Kesi ya madai katika mahakama ya wilaya
Muktasari:
Mamlaka ya mahakama ya wilaya kijiografia huwa yanaishia katika mipaka ambayo wilaya husika inaishia, isipokuwa mamlaka ya mahakama hiyo yanapoongezwa na Jaji Mkuu ili kushughulikia maeneo mengine ambayo yako nje ya wilaya husika.
Mahakama ya wilaya imeanzishwa kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha sheria ya Mahakama Sura ya 11 kama ilivyorejewa mwaka 2002. Mahakama za wilaya zimeanzishwa kwa kusudi la kushughulikia mashauri yaliyopo katika wilaya husika. Kesi husikilizwa na Hakimu wa wilaya au Hakimu Mkazi.
Mamlaka ya mahakama ya wilaya kijiografia huwa yanaishia katika mipaka ambayo wilaya husika inaishia, isipokuwa mamlaka ya mahakama hiyo yanapoongezwa na Jaji Mkuu ili kushughulikia maeneo mengine ambayo yako nje ya wilaya husika.
Mamlaka ya kifedha ya mahakama ya wilaya katika kesi za madai, kwa mali zisizohamishika yanaishia Sh150 milioni na kwa mali inayohamishika ni Sh100 milioni.
Mamlaka yake ya kirufani ni kutoa maelekezo kuwa mahakama ya mwanzo ipokee au isikilize ushahidi wa ziada, kuthibitisha, kugeuza, kusahihisha au kurekebisha kwa namna yoyote ile uamuzi au amri ya mahakama ya mwanzo iliyokatiwa rufaa.
Pia, inaweza kufuta uamuzi wowote wa mahakama ya mwanzo au kutoa amri kuwa kesi isikilizwe upya na mahakama ambayo ilisikiliza kesi. Mamlaka ya marejeo huhusisha kuita jalada na kujiridhisha juu ya usahihi wa mwenendo na uamuzi ya kesi kisheria.
Wakili anaruhusiwa kusimamia kesi katika mahakama ya wilaya. Bado linabaki kuwa ni jukumu la mdai kuwasilisha madai yake ya kesi mahakamani kupitia hati ya madai na kuhakikisha ameandaa ushahidi wa kutosha kupitia mashahidi na vielelezo sahihi ili kuthibitisha ukweli na uzito wa madai yake.
Baada ya mahakama kupokea madai na ushahidi na kusikiliza pia upande wa mdaiwa, itatoa hukumu ambayo itaamua kama madai yako yana msingi na kama una haki ya kulipwa au la. Endapo utakuwa hujaridhika na uamuzi wa Mahakama ya Wilaya unaweza kukata rufaa Mahakama Kuu.
Hakikisha umeandika barua ya maombi ya nakala ya hukumu pamoja na mwenendo wa kesi mara baada ya siku ya hukumu kwa hakimu mfawidhi ili uweze kupatiwa nakala hizo uzitumie kukata rufaa.
Kutokana na miundombinu na teknolojia hafifu ya kimahakama nakala inaweza kuchelewa lakini fanya juhudi kufuatilia na kuipata.
Rufaa yaweza kukatwa ndani ya siku 30 hadi 60 kutegemeana na uamuzi wa mahakama. Hesabu kamili ya siku zilizotolewa na mahakama ili kukata rufaa, unapaswa kuzihesabu kuanzia ile siku ambayo ulipata nakala za mwenendo wa kesi pamoja na hukumu au uamuzi wa mahakama.
Nakala hizo zitakuwa zimesainiwa na hakimu aliyetoa uamuzi huo na kugongwa muhuri wa mahakama ambapo pia tarehe hiyo ya siku uliyopata nakala hizo itajionyesha katika nakala zako za hukumu.
Katika rufaa yako ambayo itakwenda mahakama kuu unatakiwa kuonyesha sababu za msingi kwa namna ambayo mahakama ya wilaya ilikosea kisheria mpaka ikapelekea kutolewa kwa uamuzi wa namna hiyo.
Mahakama Kuu ikishapokea rufaa hiyo itaitisha jalada la kesi hiyo kutoka mahakama ya wilaya na kulipitia na kupitia sababu na maelezo yako ya rufaa na kisha kutoa uamuzi juu ya rufaa hiyo.
Ni muhimu kutafuta mwanasheria wa kukusimamia au kukushauri na kukuandikia nyaraka mbalimbali katika mchakato mzima wa madai yako. Usiogope gharama. Haki inatafutwa na inapobidi hata kwa kuigharamikia ni vyema kufanya hivyo ili kupata haki yako.