Zingatia sheria na haki kuvunja mkataba wa kazi
Muktasari:
- Kila upande huwa na picha ya namna mambo yatakavyokuwa mazuri kwa upande wake. Matarajio huwa makubwa.
Mkataba wa ajira husainiwa kwa amani, shukrani huku nyingi nyuso za pande zote mbili zikionyesha furaha ya ukurasa mpya wa maisha.
Kila upande huwa na picha ya namna mambo yatakavyokuwa mazuri kwa upande wake. Matarajio huwa makubwa.
Mwajiri huona namna ofisi yake itakavyofanikiwa kwa kumpata mtu sahihi atakayetimiza majukumu na mfanyakazi huona namna atakavyotumia vizuri fursa zilizopo kuboresha maisha yake.
Changamoto hutokea kazi inapoanza kuonekana chungu. Upande mmoja unapoanza kuonyesha dalili za kutaka kuvunja mkataba wa kazi.
Hata kama mkataba una vipengele vya kuuvunja, mara nyingi hiyo huwa ni habari mbaya kwa pande zote mbili. Mfanyakazi anaweza kuamua kuacha kazi kwa sababu yoyote ile au mwajiri ana changamoto za kiuchumi.
Usipokuwa makini unaweza ukavunja mkataba kiholela na kukugharimu fedha nyingi na usumbufu unaoepukika ukifuata Sheria ya Mikataba ya mwaka 2002, Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004 na kanuni zake.
Sheria inaeleza, mkataba wa kazi unaweza kuvunjika kwa wahusika kufariki, matakwa ya kisheria, mfanyakazi kujiuzuru, makubaliano ya kuvunja mkataba, mfanyakazi kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai au mfanyakazi kushindwa kufanya kazi kwa sababu za kiafya.
Mwajiri anaweza kumfukuza au kumwachisha kazi mfanyakazi kutokana na utovu wa nidhamu, uwezo mdogo wa kufanya kazi au sababu za uendeshaji wa taasisi.
Sheria inamruhusu mfanyakazi kuvunja mkataba wa ajira. Mfanyakazi atapaswa kufuata matakwa ya vipengele vilivyoko katika mkataba wake wa kazi ili aweze kuvunja mkataba wake wa kazi na mwajiri.
Sheria inamtaka mfanyakazi kutoa taarifa ya maandishi mwezi mmoja kabla au kumlipa mwajiri mshahara wake wa mwezi mmoja endapo atatoa taarifa ya saa 24 kuacha kazi.
Ukiacha malipo ya kiinua mgongo, mfanyakazi aliyevunja mkataba ana haki ya kulipwa haki zake zote zinazojumuisha malimbilikizo yoyote ya mshahara, malipo ya likizo, nauli, notisi kama haikutolewa na mengine.
Kwa upande mwingine, mwajiri ana haki ya kuvunja mkataba anapokuwa na sababu msingi, halali na zimezingatia kanuni vinginevyo inaweza kumgharimu fedha na usumbufu ukiwamo wa kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Usivunje mkataba wa kazi kwa jazba, kwa kumkomoa mfanyakazi, kwa maslahi yako binafsi au kwa sababu isiyokubalika kisheria. Itakugharimu sana.
Makosa makuu mawili hufanywa na wengi. Kwanza ni sababu ambayo inapaswa iwe halali na sahihi kisheria kwani kinyume chake mchakato mzima utakuwa batili.
Eneo la pili ambalo huangaliwa sana ni utaratibu uliotumika kuvunja mkataba. Sababu ya kuvunja mkataba wa kazi inaweza kuwa halali kisheria lakini endapo utaratibu uliotumika utakuwa si halali, hilo linatosha kuubatilisha mchakato wa kuvunja mkataba.
Utaratibu ulioainishwa ni pamoja na kutoa notisi kwa mhusika mwezi mmoja kabla au kumlipa mshahara wa mwezi mmoja badala yake.
Mchakato huo unaweza kuhusisha majadiliano ya pande mbili kupata muafaka wa pamoja wa kuvunja mkataba ambayo ni namna bora zaidi.
Ni muhimu kuomba ushauri kwa wataalamu wa sheria kabla ya kuvunja mkataba wa kazi pasipo kujisababishia madhara wala hasara ya namna yoyote.
Mfanyakazi aliyeachishwa kazi isivyo halali ana haki ya kulipwa mishahara yake yote ya muda ambao hakuwepo kazini, mshahara wa mwezi mmoja badala ya notisi, malimbikizo ya likizo, kiinua mgongo, malipo ya usafiri, mafao ya hifadhi ya jamii, cheti cha utumishi, fidia ya mishahara ya miezi 12 na malipo mengineyo yatakayobainishwa.
Ukitumia nguvu, sheria itakuzidi. Mkataba uvunjwe kistaarabu na kiungwana ili hata kesho msalimiane.