Kwa fikra na malengo sahihi utaondoka kwenye umaskini

Adam Ngamange
Muktasari:
Mafanikio ya fedha yatakayokuondoa kwenye umaskini yana siri nyingi ambazo unapaswa kuzifahamu. Nitazizungumzia chache ili upate pa kuanzia unapoelekea kwenye uhuru wa kiuchumi.
Kila afanikiwaye ana siri yake. Hii katika maeneo yote; kazini au kwenye biashara. ni muhimu kwa kila mtu kufahamu namna ya kufika mbali kwenye kile anachokifanya.
Mafanikio ya fedha yatakayokuondoa kwenye umaskini yana siri nyingi ambazo unapaswa kuzifahamu. Nitazizungumzia chache ili upate pa kuanzia unapoelekea kwenye uhuru wa kiuchumi.
Yapo maswali kadhaa ambayo wengi wanajiuliza pasipo majibu yanayojitosheleza. Wapo wanaotamani kuijua siri ya fedha ambayo haifahamiki kwa wengi. Wapo wanaoshindwa kuelewa kwa nini baadhi ya matajiri wanapoteza mali zao zote na kurudi tena kwenye maskini.
Malengo
Hakuna mafanikio yanayopatikana bila kutanguliwa na malengo. Ili kupata mafanikio makubwa maishani ni muhimu ukajua namna ya kujiwekea malengo yatakayokufikisha utakako.
Malengo haya yanapaswa kuwa zaidi ya matokeo ya kazi au shughuli za kila siku. Mkulima anaweza akawa na dhamira ya kuongeza mavuno yake au mfanyakazi akataka kujituma ili aongezewe mshahara. Malengo yanatakiwa yawe makubwa kuliko vitu hivi.
Ili ufike unakotaka kwenda, tumia dakika chache fikiria kwa undani kuhusu unapotaka kuyafikisha maisha yako binafsi. Bila kujali hali uliyonayo, anza kuyaishi maisha yako mapya kwa kufanya mabadiliko muhimu.
Angalia na kuchagua njia bora za kuboresha akili na mwili sambamba na zisizofaa unazotakiwa kubadili. Tathmini aina ya uhusiano unaoutaka na ujuzi unaopenda kujifunza. Chukua hatua zinazostahili kwenye kila unalodhani unapaswa kuachana nalo.
Hii ni moja ya hatua muhimu za kuianza safari ya maisha unayoyatarajia. Hii ni sehemu rahisi na muhimu. Kiini chake ni kujipa changamoto binafsi, kushinda imani potofu na kupandisha shauku ya ndoto yako.
Fikra
Mwanzo wa malengo ni fikra baadaye maneno. Maisha ni mlango wa bahari ambao huruhusu habari, mashauri, matukio, taarifa na maneno yapite. Habari moja huanzisha nyingine. Nawe ni kama dishi, dunia ikiwa satelaiti hivyo unahitaji kuunganishwa ili mambo yatokee.
Binadamu wa kawaida ana uwezo wa kuzalisha fikra 60,000 kwa siku. Wataalamu wanashauri uchukue moja yenye ushawishi mkubwa na uifanyie maandalizi ili iweze tokea.
Tumia karatasi na peni kuunganisha fikra na maneno hayo kuwa malengo kabla hujayaona matokeo unayoyatarajia. Moja ya jambo muhimu unalotakiwa kulizingatia wakati unaelekea kwenye mafanikio ni maneno unayojiambia kila wakati.
Mara nyingi kile tunachojiambia mara kwa mara ndicho kinachoumba maisha yetu pengine hata bila kujua. Maisha yanatokea hivyo. Kila fikra inayotawala maisha yako hutimia. Fikra zako zinaumba maisha yako ya baadaye.
Naamini kuna vitu huwa unajiambia mwenyewe karibu kila siku. Unaweza ukawa unajiambia nitafaulu mtihani wangu wa mwisho, mimi ni maskini, mimi siwezi kufanikiwa, mimi ni mbaya, kilimo hakiwezi kunilipa, mwaka huu ni njaa na mengineyo mengi.
Hayo unayojiambia bila kujali hakuna mtu mwingine anayesikia au unaona hayana maana katika hali ya kawaida ndiyo yanayoumba maisha yako na kukupa matokeo halisi. Akili yako huyasikiliza mawazo yako kwa makini.
Tambua, kila unachojiambia hutokea kwenye maisha yako ya kila siku. Inaweza isiwe leo. Fahamu tu kwamba akili hutekeleza amri zako unazozitoa hivyo ni hekima kuchagua mawazo yanayotawala fikra zako.
Ukijifikirisha kushindwa au afya iliyotetereka itakuwa hivyo. Kama unajiambia mshindi, mafanikio, uwezo wa kushinda majaribu, hayo yote yatatimia hata kwenye mazingira ambayo huyakutegemea na kukamilisha malengo yako.
Maneno yako yana ushwishi mkubwa akilini mwako. Ubongo wako huwa msikivu kwa kiwango cha juu kutekeleza unachoambiwa. Mara moja hutafuta namna ya kufanikisha ulichoambiwa. Ifike mahali utambue nguvu ya maneno unayojiambia kwamba yana uwezo mkubwa wa kukamilisha malengo yako na kubadilisha maisha yako. Hii ni kanuni inayotumiwa na watu wenye shauku ya maendeleo makubwa. Wagunduzi, wanasayansi hata watawala na wanasiasa wenye ushawishi mkubwa.
Badilisha fikra zinazotawala kichwa chako. Ukichunguza maneno uliyojiambia siku nyingi za nyuma utagundua kuwa yametimia kwa namna ambayo hukuitarajia. Kama kuna wakati ulijiambia wewe ni mnyonge na ukaendelea kuwa nao kwa muda mrefu, sina shaka unyonge huo ndiyo ulio nao hadi sasa.
Muda na wakati wote chagua maneno mazuri ya kujinenea mwenyewe kila siku asubuhi, mchana na jioni au usiku. Ukifanya hivyo malengo yako yatafanikiwa tu kama ilivyotokea kwa watu wengine.
Unapokuwa na fikra ya kitu au jambo fulani ni vyema ukatumia muda kulijadili kwa upana wake. Ni bora kukaa masaa matatu kupanga kitu cha kufanya na ukatumia nusu saa kupata faida lukuki kuliko kupanga kwa dakika 10 kitu utakachokitekeleza kwa majuma kadhaa kwa faida ndogo.
Kichwa chako ndiyo maisha yako na matamanio yako hutimizwa na ubongo wako.