Ester zao la shule za kata aliyetamba kwenye fani ya umeme kimataifa

Muktasari:

  • Miaka 29 iliyopita katika Kijiji cha Katangara mkoani Kilimanjaro alizaliwa binti. Hakuna aliyefahamu kwamba siku moja binti huyo wa kwanza katika familia ya watoto watano kutoka kijijini hapo angetambulika kimataifa.

Miaka 29 iliyopita katika Kijiji cha Katangara mkoani Kilimanjaro alizaliwa binti. Hakuna aliyefahamu kwamba siku moja binti huyo wa kwanza katika familia ya watoto watano kutoka kijijini hapo angetambulika kimataifa.

Ester Marcel ameandika historia katika Chuo Kikuu cha Manchester cha Uingereza kwa kuwa mwanafunzi bora wa shahada ya pili ya uzamili katika kozi ya umeme (electrical power system engineering) akipata ufaulu wa juu zaidi ya wenzake 69 kutoka mataifa 10 duniani.

“Wakati nasoma sikuwa na lengo la kupambana niweze kuwa mwanafunzi bora ila siku zote huwa naweka jitihada zangu zote kwa kila ninachokifanya ili baadaye nisije kujuta. Nilipopata barua pepe ya kunipongeza kutoka chuoni kwamba nimeongoza kwenye kozi yetu nilifurahi. Nikasema Mungu ameamua kuniinua,’’ anasema Ester, ambaye kwa sasa ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) akifundisha masomo yanayohusiana na umeme.

Mafanikio kwenye elimu upande wa Ester hayakuanzia Manchester, Uingereza kwani mwaka 2016 alitangazwa pia kuwa mwanafunzi bora akiongoza katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alikokuwa akisoma shahada ya uhandisi wa umeme kwa kupata daraja la juu la GPA ya 4.8.

Hakuwa mkali wa masomo chuoni tu, Ester ana historia ya kufanya vizuri kwenye masomo yake tangu akiwa ngazi za chini. Mwaka 2012 Ester alikuwepo pia kwenye orodha ya wasichana kumi bora katika matokeo ya mtihani wa kidato cha sita baada ya kupata daraja la kwanza la katika mchepuo wa PGM na kuwa sehemu ya wanafunzi walioitwa bungeni kwa ajili ya kupongezwa.

Kwa wale wanaozibeza shule za kata, wamenoa. Licha ya kusoma katika sekondari ya kata bado matokeo yake ya kidato cha nne yalikuwa mazuri kwani, alifanikiwa kupata daraja la kwanza.

“Ukweli ni kwamba sikutoka kwenye familia yenye uwezo kifedha ndiyo maana hata shule nilisoma za kawaida. Nakumbuka shule niliyosoma kidato cha kwanza hadi cha nne ndiyo ilikuwa inaanza hivyo, wanafunzi tulishiriki kwenye shughuli mbalimbali katika kuhakikisha ujenzi unaendelea. Kuchimba vifusi, kubeba mchanga, kuchota maji, kuzoa kokoto ilikuwa sehemu ya maisha yetu. Hili lilinichosha nikamwambia baba anihamishe akanieleza wazi kuwa hana uwezo wa kunipelekea shule ya kulipia, lakini nimwambie kila ninachohitaji ili niweze kusoma,” anasema.

Anasema msimamo wa baba yake ulimfanya atamani kuendelea kusoma kwani kila alichohitaji ikiwemo vitabu alivipata hata kama kwa kuchelewa alihakikisha anatumia vizuri fursa hiyo ili aweze kutimiza ndoto yake ya kuwa mwana anga.

Aliaminishwa kuwa ili awe mwanaanga ni lazima ajue vizuri hesabu na jiografia na alihakikisha anafanya vizuri katika masomo hayo na kufanikiwa kuchaguliwa mchepuo wa PGM katika shule ya ufundi ya Ifunda mkoani Iringa.

Huko nako alisoma kwa jitihada zote akiamini ndoto yake ya kuwa mwana anga ingeenda kutimia. Hata hivyo, alipomaliza kidato cha sita akabadili mawazo na kugeukia fani nyingine ambayo leo imempa mafanikio makubwa.


Abadili fikra kuhusu fani

“Sikuwa na taarifa za kutosha kuhusu nini nifanye niwe mwanaanga, sikupata mtu anayefahamu kwa kina fani hiyo na ukizingatia nimetokea mazingira ya kijijini, nikawaza hivi ni kitu gani kingine naweza kusomea nikienda chuo kikuu ambacho kinaweza kuwa na tija,” anaeleza.

Anaongeza: “Sikupata jibu kwa haraka lakini nikakumbuka baba yangu pale nyumbani huwa anatengeneza vitu vya umeme, sio fundi aliyesomea lakini ana utundu na vitu vya umeme hapo hapo nikapata wazo chuoni nikasomee umeme, nilipoomba kozi ya umeme nilichaguliwa Chuo Kikuu cha Dar es Salam,” anasema.

Huo ndio ukawa mwanzo wa masuala ya umeme kuingia kwenye maisha ya Ester, ambaye kwa sasa anaweza kutambulika kama miongoni mwa wanawake waliobobea katika fani hiyo adimu kusomwa na wanawake.

Baada ya kumaliza shahada ya kwanza na kufaulu vizuri akatakiwa kubaki chuoni kwa ajili ya kufindisha, huku pia akilazimika kujiendeleza ili aweze kuitumikia nafasi hiyo. Ndipo alipoomba ufadhili na kufanikiwa kupata fursa ya kwenda kusoma shahada ya pili nchini Uingereza.

Ili kukamilisha shahada hiyo katika chuo cha Manchester ambacho kimo nafasi ya 27 kwa viwango duniani, Ester alilazimika kufanya utafiti wa namna ya kuzalisha umeme vijijini kwa kutumia nishati mbadala na kuhifadhi umeme huo kwenye betri kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

“Natambua umeme una mchango mkubwa kwenye kila sekta kwa sasa, nikaona kuna vijiji havina nishati hii muhimu. Mfano wangu ulikuwa kijiji cha Ngwamkanga kilichopo Shinyanga nikaangalia kwa hesabu nilizofanya kile kijiji kinaweza kupata umeme kwa kutumia nishati mbadala kama jua.

Nilifanya kila kinachotakiwa kwa nadharia kuhakikisha umeme unaweza kuwaka pale kijijini ikiwa ni pamoja na kufanya hesabu za vifaa kilichobaki sasa ni kupata fedha. Nina uhakika akitokea mfadhili huu mradi ukatekelezwa, kile kijiji kitapata umeme kwa kuwa kila kitu kipo kwenye makaratasi,” anasema.

Anasema ndoto yake siku moja Tanzania iwe na umeme wa uhakika ambao hautakuwa ukitegemea chanzo kimoja kama ilivyokuwa hapo awali ambapo maji ndiyo yalikuwa chanzo tegemezi cha nishati ya umeme nchini.

Mtaalam huyu wa umeme matamanio yake ni kuongeza zaidi ujuzi kwa kufanya shahada ya uzamivu (PHD), lakini anashindwa kutimiza hilo kwa kuwa hana mfadhili wa kumsomesha.

“Natamani nifanye PHD changamoto sijapata ufadhili nimejaribu kuomba sehemu mbalimbali bado sijapata majibu natamani nikaongeze zaidi ujuzi ili pamoja na kufundisha niweze kujikita zaidi kwenye kufanya utafiti kuhusu vyanzo vya asili vya nishati ya umeme,” anaeleza.

Mtazamo wake na masomo ya sayansi

Ester anasema kama nchi tuna uwezo wa kuzalisha wanasayansi, endapo jamii itaacha kuamini kwamba masomo ya sayansi ni magumu.

“Huwa sielewi watu wanaosema sayansi ngumu wanamaanisha nini; unaweza kukuta mtu hajawahi kusoma sayansi halafu anamwambie mwingine sayansi ni ngumu. Hii ni hatari inawakatisha tamaa wenye nia ya kuingia kwenye masomo hayo.

Naamini hakuna ugumu wowote, Serikali iweke nguvu kwenye miundiombinu kwa kuhakikisha shule zina maabara zenye vifaa na walimu ili kumuwezesha mwanafunzi kufanya majaribio. Sayansi inahitaji majaribio nimeshuhudia hilo kule chuoni Uingereza kila mnachosoma mnaingia maabara,” anasema Ester.


Wito wake wa wasichana

Anaumia kuona msichana hasa aliyetokea kijijini ndoto yake ikikatishwa kwa sababu ya vitu vidogo mfano chipsi kuku au simu. Anasema huko ni kuwaumzia mno wazazi.

‘’Ni muhimu kupambania ndoto yako, kuwa mvumilivu kwani siku zote anayevumilia hula mbivu. Wakati utafika utafanya kila unachojisikia kufanya na hakuna atakayekuuliza, lakini kama unasoma basi elekeza mawazo yako kwenye elimu ili uweze kusoma kwa ufanisi na kuweza kupata matokeo yatakayokuwezesha kupata tija,” anasema.