Tahadhari Serikali ikibariki mtalaa wa Akili Bandia

Ni dunia ya mabadiliko makubwa ya teknolojia. Ni upepo ambao Tanzania haiwezi kuukwepa kama kweli inataka kupiga hatua ya maendeleo.

Mabadiliko hayo kwa sasa yanashuhudia teknolojia ya Akili Bandia (Artificial Intelligence- AI), kama sehemu muhimu ya mapinduzi ya tano ya viwanda ambayo teknolojia inatajwa kutamalaki zaidi.

Serikali ya Tanzania imeona umuhimu wa teknolojia ya Akili Bandia na sasa imetangaza kuwapo kwa mtalaa wake katika mfumo wa elimu nchini.

 Hatua hiyo kwa mujibu wa wadau wa elimu,ni ya kupongezwa wakisema ni mapinduzi makubwa ya kuliingiza Taifa katika matumizi ya teknolojia za kisasa.

Hata hivyo, wadau hao hawakusita kueleza shaka kuhusu upande wa pili wa teknolojia hiyo katika kuandaa wanafunzi bora.


Mtalaa wa Akili Bandia

Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Omar Juma Kipanga,akizungumza jijini Arusha mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema kuingizwa kwa mtalaa wa Akili Bandia, ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo la Rais Samia Suluhu Hassan aliyetaka kuhuishwa kwa mfumo wa elimu ili uendane na mahitaji ya dunia ya sasa.

Anasema katika maboresho ya mtalaa wa elimu uliofanywa hivi karibuni sambamba na mapitio ya sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014, kuanzia mwakani, teknolojia ya Akili Bandia, itaanza kufundishwa kuanzia elimu ya msingi, sekondari na vyuo.

“Kupitia somo ya Teknolojia na Mawasiliano (Tehama), wanafunzi watakuwa wakifundishwa matumizi ya akili bandia katika fani mbalimbali, “anasema.

Anasema ili kufanikisha somo hilo, Serikali inaendelea kuwezesha taasisi za elimu na utafiti nchini,kufanya utafiti na bunifu mbalimbali katika matumizi ya teknolojia za kisasa na kwamba Serikali imetenga kiasi cha Sh9 bilioni kwa ajili ya mchakato huo.

Kipanga aliyasema hayo katika kongamano la kwanza la kimataifa kujadili juu ya matumizi ya akili bandia kwa muktadha wa Afrika, lililoandaliwa na Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknlojia cha Nelson Mandela na Chuo Kikuu cha Dodoma.

Naibu Waziri huyo, anasema Tanzania haiwezi kujitenga na dunia katika matumizi ya akili bandia.

“Dunia ndio imefika huko na sisi lazima twende kwani hatujachelewa,hivyo lazima tujiandae kuwafundisha vijana wetu matumizi ya akili bandia,”anaeleza.


Ijue akili bandia

Akili bandia ni matumizi ya kompyuta, roboti au chombo cha kielekroniki, kinachoweza kufikiri kama binadamu, kujifunza, kutoa mawazo mapya na kufanya kazi mbalimbali kama binaadamu.

Mambo mengine ambayo yanaweza kufanywa na akili bandia ni kuelewa lugha za binaadamu, kushindana kwenye michezo inayohitaji kufikiri, kuendesha gari bila dereva, kutoa tiba na ushauri wa magonjwa kadhaa.


Wadau waguswa

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tecknolojia cha Nelson Mandela,(NM-AIST) Profesa Maulilio Kipanyula, anasema matumizi ya akili bandia(AI), yatasaidia kuboresha uzalishaji wa nafaka, kukuza uchumi na kuboresha maisha ya watu kama ikitumiwa vizuri.

Anasema: ‘’Taasisi za elimu ya juu, kuna makundi yanaendelea kufanya utafiti katika AI ili kuwa na utayari wa nchi kuitumia kwa ajili ya maendeleo,” anasema.

 Anasema wa Chuo cha Nelson Mandela kinaendelea kuwajengea uwezo watalaamu na kuna kituo cha umahiri cha Tehama kinachotoa mafunzo ngazi ya uzamili na uzamivu .

"Kituo hiki ambacho kina wataalamu waliobobea wa ndani na nje ya nchi kitawezesha kuandaliwa watalamu sio kwa Tanzania tu bali Mashariki na duniani ”anasema.

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma Profesa Lughano Kusiluka, anasema Akili Bandia ina faida na hasara ikiwamo watu kupoteza ajira. Hata hivyo, anawasihi Watanzania kutoiogopa teknolojia hiyo.

Anasema changamoto ya akili bandia inajitokeza pale vijana na wasomi wazembe ambao watataka kuitumia teknolojia bila ya wao kutumia pia akili zao za kibaiolojia.

“Ni muhimu sana kuchanganya akili bandia na akili ya kibailojia katika matumizi, kwani kuna maeneo lazima akili ya kibaiolojia itatumika, “anasema.

Anasema kutakuwa na shida katika taasisi za elimu pale wanafunzi wazembe watakapoitumia AI pekee katika maandiko yao, hata hivyo anasema tayari wamejipanga kuwachukulia hatua kali watakabainika ikiwamo kuwafukuza chuo.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Vyuo Vikuu la Nchi za Afrika ya Mashariki (IUCEA), Profesa Gasper Banyankimbona, anasema akili bandia pia inapewa uzito na baraza hilo na kwa sasa vyuo vikuu vya Afrika Mashariki, vimeungana kushirikiana kutoa mafunzo ya Tehama kupitia kituo cha umahiri cha Nelson Mandela.

Profesa Banyankimbona anasema, ni muhimu kuwaandaa wasomi katika nchi za Afrika ya Mashariki katika matumizi ya akili bandia na watahakikisha kupitia Kituo cha Nelson Mandela watakuwa na wataalamu wa kutosha katika teknolojia ya dijitali.

"Lazima Afrika Mashariki tuwe na wataalamu wetu wa kutosha ambao wataweza kufundisha mambo ya kidigitali ikiwamo kuweka mifumo ya Akili Bandia kwa mtazamo wa Kiafrika, "anasema.

 Kwa upande wake, Mkurugenzi mtendaji wa Nukta Afrika, Nuzulack Dausen anasema tasnia zote zinaguswa na AI ikiwemo taaluma ya habari hivyo kuhitaji mafunzo, maboresho ya masuala kadhaa yakiwamo ya kimaadili ili kwenda sambamba na teknolojia hii.

Dausen anasema, Akili Bandia itasaidia sana kurahisisha kazi katika uandishi wa habari, ikiwemo kupata mawazo ya habari, kuhariri, lakini pia kuibadili habari katika lugha mbalimbali.

"Matumizi ya AI yatahitaji sasa vyombo vya habari kuwa na watu wenye uwezo wa kusaidia kutumika AI lakini hakutaondoa umuhimu wa kutumia akili ya binaadamu, "anafafanua.


Akili bandia na ufundishaji

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Dk Jabhera Matogoro, anasema matumizi ya AI katika mifumo ya elimu yatakuwa na manufaa makubwa sana.

Anasema katika shule AI itawezesha kufuatilia uwezo binafsi wa kila mwanafunzi na kuweza kumtengenezea ratiba rahisi ya jinsi ya kusoma na hivyo kuelewa kwa urahisi zaidi.

"Katika shule na vyuo, kuna changamoto ya kuwa na wanafunzi wengi darasani, hivyo sio rahisi wanafunzi wote kuelewa somo mwalimu anapofundisha, " anasema.

Anasema hivyo Akili Bandia itawezesha kutengeneza ratiba rahisi na maswali kwa kila mwanafunzi ili aweze kujifunza kwa kutegemea muda wake na kuelewa na hii itatokana na taarifa binafsi za mwanafunzi ambazo zitakusanywa, "anasema.

Anasema kama mwanafunzi anapenda kitu fulani kama muziki au mchezo, masomo yake yanaweza kuwekwa kupitia kitu anachopenda na hivyo kuwa rahisi kujifunza.

"AI inaweza kutengeza ratiba ya kusoma kupitia muziki, hivyo kama mwanafunzi anapenda muziki ataelewa kiurahisi, "anasema.

Anasema kuhusiana na changamoto ya uhaba wa walimu, AI inaweza kuiondoa kwa kufundisha wanafunzi wengi na wakaelewa zaidi.

Hata hivyo, anasema Akili Bandia lazima ifanye kazi nyuma ya binaadamu ambaye ndiye anayeweza kuandaa programu zote.

"AI inakwenda kuzalisha ajira kwa sababu lazima kuwepo mtu nyuma ya mfumo ambaye ndiye atatengeneza programu na kuweza kutumika kwa kufundisha kwa kila mwanafunzi hivyo ajira mpya zitaongezeka, "anasema.

Dk Matogoro anasema vyuo vikuu vitatoa watalaamu ambao wataweza kujiendeleza hadi nje ya nchi na jinsi ya kuandaa mifumo ya kujifunza.

Anasema wataalamu hao ndio ambao watakuwa nyuma ya AI ili kuwezesha kupatikana kwa maarifa kwa urahisi na kuongeza uelewa.

Hata hivyo, anasema faida hizi kubwa za Akili Bandia katika elimu zitaonekana pale shule, sekondari na vyuo zitakapounganishwa na mitandao ya intaneti na uwepo wa kompyuta au vifaa vya kielekroniki kama simu ili kumwezesha mwanafunzi kusoma.