Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi za wasichana waliokimbia kuozeshwa, sasa wapo darasani

Muktasari:

  • Kati ya wanafunzi wa kike 28 wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Namnyaki, wanne tu wamesalia kuhitimu kidato cha nne

Iringa. “Hata kama nipo darasani bado sina furaha kwa sababu wadogo zangu wameshaozeshwa na sasa wanaishi kwa waume zao, mmoja ana miaka 14 na mwingine 16.”

Ni sauti ya mwanafunzi wa kike mmoja kati ya watatu waliofanikiwa kutoroka ndoa za utotoni na sasa wapo darasani, mmoja akisoma kidato cha kwanza, mwingine cha pili na watatu cha tatu.

Hakika sio rahisi kusikiliza simulizi zao, japo nililazimika kufanya hivyo walau nikamilishe makala hii.

Kila mmoja ana simulizi ya namna alivyokimbia kuozeshwa baada ya kuhitimu darasa la saba na kufaulu kujiunga kidato cha kwanza na sasa wanapambania ndoto zao za kielimu.

Wanafunzi hawa watatu wanasoma Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Namnyaki, Kijiji cha Image, wilayani Kilolo ikiwa ni kilomita 20 kutoka barabara kuu ya Iringa - Dar es Salaam.

Namnyaki ni shule iliyoanzishwa maalumu kwa ajili ya kuwasaidia wasichana kutoka jamii ya kifugaji kupata haki ya elimu badala ya kuozeshwa.

Kati ya wanafunzi 28, walioanza kidato cha kwanza kwenye shule hiyo miaka minne iliyopita, wanne tu ndio wamefanikiwa kufika kidato cha nne mwaka huu.

Mkurugenzi wa shule hiyo, Mchungaji Paulo Ole Kampashi anasema wanafunzi wengine wameishia njiani kutokana na mila na desturi zinazolazimisha kuolewa kwenye umri mdogo.

Hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi alinukuliwa akisema Tanzania inakuwa miongoni mwa nchi 11 duniani zenye mabibi harusi watoto baada ya makadirio kuonyesha wanawake watatu kati ya 10 waliingia kwenye ndoa wakiwa na umri chini ya miaka 18.

Ukweli ni kwamba kumekuwa na matukio mengi ya watoto kuozeshwa na Ole Kampashi anakiri wazi hali ya ndoa za utotoni hasa kwenye jamii za wafugaji bado ni mbaya.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), Mkoa wa Shinyanga unaongoza kwa kuwa na asilimia 59, Tabora 55 na Mara asilimia 55 kwa ndoa za utotoni.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa asilimia 31 ya wasichana nchini wanaolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 na asilimia tano kabla ya umri wa miaka 15.

Agosti 17, 2022, Gazeti la Mwananchi liliripoti habari ya polisi kuzuia ndoa ya mtoto ambaye alilipiwa ng’ombe 10, mkoani Shinyanga baada ya kupewa taarifa.

Ole Kampashi anasema bado kuna kazi kubwa ya kufanya ili kuwaokoa watoto wa kike wengi ambao ndoto zao za elimu zinapotea kutokana na uwepo wa ndoa za utotoni.

“Wasichana wengi bado wanaolewa chini ya miaka 18, nataka nikuambie sio hawa tu watatu ulioongea nao, watoto wa kike wa jamii za kifugaji wanapitia changamoto,” anasema Ole Kampashi.

“Wakifunga shule na kurudi nyumbani wengine hawaji tena ndio unaona kidato cha nne mwaka huu watoto wamebaki wanne tu, kwao mahari ni bora zaidi kuliko elimu ya mtoto, wasichana ni vitega uchumi hawataki kabisa mtoto wa kike asome.”

Simulizi za wasichana

“Kabla sijaanza mitihani ya darasa la saba, baba aliniita akaniambia ole wangu nifaulu, aliniambia natakiwa niboronge kwa sababu yeye hana pesa ya kunilipia ada,” anaanza kusimulia Anita Lulumay (15) (sio jina halisi).

Ilichukua kati ya dakika mbili hadi tatu kwa msichana huyo kuanza kuzungumza alipoulizwa swali. Muda mwingi alikuwa amejiinamia na wakati mwingine, alifuta machozi.

Anasema siku ya mtihani wake wa darasa la saba, mama yake aliyekuwa mjamzito alipata maumivu, hivyo akakimbizwa hopitali kwa ajili ya kujifungua.

“Bahati mbaya mama yangu alijifungua mapacha walioungana, hivyo alibaki kulekule hospitali, hakurudi nyumbani,” anasimulia Anitha ambaye wakati huo alikuwa na miaka 14.

“Nilipomaliza mitihani baba akauliza tena, mitihani ilikuwaje? Nikasema ilikuwa migumu, akauliza kama nitafaulu nikasema sijui kama nitafaulu,” anasema.

Anasema kwa sababu mama yake alikuwa bado anawauguza wadogo zake, alimuomba pesa baba yake ili aende Hospitali ya Ipamba kumtazama mama yake.

“Baba alinipatia nauli, nikapanda kwenye basi kumbe alikuwa amewatuma vijana waniteke,” aliongea kwa uchungu na kuinama chini akilia.

Anasema hakujua kama baba yake anataka kumuozesha, aliamini kuwa hapendi shule kwa sababu hana ada ya kumlipia.

Anasema siku hiyo alipanda basi na alipofika njiapanda ya Tosamaganga, alishuka na kukuta bajaji imepaki kama inasubiri abiria.

Alikaribishwa kwenye bajaji hiyo akaingia, akijua inaelekea kwa mama yake kwa sababu, walionekana kumfahamu.

“Vijana hawa na bajaj waligeuza kurudi nilikokuwa nimetokea. Walinipeleka kijiji kingine na mimi nilijua ndio hospitali. Nilipofika nikashangaa na kuwauliza, wakaniambia hakuna shida, kumbe baba aliandaa mpango wanitoroshe,” anasema Anitha.

Hapa aliinama tena akilia na safari hii ilichukua muda kidogo mpaka kuzungumza tena.

“Siwezi kusema kilichotokea lakini baada ya wiki moja, nilitafuta mwanya nikampigia simu mama akanitumia nauli nikakimbia. Nilienda nyumbani nikamuuliza baba, kwa nini uliwatuma waniteke? Baba akasema hana ada ya kunisomesha,” anasema Anitha.

Anasema kwa sababu mama yake alikuwa bado hospitali aliamua kwenda kumuona mama yake kwa mara nyingine.

“Bahati mbaya wadogo zangu wakafariki dunia, kwenye msiba nikakutana na Tukuswiga Mwaisumbe, aliponiuliza kama nasoma nilimwambia ukweli, kila kitu ndio akanisaidia, akaniunganisha na hii shule (Shule ya Namnyaki), sasa hivi nipo kidato cha pili,” anasema.

Mwaisumbe anasema aliamua kumchukua msichana huyo ili amsaidie.

“Nilimpeleka shuleni na mpaka sasa amekuwa kama mwanangu, nampa huduma zote kabla hajaenda kwao. Ndoa za utotoni zinakatisha ndoto za wasichana wengi sana,” anasema Mwaisumbe.

Anasema kama asingekutana na msichana huyo hospitali baada ya mama yake kujifungua na watoto kufariki dunia, asingeweza kumpatia msaada. Kinachomliza zaidi Anitha ni namna baba yake anavyomkaripia mama yake kwa sababu anaamini ndiye sababu ya binti huyo kuwa darasani.

“Kila nikiongea na mama anasema baba anamkaripia sana, mama ananiambia baba yako ananikaripia kila siku kwa ajili yako,” anasema Anitha.

Simulizi ya Pendo

“Nilitoroka nyumbani kwa sababu baba, alitaka kuniozesha, aliniambia wazi natakiwa niolewe,” anasema msichana mwingine, Pendo Lukumay (sio jina halisi), kutoka Kilosa, mkoani Morogoro.

Anasema baada ya kumaliza darasa la saba, baba yake alimtafutia mume ili amuoe.

“Yule mwanamume alikuwa mzee, mwanzoni sikujua kama anakuja kunioa lakini baadaye mdogo wangu akanitonya. Nilijifanya sijui, wakalipa mahari,” anasema.

Anasema kabla hajachukuliwa na mumewe huyo, alimpigia simu shangazi yake anayeishi Iringa akimweleza kwamba, anatamani kusoma na hayupo tayari kuolewa.

“Shangazi akasema kama unaweza njoo, nikamwambia mama akasema hana nauli ya kunipatia. Akasema baba yangu ndio kila kitu hata yeye anaogopa,” anasema Pendo.

“Ikabidi nimdanganye baba naumwa, akanipatia hela ya matibabu, hiyo ikawa ndio nauli yangu, kama kesho ndio yule mwanamume anatakiwa aje niolewe, leo mimi nikatoroka,” anasema.

Anasema alipofika kwa shangazi yake, aliomba kusomeshwa lakini kutokana na uwezo mdogo, alimtafutia ufadhili kwenye Shule ya Namnyaki ambako anasoma.

Pendo ambaye yupo kidato cha kwanza, anasema maisha yake ni magumu akiwa shuleni kwa sababu licha ya kusaidiwa kusoma bila malipo, mahitaji imekuwa vigumu kupata.

“Hapa nilipo sina hata uhakika wa taulo za kike, natumia vitambaa huwa nafua na kuanika kule nyuma, najikaza tu walau nitimize ndoto zangu,” anasema.

Simulizi ya Neema

“Kujifelisha ndio mtindo ambao wazazi wengi wa jamii ya Kimasai wanaitumia kuwasihi, waliniambia nijifelishe na baba aliniambia wazi nikifaulu nitajijua,” anasema Neema Kensipi (sio jina halisi).

Neema anasema matokeo yalipotoka alikuwa amefaulu vizuri, jambo lililomuudhi baba yake.

“Akaanza kumkaripia mama kwa nini hajakaa na mimi kunielewesha ili nisifaulu darasa la saba, ndio baba akawa ameongea na mtu anitoroshe nikaolewe.”

Anasema wakati akiendelea kukaa nyumbani baba yake alitaka kumuozesha, lakini bahati nzuri alipata msaada.

“Siku moja nimeenda shambani mama wa jirani akamuuliza mama yangu kwa nini sijaenda shuleni? Mama akamwambia baba hataki nisome, ndio yule mama akaniambia kuna shule inasaidia wasichana walio hatarini kuozeshwa, akaniunganisha na hii shule sasa hivi nipo kidato cha tatu,” anasema Neema ambaye kwao ni Mahenge.

“Kwa hiyo ningebaki ningeozeshwa kwa sababu baba alitaka hivyo, nasoma lakini sipewi mahitaji yoyote yale, nikirudi likizo nahangaika kufanya vibarua nipate hela ili nirudi shulenI.”

Anasema wadogo zake wawili wameshindwa kukimbia na tayari wameshaolewa, mmoja ameolewa Pawaga na mwingine Kijiji cha Malinyi.

“Mdogo wangu mmoja anamiaka 14 na mwingine 16, wanaishi na waume zao,”

Shule ya Namnyaki

Kaimu Mkuu wa shule hiyo, Amasha Chadali anasema wanafunzi wa kike 10 wa shule hiyo ni wale waliofanikiwa kutoroka baada ya kuandaliwa mipango ya ndoa.

“Kidato cha nne msichana mmoja alifanikiwa kukimbia na darasa zima wamebaki wasichana wanne tu,” anasema.

Chadali anasema changamoto kubwa ni namna ya kuwalinda wanafunzi hao wakati wanapokuwa likizo.

“Hata sasa tunapoongea kuna mwanafunzi hajarudi, wengine tukiwapigia simu wazazi kwa ajili ya michango, hasa chakula wanagoma na lengo lao tushindwe ili wakirudi nyumbani waolewe,” anasema.

Mkurugenzi wa shule hiyo, Ole Kampashi anasema shule ina wanafunzi wa kike 85.

Changamoto shuleni

Ole Kampashi anasema moja ya changamoto kubwa shuleni hapo ni mahitaji kwa ajili ya wasichana hao.

Anaomba wafadhili kujitolea kwa ajili ya kusaidia ada za wanafunzi hao.

Mkurugenzi wa Shirika linalojihusisha na masuala ya wafugaji la Paokodeo, Adam Mwarabu anasema tamaa ya mali ndio chanzo cha jamii ya wafugaji kutaka kuozesha watoto wao kwenye umri mdogo.