi sita, hakuna chakula ambacho hakiruhusiwi kuliwa na mtoto ila ni kwa kiasi gani anakula,” anaeleza.

Neema anasisitiza, chakula chenye mafuta mengi si sahihi kwani ni hatari kiafya kwa mtoto.

Kuhusu uzito uliopitiliza, anasema unachangiwa na vyakula anavyokula mtoto na kutojishughulisha kwa mtoto.

“Mtoto chini ya miaka mitano anapopelekwa kliniki wanapimwa uzito na pale mtaalamu akibaini uzito wa mtoto unaongezeka atahoji aina ya vyakula anavyompa mtoto na hapo anaweza kumshauri apunguze aina ya vyakula, lakini mtoto anaweza kunenepa sana kutokana na kutoshughulisha mwili,”anasema.

Neema anasema mtoto mdogo anapocheza au kubiringita kitandani ndiko nafasi ya kushughulisha mwili ili nishati iliyopo mwilini lakini anapofungiwa mgongoni muda wote hapati nafasi ya kuushughulisha mwili.

Mbogamboga, matunda na vyakula vyenye asili ya wanyama ambavyo haviwafanyi watoto kunenepeana na mtoto anapokuwa kwenye hali hiyo si sahihi kupokea ushauri wa haraka wa kumpunguzia chakula kwa lengo la kumrejesha katika hali ya kawaida.

“Kwa watoto chini ya miaka sita huyo ambaye ni mnene hiyo haina madhara kadiri muda utakavyokwenda lazima atapungua tu hakuna ushauri wa kumwambia mama punguza kumnyonyesha,

Niwashauri wazazi ukimuona mtoto wako amenenepeana hadi anakuwa na kitambi unamuweka kwenye hatari ya kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza mapema sana,” anasema Neema.


Yanayotokea usipozingatia ulaji sahihi kwa mtoto

Dk Ernest Winchislaus wa Idara ya Mafunzo na utafiti na Magonjwa ya ndani. Hospital ya Kanda ya Rufaa Mbeya anasema mara nyingi daktari wa watoto hukutana na watoto wanaoonekana kuumwa kwa muda mrefu pasipo sababu ya ungonjwa huo.

Anaeleza kuwa uchunguzi unapofanyika kufuatilia historia ya ulaji wa mtoto huthibitika hayo ni kutokana na lishe duni.

“Lishe bora ni muhimu sana katika ukuaji na maendeleo ya watoto. Ulaji usio sahihi una madhara makubwa kwa afya ya mtoto na kusababisha magonjwa mbalimbali,” anasema.

Tatizo ambalo linaweza kujitokeza kwa mtoto ni utapiamlo, Dk Winchislaus anasema hali hiyo hujitokeza pale ambapo watoto hawapati virutubishi muhimu wanavyohitaji kwa ukuaji wao kwa viwango sahihi.

Anataja aina mbili za utapiamlo yaani utapiamlo wa upungufu na utapiamlo wa kunona yaani kiribatumbo.

Anaeleza Shirika la afya duniani linakadiria nusu ya vifo kwa watoto chini ya miaka mitano husababishwa na utapiamlo, mara nyingi huwakumba watoto walio katika nchi maskini na zinazoendelea ikiwemo Tanzania,

“Utapiamlo huu husababishwa na kutopata chakula cha kutosha na chenye virutubisho vya kutosha kukidhi mahitaji ya mwili na kwa wengi hufahamika kama kwashakoo na marasmus,” anaeleza.

Mtaalamu huyo anasema kwa Tanzania asilimia 34 ya watoto chini ya miaka mitano wana utapiamlo na udumavu.

Anasema utapiamlo wa udumavu husababisha mwili wa mtoto kuwa dhaifu hivyo kupata madhara kama udumavu na maendeleo duni ya ukuaji wa kimwili na kiakili, upungufu wa mara kwa mara wa damu, kinga dhaifu ya mwili hivyo hushambuliwa na magonjwa na matatizo ya kisaikolojia.

Matatizo hayo ni kama vile msongo wa mawazo na matatizo ya kujifunza hivyo hukosa furaha wakati mwingi lakini pia huwa na maendeleo hafifu shuleni.

“Ulaji duni wa virutubisho unaathiri afya ya ngozi na nywele za watoto, wanakumbwa na matatizo kama vile ngozi kavu, vidonda vya mara kwa mara, nywele zisizo na afya, misuli na mifupa dhaifu matege,” anasema

Dk Winchislaus anasema madhara ya utapiamlo yanaonekana mpaka hata pale mtoto anapokuwa mtu mzima hasa kwa changamoto za saikolojia na akili.

Kutokana na kukua kwa uchumi, maendeleo ya kiteknolojia na ongezeko la matumizi ya vyakula vyenye sukari nyingi kumekuwa na ongezeko kubwa la watoto wanaougua kiribatumbo.

Hali hii hujitokeza pale ambapo mtu anakula vyakula vyenye kalori nyingi kuliko mwili unavyohitaji na hivyo kusababisha uzito kupindukia.

Dk Winchslaus anasema tafiti zinaonyesha, Tanzania asilimia 15 ya watoto wa shule kwasasa wanaugua kiribatumbo ambayo husababisha kupata shinikizo la damu, pumu, matatizo ya usingizi na maendeleo hafifu ya kimasomo.