Halima alivyojiandaa kuelekea Miss World Mei 2023

Miss Tanzania mwaka 2022, Halima Kopwe

Mrembo anayeshikilia taji la Miss Tanzania mwaka 2022, Halima Kopwe anatarajia kwenda kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Miss World Mei mwaka huu, ambayo yatafanyika katika nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu.

Halima, ambaye pia alishawahi kuwa Miss Mtwara, alitwaa taji hilo Mei 20, 2022 akiwabwaga warembo 20 waliokuwa wakiwania taji hilo na kukata tiketi ya kwenda kuiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia. Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, Halima anasema amejiandaa vyema kuiwakilisha Tanzania, kwa kutangaza utalii, utamaduni na fursa nyingine zilizopo nchini.

Halima anafafanua kuhusu mradi huo kwa kusema aliuanzisha kwa kufuata mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan kipindi alipokuwa Makamu wa Rais alipoanzisha kampeni ya ‘Jiongeze tuwavushe salama’ iliyokuwa inatoa elimu kuhusu wajibu wa kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto wachanga.

Anasema pia atatumia mavazi kupata kura zitakazompa ushindi na kutangaza utamaduni wa nchi. “Kwa upande wa mavazi, nataka kuutangaza utamaduni wa Tanzania ambapo nimefikiria kuja na vazi la kanga ambalo ni maarufu Zanzibar, pia vazi linalowakilisha Tanzanite na nina wabunifu wanne ambao kwa pamoja watafanikisha lengo langu,” anasema. Akizungumzia changamoto ambazo ameshawahi kukumbana nazo katika safari yake ya urembo, Halima anasema kuna wakati alikuwa anashindwa kuwa na maamuzi sahihi, kwa kuwa alikuwa ana vitu vingi anataka kufanya.

“Nilikuwa ninawaza nikasome niwe mhandisi, niwe mhudumu wa ndege, mwanamitindo, hivyo nikafikiria na kutafakari nini hatima ya maisha yangu, ndipo nikahakikisha nasimamia kitu kimoja, nikakata shauri kujikita kwenye masuala ya urembo,” anasema.

Hata hivyo, Halima anasema licha ya mafanikio aliyofikia kwenye urembo, hakupata sapoti ya baadhi ya wanafamilia, “Zaidi ya baba, mama na ndugu zangu wawili waliokuwa wanaamini nitafika mbali, wengine walikuwa wanaona kama ninajifurahisha tu.

“Hilo halikunikatisha tamaa, nilianza kuzipigania ndoto zangu ambapo nilijaribu mwaka 2018 nikaishia katika kumi bora, lakini ndani ya mwaka huo nilifanikiwa kuwa miss personality, sikukata tamaa, nikajaribu tena mwaka 2022, hatimaye ndoto ikatimia,” anasema Halima, ambaye anatamani kuona wanamitindo wanalipwa vizuri nchini kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani.


Anazungumziaje siku ya wanawake duniani

Katika kuelekea katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani Machi 8, Halima anasema anapenda kuwaasa wasichana na kina mama, kutokata tamaa kwa jambo wanaloliamini, kwani kila kitu kinawezekana ukiwa na nia. “Kwa sasa hivi wasichana na wanawake tunapewa nafasi na Serikali, hivyo tutumie fursa iliyopo kufanikisha malengo yetu.