Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ziara ya Rais wa Uturuki nchini ni muendelezo wa diplomasia ya uchumi

Rais wa Uturuki Recep Erdogan akikagua gwaride lililoandaliwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakati wa mapokezi rasmi kwenye viwanja vya Ikulu Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Ziara ya Rais wa Uturuki inapaswa kutizamwa na kutafsiriwa sawa na ziara za viongozi wa nchi nyingine kubwa kwani shabaha kuu ni diplomasia ya uchumi na biashara kuliko siasa.

Ujio wa Rais wa 12 wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan nchini ni mojawapo kati ya ziara ya kwaza kwa viongozi wa ngazi hiyo kwa mwaka 2017. Viongozi wa mataifa makubwa waliotembelea Tanzania katika miaka ya hivi karibuni ni pamoja na wa Morocco, India, China na Marekani.

Ziara ya Rais wa Uturuki inapaswa kutizamwa na kutafsiriwa sawa na ziara za viongozi wa nchi nyingine kubwa kwani shabaha kuu ni diplomasia ya uchumi na biashara kuliko siasa.

Vilevile, ziara hizi hazianzii na kuishia Tanzania bali hufanywa katika nchi za kimkakati kwa mataifa haya. Mataifa kama vile China, Marekani, India na mengineyo yana sera zake kuhusu pande mbalimbali za dunia ikiwemo Afrika.

Mataifa hayo yanavutiwa na rasilimali tofauti zilizopo Afrika, Tanzania ikiwamo hivyo kuanda mikakati ya ushirikiano ambao utakuwa na faida kwa pande zote mbili. Ziara hii, kama zilivyokuwa nyingine ina mambo mengi yatakayojadiliwa na kuafikiwa.

Biashara

Historia inaonyesha Tanzania na Uturuki zimekuwa na uhusiano wa biashara kwa muda mrefu. Bidhaa na huduma za aina mbalimbali zimekuwa nguzo ya biashara kati ya nchi hizi mbili.

Tanzania imekuwa ikiuza zaidi malighafi na mazao ya kilimo huku ikinunua bidhaa za viwandani kama vile nguo na vifaa vya ujenzi hivyo kuifanya Uturuki kuwa miongoni mwa wauzaji wakubwa Tanzania nayo kuwa mnunuzi kuliko muuzaji.

Mizania ya biashara inaangukia upande wa Uturiki. Maana yake ni kuwa Tanzania imepeleka fedha nyingi za kigeni Uturuki kuliko ilivyopata kutoka huko. Tanzania ingenufaika zaidi kama ingeuza zaidi kuliko inavyonunua kutoka huko.

Uhusiano wa kiuchumi na kibiashara ungekuwa na manufaa zaidi kama vinavyonunuliwa kutoka Uturuki vingezalishwa nchini baada ya kampuni za huko kuwekeza nchini.

Kampuni za Uturuki zikiwekeza nchini, bidhaa zake zitatengenezewa Tanzania. Kiuchumi, uwekezaji utachukua nafasi ya biashara na ni jambo jema. Hata hivyo, ili hili litokee kuna masharti kadhaa ya uwekezaji yatapaswa kuzingatiwa.

Uwekezaji

Wawekezaji wengi hutafuta mambo makuu matatu; masoko, rasilimali au malighafi na ufanisi. Mazingira rafiki ya kuvutia na wezeshi ya uwekezaji ni muhimu kwa mwekezaji kukata shauri kwa nchi yoyote ikiwamo Tanzania.

Hakuna mwekezaji anayefanya hivyo kwasababu ya kuipenda sana nchi husika bali faida za kiuchumi atakazopata kutoka kwenye miradi atakayoiendesha kwenye taifa analolichagua.

Kwa mwekezaji anayetafuta soko, anachozingatia zaidi ni ukubwa wa soko, ukuaji wake na uwezo wa wananchi kununua bidhaa na huduma atakazozalisha. Kwa anayetafuta ufanisi mambo makuu ni uwezo wa nchi kuwa na vitendea kazi au watu wenye ujuzi wa hali ya juu na mifumo na miundombinu itakayomfanya asipoteze muda katika uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma.

Kwa mwekezaji anayetafuta malighafi mambo makuu ni upatikanaji wake. Yapo mambo mengine muhimu kwa ujumla kama vile miundombinu ya aina tofauti, kutokuwapo kwa urasimu na rushwa, rasilimali watu inayotosha kwa kiasi na ubora.

Wawekezaji walioambatana na Rais wa Uturuki watazigatia mambo haya kabla ya kuamua kuwekeza mitaji yao nchini. Hawa walikutana na wawekezaji na wafanyabiashara wa Tanzania kwa uratibu wa Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Diplomasia ya uchumi

Ujio wa viongozi mbalimbali akiwamo Rais wa Uturuki ni diplomasia ya uchumi. Tunaona viongozi wa wa nchi kubwa na tajiri wakitembelea mataifa kadhaa katika jicho la diplomasia ya kiuchumi.

Hii ni diplomasia ya kutafuta masoko kwa biashara za nchi husika na uwekezaji. Hata pale inapotolewa mikopo na misaada kunaweza kuwa na jicho la kiuchumi nyuma ya pazia.

Ujio wa viongozi hawa unatufundisha kuwa tunapaswa kutoka kwenda katika nchi za kimkakati kwa uchumi wetu kutafuta masoko na kuvutia uwekezaji. Pamoja na ofisi kubwa katika nchi zetu, taasisi za kimkakati katika biashara na uwekezaji lazima zitoke nje kutafuta masoko na kuvutia uwekezaji.

Kusubiri wafanyabiashara na wawekezaji waje pasipo kuwafuata na kuwashawishi kiasi cha kutosha siyo mkakati mzuri kwa afya ya biashara na uchumi wa kimataifa.

Katika muktadha wa balozi za Tanzania nje ya nchi kwa ujumla na mabalozi wapya katika serikali ya awamu ya tano lazima somo la diplomasia ya uchumi lifundishwe na kueleweka vizuri.

Jambo la kufanya

Rais wa Uturuki amekuja Tanzania baada ya viongozi wa Morocco, India, China, Marekani na kwingineko. Hii ni dalili ya Tanzania kuhitajika na nchi hizi. Lakini, lazima Tanzania nayo ijiweke tayari kimkakati kujua inataka nini kutoka kwa mataifa haya makubwa yanayoonyesha kuihitaji na itapata vipi inachohitaji kutoka kwao.

Uturuki, China, Marekani, India na nchi nyinginezo zinataka faida za kiuchumi kutoka Tanzania. Zitashindana kuona nani ataweza kupata faida kubwa zaidi. Kiuchumi, ushindani huu unapaswa kuwa na manufaa kwa Tanzania na ikijiweka kimkakati na kufahamu ukubwa na nafasi yake katika mahusiano haya inapaswa kufaidi. Kinyume chake itavunwa.

Mwandishi ni mbobezi wa uchumi, mshauri elekezi, mtafiti na mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Mzumbe tawi la Dar es Salaam