Shule za bweni kwa jicho la saikolojia, malezi

Mapema mwaka huu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilipiga marufuku shule za msingi kutoa huduma ya bweni kwa wanafunzi wa madarasa ya awali, darasa la kwanza hadi la nne.

Kwa mujibu wa waraka namba 2 wa 2023 wa Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mutahabwa, ifikapo mwisho wa muhula wa kwanza mwaka huu, shule zote zinapaswa kuwa zimetekeleza agizo hilo. Isipokuwa kwa kibali maalum kitakachotolewa na Kamishna wa Elimu. Uamuzi huo unafanya huduma ya bweni iwe kuanzia darasa la tano na kuendelea.

Akifafanua zaidi kuhusu uamuzi huo wa Serikali, Dk Mutahabwa alieleza kuwa huduma za bweni kwa wanafunzi wenye umri mdogo, ikiwemo wale wa elimu ya awali na darasa la kwanza hadi la nne, huwanyima watoto fursa ya kushikamana na familia na jamii zao, kujenga maadili na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya familia na jamii zao.

“Taarifa mbalimbali zilizopo kutoka kwa wadhibiti ubora wa shule na ufuatiliaji unaofanywa na wizara kwa ujumla, umeonesha kwamba shule nyingi zimetoa kipaumbele katika kuwafanya watoto kupata ufaulu mzuri kwenye mitihani yao ya mwisho. Matokeo yake, kuna juhudi hafifu za kujenga maadili ya wanafunzi na kuwajengea moyo wa kupenda, kuthamini na kufanya kazi,” alisema kwenye waraka huo.

Tanzania sio nchi ya kwanza kupiga marufuku huduma ya shule za bweni kwa watoto. Mwezi Mei 2015, Rwanda ilizipa shule za msingi za bweni nchini humo miaka mitatu kuondoa huduma hizo. Kufikia wakati huo, nchi hiyo ilikuwa na shule zipatazo 34 zilizokuwa zikitoa huduma hiyo.

Aidha, nchi jirani ya Kenya nayo ilipiga marufuku shule hizi kuanzia Januari mwaka 2023. Hoja kuu ni kurudisha wajibu wa malezi kwa familia, kwa kutambua kuwa wazazi wanahitaji kuwa karibu zaidi na watoto ili kuwajengea misingi ya maisha


Maoni ya wadau

Uamuzi huu umepokelewa kwa hisia tofauti na wazazi na wadau wengine, akiwamo Agness Magesa (jina si lake), ofisa wa benki, mama wa mtoto anayesoma shule ya msingi la bweni jijini Dodoma, anayefikiri kuwa shule za bweni kwa watoto wakati mwingine ni jawabu la uhakika kwa familia zenye migogoro inayoweza kumuathiri mtoto.

“Sikuwahi kufikiri ningekuwa mama anayeona bora mtoto aende bweni. Ndugu yangu yamenikuta,”anaeleza.

 Agness ana mgogoro mkubwa na mzazi mwenzake. Ugomvi wao, anasema ulifikia ngazi ya uadui. Haikutosha wao kushindwa kuishi pamoja, lakini pia ikawa vigumu kukubaliana nani abaki na mtoto. “Tulivutana sana. Baadaye tukamua bora mtoto akae bweni. Sio kitu rahisi kwa mama anayejua uchungu wa uzazi. Nilipata shida sana kukubali mtoto wa miaka saba akakae bweni na utoto wote ule. Lakini nikwambie kitu, Sijutii. Ilikuwa afadhali awe kule kuliko kukaa nyumbani akishuhudia vituko vyetu,” anasema Agness na kukosoa vikali uamuzi huo wa Serikali kufuta huduma ya bweni kwa watoto wadogo.

Jeff Kulindwa, baba wa watoto watatu, anafikiri bweni ni mahali salama zaidi kwa watoto wake. “Ukweli sina kabisa muda wa kukaa nyumbani. Kazi zinanibana vibaya sana. Mke wangu naye muda mwingi hayupo nyumbani. Nani anabaki nyumbani kuangalia usalama wa mtoto?” anahoji.

Jeff anakubaliana na Kamishna wa Elimu kuwa wazazi wana wajibu wa kupatikana kwenye maisha ya mtoto, lakini mazingira ya kazi yanaweza kumlazimisha mzazi kumpeleka bweni kwa usalama.

“Hawa kinadada wanatufaa zaidi kwa kazi za ndani sio malezi,” anasema Jeff na kujitolea mfano yeye mwenyewe: “Nimeshawahi kukutana na vitu nisivyopenda vijirudie.”

Ingawa hakuna utafiti rasmi, lakini upo uhusiano wa moja kwa moja kati ya ongezeko kubwa la vitendo vya watoto kudhalilishwa kingono na ongezekano kubwa la wazazi kutopatikana nyumbani.

Ingawa ni rahisi kufikiri shule za kutwa ni salama kwa kuwa zinamuweka mtoto karibu na mzazi wake, hata hivyo, nazo zina changamoto nyingi kiusalama kama anavyoeleza Joseph Marwa, mwalimu wa shule moja ya msingi jijini Dodoma:

“Shule nyingi ziko mbali na hivyo mtoto analazimika kutembea au kusafiri umbali mrefu kwenda na kurudi shuleni. Mtoto huyu asipokuwa na uangalizi wa karibu, anakutana na visa vingapi vinavyotishia ustawi wake kama nguvu kazi ya taifa la kesho?”

Tafiti za usalama wa mtoto zinaonesha kuwa watoto wanapoishi mahali pamoja, uwezekano wa kuwa salama unakuwa mkubwa zaidi kuliko wanapokuwa nyumbani pasipokuwa na uangalizi wa karibu.

Sambamba na changamoto mbalimbali za kifamilia, lipo suala la mtazamo tu kuwa shule ya bweni inakuwa na raslimali zaidi kuliko shule ya kutwa na hivyo kumwezesha mtoto kujifunza vizuri zaidi. Dhana ya bweni inahusishwa na mtoto kupata muda zaidi wa kufuatilia masomo kuliko anaposoma akiwa nyumbani.

Kadhalika, wapo wazazi wanaochukulia bweni kama sehemu ya kuonesha uwezo wao wa kifedha. Kwa mfano, baadhi ya wazazi hususani wale wenye uwezo wa kifedha, hufikiri namna nzuri ya kuonesha ‘kujali elimu ya mtoto’ ni kumpeleka kwenye shule ya gharama kubwa na hata ikibidi shule ya msingi ya bweni ‘ili mtoto akazingatie masomo na apate muda wa kutulia.’

Kwa hiyo, shule za msingi za bweni ni hitaji halisi katika jamii na ni nyenzo inayokidhi mahitaji ya baadhi ya wazazi. Lakini, pamoja na faida hizo, tuna hakika shule za bweni ni mahali salama kwa malezi kwa watoto?Tafiti zinasemaje?

Hakuna tafiti nyingi zilizofanyika hapa nchini kuangazia mazingira ya ujifunzaji na mchango wake katika ukuaji wa kitabia kwa watoto wanaoishi mbali na familia zao. Hata hivyo, tafiti zilizofanyika katika nchi nyingine zinaonesha kuwa kuishi mbali na familia kuna athari nyingi kwa mtoto.

Kwa mujibu wa mwanasaikolojia nguli, John Bowlby, mtoto huzaliwa na hitaji la kuwa karibu na wazazi wake, hulka inayompa mzazi nguvu ya kumwelekeza mtoto jambo na akalielewa. Umbali wowote kati ya mtoto na mzazi katika umri mdogo, unaongeza hatari ya mtoto kutafuta mtu mwingine atakayejifunza kwake.

Kwa kuzingatia hilo, watoto wadogo wanapotumia muda mwingi bweni hupata shida kukabiliana na maisha ya kutengwa na wazazi na wengi hutafsiri kupelekwa bweni kama kutengwa, kutopendwa na kuadhibiwa.

Ingawa watoto, wakati mwingine, wanaweza kuonesha kufurahia kuishi mbali na wazazi wao, Bowlby anaeleza kuwa hizo ni jitihada anazofanya mtoto kuuzoea ukweli asioukubali wa kujitenga na watu anaowahitaji zaidi, ambao ni familia yake. Hali hii ya kupambana kuuzoea ukweli huo huathiri namna anavyojifunza tabia zinazoongoza maisha yake.

Aidha, Mary Ainsworth, mtaalamu wa malezi na makuzi ya mtoto, aligundua kuwa mtoto anayejifunza kuwa mbali na mzazi wake katika umri mdogo, anakuwa katika hatari ya kujenga mtazamo hasi na watu, mtazamo hasi na yeye mwenyewe, hali zinazoweza kuchangia kumfanya awe na tabia na misimamo isiyokubalika katika jamii.

Ipo mifano mingi ya watu wenye historia ya kusoma shule hizi kujitambulisha zaidi na marafiki kuliko familia zao kama anavyoeleza Dk Maria Marandu, mkazi wa Dodoma:

“Wazazi wangu walikuwa na kazi zinazofanya wasitulie nyumbani. Ilibidi kuwapeleka wadogo zangu wawili shule za bweni. Huwezi kuamini wadogo zangu sasa hivi ni watu wazima lakini hawana muunganiko wa karibu na ndugu wa familia. Hatugombani na tunaishi vizuri lakini unaona tu wana connection (uhusiano wa karibu) na marafiki zao kuliko sisi. Kitu mpaka uje ukisikie maana yake huko kwa marafiki zao hawajapata ufumbuzi.”

Umri wa hadi miaka nane unalenga kuimarisha ujenzi wa tunu za maisha zitakazoongoza maamuzi ya mtoto ukubwani. Mtoto anapokosa fursa ya kuwa karibu na wazazi wake katika miaka ya mwanzo ya umri wake, anakuwa kwenye hatari zaidi ya kupotelea kwenye misukumo ya tabia rika zinazoweza kumfundisha tabia zisizokubalika.

Dk Sayuni Philipo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma anafikiri watoto kuishi mbali na wazazi kunafungua milango ya kupata walimu wengine wa maisha tusiowafahamu vyema.

“Mtoto mdogo akiwa mbali na nyumbani anakutana na wenzake waliotoka kwenye familia zenye maadili tofauti. Hana ufahamu mkubwa wa kuchambua kile anachokiona. Bahati mbaya, katika mazingira ya shule zetu, watoto wanakuwa wengi kuliko idadi ya walezi na hivyo inakuwa vigumu walezi kuwasikiliza na kujua kinachoendelea kwenye maisha yao ya faragha,’’ anasema.