Dar es Salaam. Mtindo wa maisha wenye afya unaozingatia lishe bora, mazoezi na kuepuka vitu vinavyoweza kuwa na madhara ni miongoni mwa mambo muhimu anatakiwa kufuata mjamzito ili ujauzito uendelee vizuri.
Mambo hayo kama yakifuatwa yatamsaidia mama na mtoto kuepuka hatari zisizo za lazima.
Inaelezwa mtindo wa maisha ni mojawapo ya sababu zinazochangia hatari kubwa kwa wajawazito na hata kusababisha vifo vya mama au mtoto.
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Isaya Mhando anaeleza mtindo wa maisha unaweza kuwa na athari kwa mama kuanzia anapobeba mimba hadi wiki 42 baada ya kujifungua.
“Uzito kupita kiasi unamuweka mama hatarini ingawa si moja kwa moja. Wakati wa kujifungua kunakuwa na mwingiliano wa mafuta na misuli katika mji wa mimba na hii pia huchangia wengi kutopona kwa haraka hasa wanapofanyiwa upasuaji,” alisema
Alisema: “Wanawake wengi wanene sana ukifanya uchunguzi mara nyingi mimba zao huharibika zikiwa changa. Lakini kisukari na shinikizo la damu vinachangia vifo wakati wa kujifungua ijapokuwa si moja kwa moja.”
Anasema mjamzito kutofanya mazoezi, kunywa pombe kupita kiasi na kuvuta sigara ambayo ina kemikali zaidi ya 200 kunaweza kuathiri mishipa ya damu ya mama na ukuaji wa mtoto tumboni.
“Shinikizo la damu na kifafa cha mimba, husababisha kifo kwa kiwango kikubwa. Mama anaweza kuwa na shinikizo la damu kwenye familia akabeba mimba, presha inaweza kuwa juu ikasababisha athari kwenye ubongo, mishipa ya damu ikapasuka damu ikaingia kwenye ubongo. Inayopoteza kinamama wengi ni ile inayosababisha kifafa cha mimba,” alisema.
Anaeleza magonjwa mengine yanayomuweka mama hatarini kuwa ni malaria, upungufu wa damu, maambukizi ya virusi vya Ukimwi, ugonjwa wa moyo na kisukari ambacho kimegawanyika maeneo mawili, ya kurithi na itokanayo na ujauzito.
Dk Mhando anasema mazingira ya kijamii na kiuchumi yanaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa msongo wa mawazo kwa mama na ikaleta athari kwa ujauzito kuharibika au kifafa cha mimba.
Akizungumzia kuhusu changamoto za uzazi, Nelly Kihongosi mkazi wa Iringa anasema: “Nilipokuwa najifungua nesi alinishambulia kwa maneno, ilinipa msongo wa mawazo na hasira. Nilipopimwa presha ikawa inapanda wakasema inabidi nifanyiwe upasuaji, lakini wakati huohuo mtaalamu wa dawa za usingizi hakuwepo ilibidi nisubiri, nilitoka salama sikuamini.”
Nelly alisema lugha hizo hazisaidii wagonjwa bali kuwapa msongo wa mawazo na hasira, hivyo kuchangia kupata presha.
“Mtoto wangu wa kwanza nilijifungulia Hospitali ya Rufaa ya Amana mwaka 2009 nakumbuka nilipigwa vibao vya mapaja, ile hali ilisababisha mpaka mtoto anatoka presha ilikuwa juu nilishindwa kunyonyesha siku mbili mpaka nilipokaa sawa,” anasema Rahma Juma, mkazi wa Mbezi Dar es Salaam.
Takwimu zinaonyesha takribani kinamama 2,200 hufariki dunia nchini kila mwaka wakijifungua.
Vifo 104 vya wajawazito vitokanavyo na uzazi katika kila vizazi hai 100,000 hutokea nchini, huku watoto takribani milioni mbili huzaliwa kila mwaka ikiwa sawa na kusema wanawake 2,200 hufariki dunia kila mwaka wakijifungua.
Licha ya ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) ya mwaka 2022 kuonyesha vifo hivyo 104 vimepungua kwa asilimia 80 kutoka 556 mwaka 2016/2017, hata hivyo, bado jamii ina wasiwasi kuhusu kupata watoto.
Mhadhiri wa chuo cha Sayansi na Afya Shirikishi (Muhas) Dk Ali Said anasema:
“Idadi ya 104 bado ni kubwa, kama tumewahi kushuhudia ajali zinazotokea Coster (gari aina ya Toyota) moja ikiua abiria wote 34 ni msiba mkubwa kwa Taifa, lakini hii hatuoni kwa sababu mmoja atafariki dunia Songea, mwingine Kigoma na maeneo mengine, ni janga kubwa lisiloonekana,”
Rais Mteule wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko alisema: “Vifo vitokanavyo na uzazi idadi ya 104 bado ni kubwa ni lazima tunakoenda tupange kuwa na idadi ya vifo vinne katika kila vizazi hai 100,000, tutakuwa tumefikia malengo.”
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinakadiria kuwa kila baada ya dakika mbili, kuna mwanamke anafariki akijifungua kwa matatizo yanayodhibitika na kutibika, huku asilimia 70 ya vifo vyote vitokanavyo na uzazi hutokea nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo.
Mbali ya mtindo wa maisha, mambo mengine yanayotajwa kuchangia vifo vitokanavyo na uzazi nchini ni mama kucheleweshwa kufika kituo cha afya, miundombinu, maadili na ujuzi wa watoa huduma.
Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi, Elias Kweyamba anasema mama kwenda hospitali kwa kuchelewa ni miongoni mwa sababu zinazoua wajawazito wengi.
“Pia anaweza kupata changamoto ya miundombinu ya kumfikisha hospitalini ikiwemo usafiri, mawasiliano ya simu, fedha za maandalizi na mahitaji yote baada ya kuamua kwenda hospitali,” anasema na kuongeza:
“Wahudumu wa afya kuchelewa kuchukua hatua za kimatibabu. Uwepo wa watumishi vituoni, vitendea kazi, dawa, vitendanishi na miundombinu ya hospitali, vyote vikiwa sawa hakuna kifo cha mama na mtoto.”
Takwimu za Wizara ya Afya za mwaka 2022 zinaonyesha zaidi ya asilimia 80 ya wajawazito nchini wanajifungulia hospitali.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Wizara ya Afya, Profesa Paschal Rugajjo alisema kwa sasa kuna madaktari bingwa, vifaa na vifaatiba vya kisasa na wanahakikisha kila hospitali inaona wagonjwa kulingana na uwezo wake na matarajio yao.
Mkurugenzi Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto, Dk Ahmed Makuwani, alisema wamepunguza vifo vya uzazi kwa asilimia kubwa na juhudi zaidi zinawekwa ili kufikia malengo.
“Tumepunguza vifo kutoka 556 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2015 sawa na kinamama 11,000 mpaka 104 kwa kila vizazi hai 100,000 sawa na kinamama 2,200” alisema
Sababu mama kufariki wakati akijifungua
Dk Kweyamba alisema kuna mazingira mengi yanayochangia vifo vya kina mama wakati wa kujifungua, sababu zingine zikihusisha ujuzi wa wataalamu na zingine za kibaolojia.
Alisema iwapo mama atapata maambukizi ya bakteria baada ya kujifungua, wanaposambaa mwilini huingia kwenye damu, na hilo linaweza kusababisha kifo.
Anasema mama kuchelewa kupata huduma kituoni ni sababu kuu inayochangia vifo kwani wapo ambao hawawezi kwenda hospitali bila idhini ya mume, hana fedha, hana mtu wa kumpeleka, vyombo vya usafiri na changamoto ya miundombinu.
Pia anaweza kufika kituoni kukawa hakuna vifaa vya matibabu, damu na vitu kama hivyo au vipo lakini watoa huduma ni wachache wanaweza kufanya mama achelewe kupata huduma kwa wakati.
Dk Kweyamba anasema vifaa vinaweza kuwapo na watoa huduma, lakini hawana ujuzi wa kutosha kutokana na kada zao, hivyo kuchangia vifo.
“Anatakiwa kufanyiwa upasuaji lakini wanaotoa huduma si madaktari wa upasuaji, au daktari yupo mtu wa dawa za usingizi hayupo kwa hiyo mama atachelewa au atatakiwa kupewa rufaa,” alisema Dk Kweyamba.
Anasema inawezekana pia watoa huduma wapo wana ujuzi, wanatosha na vifaa vipo lakini maadili yao ya kumhudumia mgonjwa si mazuri, au wapo wana ujuzi wana maadili lakini kuna ujuzi wanakosa, hawajui kumtibu mgonjwa anayetokwa damu nyingi au mama mwenye kifafa cha mimba.
“Kifo cha mama mjamzito sababu hazifanani. Lazima mazingira ni tofauti na sababu tofauti jinsi ya kumhudumia mama anayetoka damu na mwenye kifafa cha mimba ni tofauti na inaweza kuhitaji wataalamu tofauti,” anasema.