Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BEN POL: Kumbe hana mpango wa kutengenea video nje

Ben Paul

Muktasari:

Ben Pol amesema licha ya video zake nyingi kuwa amezifanyia hapa nchini, lakini zimefanikiwa kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni Afrika Kusini na Afrika Mashariki kwa jumla.

Dar es Salaam. Wakati wasanii wengine wakifanya juhudi kuhakikisha wanasafiri kwenda nje ya nchi kwa ajili ya kutengeneza video za nyimbo zao,, mwimbaji mwenye sauti ya kuvutia, Bernard Paul maarufu ‘Ben Pol’ amesema kuwa hana mpango wa kutengeneza video nje ya Tanzania.

Ben Pol amesema licha ya video zake nyingi kuwa amezifanyia hapa nchini, lakini zimefanikiwa kuonyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni Afrika Kusini na Afrika Mashariki kwa jumla.

“Iwapo nitataka kutengeneza video kali ya kimataifa, nitamchukua mwongozaji kutoka nje na kumleta hapa Tanzania,” hivi ndivyo anavyosema.

Anasema kuwa ndani ya Tanzania kuna vivutio vingi anavyoamini akimchukua mwongozaji mwenye vifaa vya kutosha vya kimataifa, ataweza kutengeneza video yenye ubora.

“Unapomchukua mwongozaji kutoka nje na kumleta hapa, bila shaka itampa umakini mkubwa hata yeye mwenyewe, hivyo kufanya mambo makubwa zaidi ya afanyavyo akiwa huko. Hapa kwetu tuna vivutio vingi , maeneo yanayovutia kuna Lushoto, Arusha, Zanzibar, Bagamoyo na mengine yanayoweza kutumika kwa shughuli hii na ukaushangaza ulimwengu,” anasema Ben Pol.

Anasema kuwa bado anahisi anao wajibu wa kuutangaza utalii wa ndani kupitia kazi yake ya muziki.

“Nina wajibu na jukumu la kuwa balozi mzuri nyumbani kwetu. Najua labda watu wa nje wangependa kuona vitu vya nyumbani, ninapojitangaza kwamba mimi ni mwanamuziki kutoka Tanzania, hata kwenye kazi zangu waone mazingira ya nchi yangu,” anasema.

Je, hiyo ni sababu pekee ya uamuzi wake kufanyia kazi zake Bongo?

Ben Pol anaeleza kuwa, anapoona kazi zake zinatumika na kuombwa na watu wengi waishio nje ya nchi, hufarijika kwani inaonyesha inaeleweka.

“Najua kazi yangu inaeleweka, kwa watu wanaoijua lugha ninayoimba, hata kwa wale ambao Kiswahili kwao ni mtihani. Napokea pongezi nyingi, mfano wimbo wa ‘Jikubali’ ni kati ya kazi zangu zilizonipa umaarufu mkubwa nje ya nchi na ndiyo wimbo uliopigwa zaidi nje kuliko kazi zangu zote,” anasema Ben Pol.

Kuhusu usimamizi wa kazi zake Ben Pol anasema kuwa kwa sasa kuna mtu wa karibu anayemsaidia katika suala hilo. Anamtaja kuwa ni mshirika wake wa karibu na wanasaidiana katika kazi za muziki, lakini hana meneja.

Anabainisha kuwa kuna faida kubwa kwa msanii kuwa na usimamizi, lakini akasema bado kuna uhaba wa mameneja wa kazi za wasanii na kwamba kwa walipo sasa, wengi hawana ufahamu wa kazi zao.

“Kuna faida kubwa iwapo msanii atapata meneja mzuri wa kazi zake, lakini tatizo lililopo kwa wengi ni kwamba wanakuwa ni watu wa kusambaza nyimbo za msanii, jambo ambalo hata mimi mwenyewe naweza kulifanya. Mameneja wamekuwa watu wa kula pesa ya msanii, badala ya kumwonyesha njia mbalimbali zitakazotengeneza pesa,” anasema.

Anaeleza kuwa wengi wao wamekuwa wavivu wa kufanya utafiti kuhusu kazi za msanii na njia za kutumika ili kufanya muziki uwe mzuri na kujitangaza zaidi.

Anasema: “Mameneja wengi hawana mitaji, hawajui hata kumtafutia msanii wake kolabo, kila kitu kinafanywa na msanii mwenyewe, hata makubaliano na kampuni mbalimbali. Kwao hata kumtafutia soko msanii wake inakuwa ni shida.”

Nje ya muziki ni mwekezaji

Licha ya kuwa mwanamuziki, Ben Pol ni mjasiriamali. “Nimawekeza zaidi kwenye hisa, hiki ndiyo kitu kinachonifanya kila siku niendelee kutafuta ili niwekeze zaidi, mimi ni mjasiriamali mdogo mdogo,”anabainisha.

Anasema kuwa licha ya kujituma katika muziki, muda mwingi hupendelea kufuatilia mambo mbalimbali ikiwamo kusoma vitabu, taarifa za kijamii na matukio, afya, uchumi, lakini anapendelea zaidi kusoma.

“Napendelea zaidi kusoma vitabu hasa maktaba, ingawa sikumaliza masomo katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), natarajia kurudi kwa mara nyingine mwaka huu ili nimalize miaka yangu miwili,” anasema Ben Pol na kufafanua kwamba aliomba kusitisha masomo kutokana na kusongwa na shughuli za kimuziki, na kueleza kuwa anapenda elimu akitambua umuhimu wake na faida zake kwake na jamii kwa jumla.