AJIRA NA KAZI: Kinachowashinda wengi kwenye usaili wa ajira
Muktasari:
Wengi tunaposhindwa, tumekuwa wepesi wa kutafuta sababu na visingizio, badala ya kutenga muda na kutafakari sababu ya kushindwa ili tutafute ufumbuzi.
Kuna kauli ya busara isemayo; kama hujajiandaa kushinda, ni wazi umejiandaa kushindwa.
Wengi tunaposhindwa, tumekuwa wepesi wa kutafuta sababu na visingizio, badala ya kutenga muda na kutafakari sababu ya kushindwa ili tutafute ufumbuzi.
Mtazamo huu unawagusa watu wengi wanaotafuta ajira na kujikuta wakitoka kapa.
Kuna sababu nyingi zinazowafanya watahiniwa wengi kushindwa kwenye usaili
Makala haya yatajadili sababu hizo na kupendekeza njia mwafaka za kukabili tatizo hili linalowakumba wahitimu wengi nchini.
Tambua kuwa ili uitwe kwenye usaili, kutatokana na jinsi mwajiri alivyoridhika na wasifu wako ambao uliuwasilisha baada ya kuona tangazo la nafasi ya kazi.
Wengi hawajui kuwa usaili ni kama vita, unapokwenda kwenye usaili unakwenda kupambana na watu wengine wenye hamu ya kuipata kazi unayoiomba.
Wakati wa usaili, waajiri huangalia vitu vingi kutoka kwa waajiriwa. Vitu hivi ni kama uwezo wa katika kuwasiliana, uelewa wa maswali na namna unavyoweza kupanga majibu yako, ujasiri na zaidi namna unavyoweza kushawishi wanaokuhoji, ili waamini kuwa wewe ni mtu sahihi kwa nafasi ya kazi uliyoomba.
Kuchelewa kufika kwenye usaili
Watahiniwa wengi huchukulia usaili kama ni jambo la kawaida, hawajui kuwa usaili unapaswa kupewa umuhimu wa hali ya juu.
Unawezaje kuchelewa miadi tena ikiwa siku ya kwanza? Unafikiri mwajiri atawaza nini juu yako? Picha atakayopata ni kuwa hata akikupa kazi bado utakuwa mchelewaji na hautafanya kazi zake kwa wakati.
Kama una nafasi, jitahidi siku mbili au moja kabla ya usaili, utembelee eneo ambalo usaili utafanyika ili ufahamu mazingira na pia kutazama changamoto zozote zinazoweza kujitokeza siku husika.
Ni muhimu kuwahi eneo la usaili angalau kwa 30 ama 15 kabla ya muda, hii itakusaidia kupata nafasi ya kupumzika na kujiandaa vema.
Kutofanya utafiti
Mwanzoni tumesema huwezi kupanga safari kama hujui unataka kwenda wapi. Umeomba kazi, unapigiwa simu ya kuitwa kwenye usaili, kinachofata ni wewe kujiandaa na usaili.
Maandalizi hayo lazima yajumuishe kufanya utafiti hata kama ni kwa kiasi tu juu ya kampuni uliyoomba kazi. Utafiti wako unaweza kukusaidia kufahamu kuhusu huduma na bidhaa wanazozalisha, historia fupi ya kampuni na baadhi ya mambo muhimu kama maono na dira ya kampuni.
Kufahamu haya yatakusaidia kujibu swali ambalo mara nyingi waomba kazi wamekuwa wanaulizwa na kubaki wakibabaika katika kutoa majibu. Swali hili huuliza: Kwa nini unataka kufanya kazi nasi?
Kutoelewa kazi unayoomba
Wakati wote unapoitwa kwenye usaili hakikisha umesoma na kulielewa tangazo la nafasi ya kazi uliyoomba. Waajiri wanaamini kwamba uliona tangazo, ukajitathmini na kuona unakidhi vigezo na unafaa kuifanya hiyo kazi.
Kabla ya kwenda kwenye usaili, hakikisha umefanya marejeo ya kutosha juu ya nafasi uliyoomba kisha husianisha na uzoefu wako wa sasa, hapo utakuwa na maarifa ya kutosha yatakayokuwezesha kuelezea majukumu yako. Pia, hilo litawashawishi wanaokuhoji wajue wewe ni mtu sahihi kwa nafasi hiyo.
Kutoa majibu yasiyojitosheleza
Hili ni tatizo linalowasumbua waombaji wengi katika usaili, kujibu maswali kwa kifupi kupita kiasi kitu ambacho huwafanya kushindwa kukidhi haja ya wanachotaraji kukisikia wahusika.
Unapaswa kujipambanua kwa kufafanua hoja mbalimbali unazoeleza ikiwezekana kwa kuambatanisha na mfano mmoja ambao umewahi kukutokea ama kuufanya. Kwa kufanya hivi, itakusaidia kujenga picha halisi ya namna unavyoweza kutekeleza majukumu yako.
Kutoonyesha shauku ya kutaka kufanya kazi
Mtihani wowote huleta hofu lakini kwa kawaida unapaswa kutumia sekunde nane tu kuikabili hofu hiyo na kurudi katika hali ya kawaida itakayoweza kukupa ujasiri wa kuweza kukabiliana na jopo la wajumbe wa usaili.
Waulizaji katika usaili wangependa kukuona unaingia kwenye chumba cha usaili ukiwa unatabasamu na ukionyesha uchangamfu. Zaidi watapenda kuona namna utakavyokuwa ukiweka msisitizo wa namna unavyoweza kufanya kazi na kufikia malengo ukitaja baadhi ya mbinu au njia unazoweza kuzitumia.
Kumuongelea vibaya kiongozi wako ama kampuni unayotoka
Kwenye usaili siyo mahali pa mtu kuelezea hasira, chuki ama kutofurahishwa na kiongozi wako ama kampuni unayotoka. Ukianza kumshutumu mwajiri wako aliyepita, ni wazi jopo la usaili litakutazama kama mtu mlalamishi unayeweza kuwa chanzo cha matatizo kwa wafanyakazi wengine.
Sababu za kushindwa kwenye usaili ziko nyingi, ila kumbuka kuwa makini na muonekano wako wa kimwili, matumizi ya lugha na uchaguzi wa maneno.
Unaposhindwa kwenye usaili, isiwe sababu ya kukata tamaa, unapaswa kutafakari ni wapi ulikosea na nini ufanye kurekebisha hali hiyo. Jiandae ili wakati mwingine uibuke mshindi na kujipatia ajira ya ndoto yako.