Kinywaji cha Togwa kilivyoboreshwa Tarime
Kinywaji cha Togwa.Picha ya mtandao
Muktasari:
Kinywaji hiki kwa kawaida ni baridi kinatengenezwa kwa nafaka au maji ya matunda. Namna ya kutengeneza ni sawa na pombe ya kawaida ila tu haibadiliki kuwa na kilevi.
Togwa maarufu busara ni kinywaji cha asili kinachodumisha kama utamaduni kwa kabila la Wakurya wilayani Tarime na maeneo mengine mkoani Mara kwa ujumla, kinywaji hiki hutumika katika harusi na sherehe mbalimbali.
Kinywaji hiki kwa kawaida ni baridi kinatengenezwa kwa nafaka au maji ya matunda. Namna ya kutengeneza ni sawa na pombe ya kawaida ila tu haibadiliki kuwa na kilevi.
Kinywaji hiki cha togwa ndiyo itakayokuwa pombe ikikaa. Kwa mfano, togwa ya ulanzi ni utomvu kutoka kwenye mianzi baada ya saa kadhaa, hubadilika kuwa pombe hasa baada ya kukaa siku mbili.
Wakurya hupenda kukitumia kinywaji hiki kwa sababu wanasema kinatuliza kiu kwa madai kwamba ni sawa na unapokunywa maji au soda.
Kinywaji hiki licha ya kuwa kinadumishwa tangu vizazi na vizazi, kinazidi kushika kasi na kupendwa zaidi ambapo pia hata makabila mengine yaishio Tarime yanakitumia na mengine wanajua hata kuitengeneza.
Pia, ni kinywaji ambacho hutumiwa na wajawazito wakiamini kuwa unapokunywa togwa inasaidia kusafisha tumbo hivyo mtu akijifungua mtoto atatoka akiwa msafi kabisa.
Kutokana na umuhimu wa kinywaji hicho vimejitokeza vikundi mbalimbali kuamua kukitengeneza ikiwa ni sehemu yao ya ujasiriamali.
Jacob Matiko, ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Jipaze ambacho kina wanachama 15 kikiwa na makazi yake Mtaa wa Msati, Kata ya Nyamisangura wilayani Tarime, anasema kikundi hicho kimeanzisha mradi wa togwa ya asili kwa kuiboresha katika kuihifadhi kwa ubora na kuipaki kwenye chupa za kisasa tofauti na ilivyozoeleka kwa kuuzwa kwa kupima kwenye kikombe au kwenye mifuko.
Anasema togwa hutengenezwa kwa mchanganyiko wa ulezi uliooteshwa maarufu (kimera), unga wa mahindi na unga wa muhogo lakini wameiboresha kwa kutengeneza kwa mchanganyiko wa ulezi (kimera), viazi vitamu, mtama na unga wa muhogo.
“Ujasiriamali ni popote na ubunifu unaozalisha huleta fursa, tuliamua kuja na ubunifu huo baada ya kuona ina soko na tukaongeza ubora wa kuiuza katika chupa za plastiki ambazo ni salama na safi zilizofungwa kisasa sawa na maji ya chupa yanayouzwa madukani,” anasema Matiko.
Anasema kinywaji hicho wanakiweka kwenye chupa maalumu ambazo huziagiza kutoka Kenya, huuza kwa Sh500 na kwa siku wanazalisha chupa 200 na kwa siku wanaweza kupata Sh50,000.
Matiko anasema baadhi ya wananchi hudhani togwa hutengenezwa kwa kemikali licha ya kuwa ni ya asili inakuwa ni jambo geni kwao kwa kuwa tu imeboreshwa kisasa kwa kupakiwa kwenye chupa zilizo na nembo, pia bei ya Sh500 inaonekana ni kubwa huku wengine wakiuza kwa Sh100 zilizopakiwa kwenye mifuko
Matiko anaitaka Serikali kuviwezesha vikundi kutokana na kuwa vingi vimekuwa haviendelei kutokana na mitaji midogo lakini iwapo vikiwezeshwa Tarime itakuwa na viwanda vingi vinavyotokana na wajasiriamali wadogo huku akipongeza Halmashauri ya Mji Tarime kwa kuwapatia mkopo wa Sh3.5 milioni ambao umewawezesha kuongeza uzalishaji.
“Serikali iunge mkono jitihada zetu ukizingatia inahamasisha Tanzania ya viwanda, ni kweli iwapo viwanda vidogo vitaungwa mkono vitakuwa vikubwa tena vyenye ajira nyingi hivyo Tanzania itakua kiuchumi na kupunguza umaskini,” anasema.
Matiko anasema malengo yao ni kuwafikia watu zaidi ya milioni 10 kupitia kinywaji cha togwa, anawashauri wafanyabiashara kukitambua kuwa kina pendwa na watu wengi wakizalishe kwa wingi kama ilivyo soda, huku uboreshaji ukizingatiwa ili kitambulike kitaifa na kwamba malengo yao ni kuwa wawekezaji wakubwa na kuibua miradi mingine
Ghati Mwita, mkazi wa Rebu anasema sasa ni wakati wa ubunifu hivyo wanaTarime wanatakiwa kuondokana na tabia ya kukariri, badala yake wabuni vitu ambavyo vinaweza kuwaingizia kipato.
Mwita anasema togwa hiyo imezingatia usafi tofauti na zingine zinazouzwa katika mazingira yasiyo salama.
“Kuna hizi togwa zinazouzwa kwenye chupa ambazo huokotwa kwenye baa au kumbi za starehe watu wakishakunywa maji wanaokota na kwenda kuziosha, zingine hazioshwi vizuri wala kwa maji yaliyochemshwa hali ambayo ni hatari kwa afya za watumiaji,” anasema Mwita.