Prime
Sababu za janga la uhaba wa wahadhiri, maprofesa vyuoni

Muktasari:
- Aliyeibua majadala wa uhaba wa wahadhiri hususan maprofesa vyuoni, ni Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Tea Ntala aliyesema kwa sasa nchini kuna maprofesa 93, huku vyuo vilivyopo vikihitaji maprofesa 516.
Dar es Salaam. Serikali kutoajiri wahadhiri kwa muda mrefu na urasimu wa kupandisha madaraja katika vyuo vikuu nchini, vimetajwa kuwa miongoni mwa sababu kuu za uhaba wa wahadhiri na hasa maprofesa katika vyuo hivyo.
Hayo yamebainishwa ikiwa ni siku chache tangu wabunge wachambue undani wa changamoto hiyo,wakati wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia bungeni jijini Dodoma.
Aliyeibua hoja hiyo ambayo hata hivyo si ngeni kwa wadau wa elimu, alikuwa Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Tea Ntala aliyesema kwa sasa nchini kuna maprofesa 93, huku vyuo vilivyopo vikihitaji maprofesa 516.“Kwa sasa nchini tunao maprofesa 93 ambao wakifika miaka 70 tunataka wastaafu huku wengine hamjawajenga. Nashauri tuongeze muda wa miaka ya kustaafu na tuhakikishe tunaongeza wengine kutoka nje ya nchi,” alidai Dk Ntala bila kutaja rejea aliyoitumia kutoa takwimu hizo.
Hata hivyo, taarifa za ilizonazo Mwananchi zinaonyesha mwaka 2022, Tanzania ilikuwa na maprofesa 226, kati yao 163 walikuwa maprofesa washiriki na 63 maprofesa kamili.
Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia.
Wako wapi maprofesa?
Mwananchi linatambua uwepo wa wabunge wanane ambao ni maprofesa, huku pia kukiwa na makatibu wakuu wa wizara wawili ambao ni maprofesa.
Kwa upande wa makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu wa wizara, Mwananchi imebaini kuwapo wa zaidi ya wasomi 10 katika nafasi hiyo wakiwa na shahada ya uzamifu (PhD).
Maprofesa na madaktari pia wamo katika nafasi mbalimbali za utumishi katika vyombo vya kiserikali kama taasisi, mashirika na mamlaka mbalimbali.
Japo ni sehemu ya watumishi wa umma wanaoweza kufanya kazi katika eneo lolote serikalini, kukosekana kwao katika taasisi za kielimu, kunatajwa kama pengo linalochangia kuzorota kwa taaluma vyuoni.
Aidha, ikumbukwe kuwa katika miaka ya karibuni, wasomi wengi vyuoni, wamekacha kufundisha na kukimbilia kwenye nafasi za kisiasa, zinazoelezwa kuwa na maslahi zaidi.
Si kukimbilia tu, utashi wa viongozi wakuu wa Serikali kuwateua wasomi wao katika nafasi mbalimbali kisiasa, unatajwa kama mojawapo ya sababu za kurudisha nyuma taaluma vyuoni.
Uwiano wanafunzi na wahadhiri
Kwa mujibu wa maelezo ya aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Sifuni Mchome, mwalimu mmoja anapaswa kufundisha wanafunzi 20 wa masomo ya sayansi ya jamii, mwalimu mmoja watoto 10 wa fani za ukandarasi na mwalimu mmoja kwa wanafunzi watano wa masomo ya udaktari.
Undani wa tatizo
Akizungumza na Mwananchi, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Elimu ya Juu Tanzania (THTU), Dk Paul Louisuile alisema tatizo la uhaba wa wahadhiri vyuoni lina historia ndefu.
“Inaonyesha miaka ya 1990 kuna kipindi cha miaka 10, Serikali iliacha kuajiri wahadhiri kuanzia ngazi ya chini. Sasa hicho kipindi, kimesababisha uhaba uliopo sasa, kwenu wahadhiri wengi waliokuwepo sasa wamestaafu,” alisema.
Dk Louisuile ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udoma), anasema baada ya vyuo vikuu kuanza kuongezeka, Serikali ikaanza kuajiri wahadhiri kuanzia mwaka 2005, 2006 na kuendelea.
“Kinachofanyika sasa ni kuhakikisha wale walioajiriwa wanawezeshwa. Kwa mfano Udom imefanya kazi kubwa kuwainua wahadhiri, kuanzia kuwa mhadhiri msaidizi asome shahada ya uzamili, halafu shahada ya uzamivu na hao wachapishe machapisho yanayoeleweka.”
Kuhusu urasimu, alisema pia umechangia kupungua kwa maprofesa akisema baadhi ya vyuo vimeweka kanuni na miongozo migumu kutekelezeka kwa kisingizio cha kulinda ubora.
Kwa hiyo unakuta katika huo mchakato ndio zinatungwa sheria, kanuni na miongozo ambayo inakuwa migumu kiasi kwamba watu wanakata tamaa.

Wahitimu kama hawa ili waive barabara, wanapaswa kusomeshwa na wahadhiri wenye sifa wakiwamo maprofesa.
Tumeshaomba sana, ni vita ya kila mara kwenye vikao. Bahati mbaya ni kwamba ni miongoni mwetu. Alisema unakuta mtu ni Makamu Mkuu wa chuo Msaidizi (VC), anaunda jopo linalotengeneza kanuni ngumu.
“Kwa mfano, kuchapisha makala katika majarida ya kimataifa kuna ya kulipia na ambayo sio ya kulipia. Hivyo walisema mtu atakayechapisha makala yake kwenye jarida la kulipa litaondolewa kwenye orodha ya matakwa kwa kupandishwa.
“Wanasema makala za kulipia zinakosa ubora kwa sababu wale wenye jarida wanataka pesa tu, lakini hawazingatii ubora,” anasema.
Anaasema baada ya kuona malalamiko ya wahadhiri walipambana kwenye mabaraza ya wafanyakazi wa vyuo vikuu.
“Ndio tukaanza kupambana tukasema sio majarida yote yanayolipiwa hayana ubora. Kwa hiyo tumepambana miaka miwili na kuna watu wamekata rufaa. Huo ndio mfano wa miongozo ya vyuo vikuu.
“Sasa baada ya kupambana sana, wakasema kwa wanaotaka kulipia iwe dola 500,” anasema.
Kuhusu maprofesa kuteuliwa serikalini, alikiri kwamba kunawapunguza, lakini akasema nao wanastahili kufanya utumishi wa umma.
“Nao ni watumishi wa umma, kwa hiyo kama mtu anakwenda kusaidia serikalini, anakwenda,” anasema
Dk Lousuile anaongeza kutaja ukosefu wa pesa za utafiti kama miongoni mwa mambo yanayokwamisha wengi kuupata uprofesa.
Tafiti nyingi zinahitaji pesa ambayo nchi za kiafrika hazina. Pesa nyingi za kufanyia tafiti zinategemewa kutoka kwa wafadhili,”alisema katika mazungumzo na Mwananchi siku za nyuma.
Anataja pia tambo na majigambo miongoni mwa wahadhiri wenyewe kama kikwazo, akisema wale maprofesa waliofanikiwa huwa wanakuwa na majigambo na hivyo kukosoa machapisho ya wenzao kiasi cha kuwakatisha wengine tamaa au hata kuwachelewesha kupanda ngazi za kitaaluma.
Hoja ya utafiti
Mbunge wa Manyoni Mashariki na aliyewahi kuwa mhadhiri wa elimu ya juu, Dk Pius Chaya anasema kufanya utafiti ili mhadhiri kupanda daraja ni gharama, akisema utafiti mmoja kwa kawaida unahitaji Sh30 milioni hadi Sh 50 milioni, huku utafiti wa kisayansi ukifika hadi Sh1 bilioni.
“Ukiangalia kwa haraka haraka bado Serikali haijawekeza vya kutosha kwenye utafiti na ni eneo tunahitaji kuishauri Serikali. Lakini Serikali imeanza kuongeza bajeti katika suala la utafiti lakini bado tunahitaji kuja na kitu mbadala. Kwa mfano mimi ninashauri tuje na mfuko wa utafiti,” alisema, alipozungumza na gazeti hili mwaka jana.
Alisema mfuko huo, ujumuishe fedha zote za utafiti zikiwemo zinazotokana na ufadhili kutoka maeneo mbalimbali na zitawanywe kwenye vyuo vyote nchini.
“Kuna tatizo jingine hata aina ya tafiti, zinazoandikwa na watu wetu, unakuta daktari anaandika tafiti nyingi lakini hazikubaliki…Kama tutawekeza vizuri kwenye fedha vijana wengi watashawishika kufanya utafiti wenye tija matokeo ya utafiti yatawawezesha kuandika makala,”alisema.
Alisema wapo wenye shahada ya uzamivu kwa miaka 10 lakini hawajawahi kuandika tafiti hata moja, ambayo inaweze kuchapishwa katika majarida ya kimataifa.
Athari sokoni
Mwalimu Adonis Byemelwa anaandika: ‘’Kufuatia wingi wa wanafunzi vyuoni ambapo kwa kila mwaka takribani wanafunzi 100,000 huhitimu masomo ya elimu ya juu kila mwaka, tuna kila sababu ya kuamini kuwa, kwa uhaba huu wa wahadhiri, wanafunzi hawa wanahitimu pasipo na ujuzi wa wa kukidhi vigezo kwenye soko la ajira. ‘’Tujiulize je, wanaweza kushindana kwenye soko la ajira na wenzao kutoka nchi jirani, ambapo huenda tatizo la maprofesa si kubwa kiasi hicho?
‘’Je, kuna mipango endelevu ya kuongeza wahadhiri bila kuathiri ari ya wengi wao kukimbilia fursa zenye maslahi zaidi ya kufundisha?
Majibu ya maswali yangu haya ni rahisi kwa sababu kila mara waajiri wamesikika wakilaumu ujuzi na maarifa ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini kuwa ni wa kutiliwa shaka.
Tumefika hapa kwa sababu ya kukimbilia takwimu za wingi wa wanafunzi vyuoni pasipo mipango madhubuti ya kuhakikisha miundombinu inawiana na idadi ya wanafunzi pamoja na wahadhiri.’’
Sio tatizo la Tanzania pekee
Utafiti uliochapishwa katika jarida la University Wolrd News, Toleo la Afrika, Novemba 2023, umeonyesha nchi za Afrika Mashariki zinahitaji zaidi ya wahadhiri zaidi ya 37,000 ili kukidhi mahitaji ya vyuo vikuu vyake na uwiano unaohitajika kati ya wanafunzi na waalimu (STR).
Utafiti huo, uliofanywa katika vyuo vikuu 133 vya umma na binafsi nchini Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini, pia umebainisha kuwa idadi kubwa ya vyuo vikuu katika nchi hizo havikukidhi uwiano wa jinsia ya kiume na kike kwa wahadhiri, ikilinganishwa na malengo yao ya wafanyakazi wenyewe, au 'sera za kawaida'.
Kutokana na utafiti huo, imeelezwa kuwa vyuo hivyo vinahitaji wafanyakazi wa ziada kufikia takriban 87,000 ili kukidhi ongezeko la usajili wa wanafunzi na malengo ya STR ifikapo mwaka 2030.
Mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wafanyakazi yamejumuishwa katika ripoti iliyoitwa Demographics of African Faculty - Lessons from East Africa Community (DAF-EAC).
Mradi wa DAF-EAC ulifanywa ili kutathmini hali ya wafanyakazi wa elimu ya juu katika eneo hilo, na kufanya utafiti wa msingi juu ya hali ya elimu ya juu, pamoja na kufanya uchambuzi wa mahitaji ya sasa na ya baadaye ya wafanyakazi.

Mhadhiri akiwajibika chuoni. Vyuo vikuu nchini vinaelezwa kuwa na uhaba mkubwa wa wahadhiri kwa ngazi ya maprofesa. Picha na mtandao.
Kulingana na takwimu za mwaka 2017 katika ripoti, Kenya ni nchi iliyo na hali mbaya zaidi, ikihitaji wahadhiri 19,980 zaidi ili kufikia 'sera za kawaida', ikifuatiwa na Tanzania, ambayo ilihitaji wafanyakazi wa kufundisha 10,989 kulingana na takwimu za mwaka 2021.
Kwa upande mwingine, utafiti uliofanywa na Baraza la Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki, (IUCEA), Elimu ya Kusini mwa Jangwa la Sahara (ESSA), Chama cha Vyuo Vikuu vya Afrika, na Wakala wa Marejeleo ya Idadi ya Watu kwa ufadhili kutoka Carnegie Corporation of New York, ilifichua kuwa nchi zenye vyuo vikuu vichache na idadi ndogo ya wanafunzi, kama vile zile za Burundi na Sudan Kusini, zilikuwa na pengo dogo zaidi la STR, zikihitaji walimu 515 na 108 mtawalia kufikia malengo yao.
Tena, Kenya iliongoza katika idadi ya wafanyakazi wa kufundisha wa ziada wanaohitajika ili kukidhi ongezeko la usajili wa wanafunzi na STR ifikapo mwaka 2030, ikihitaji wahadhiri 35,232 kushughulikia idadi kubwa zaidi ya wanafunzi.
Tanzania inafuata kwa karibu, ikihitaji kuajiri wahadhiri 33,291 kukidhi mahitaji na kudumisha uwiano.
Mkakati wa Wizara
Akihitimisha mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema Serikali imewekeza Sh1 trilioni katika Mradi wa Mageuzi ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), unaolenga katika kuboresha miundombinu na nguvu kazi wakiwamo wahadhiri.
Akijibu hoja za wabunge, Waziri Mkenda alisema kwa sasa hivi vyuo vikuu vina uhaba kwa sababu ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi.
“Huko nyuma ajira zilisimamishwa kwa muda mrefu tu, kwa hiyo unakuta wakati mwingine kuna maprofesa wanakaribia kustaafu na wale wanaokaribia kupanda kufikia nafasi ile bado wako mbali sana.
“Kwa hiyo kwa sasa hivi tunaendelea na utaratibu wa kuajiri na sasa hivi tumeanza mazungumzo kuhakikisha kwamba wameruhusiwa kuajiri na pia tunapeleka wahadhiri kwenda kusoma kupitia mradi wa HEET mahali popote hapa nchini,” alisema.
Alibainisha kuwa kwa sasa hivi wahadhiri 519 wameshapata nafasi za kwenda kusoma.
Kuhusu kuchapisha maandiko yao kwenye majarida ili wapande madaraja, Profesa Mkenda alisema wametoa motisha na wameanza na fani za sayansi, elimu tiba na uhandisi.
“Kwa hawa maprofesa tulionao tangu mwanzo walikuwa wanachapisha tu hata bila kuwa na motisha ambayo tumewaanzishia sasa hivi,” alisema.
Hata hivyo amewatahadharisha wahadhiri wanaokimbilia kuchapisha kwenye majarida yasiyo na sifa kwa lengo la kupanda haraka.