Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hofu yatanda fursa lugha ya Kiswahili kutotumika vyema

Julai 7 dunia iliadhimisha siku ya lugha ya Kiswahili. Lugha hii ambayo asili yake ni Pwani ya Afrika Mashariki inaweka rekodi ya kuwa lugha ya kwanza kutoka bara la Afrika kutengewa siku yake duniani.

Watu kutoka kila pembe ya dunia wanaozungumza Kiswahili hii huitumia siku hiyo kujadili mustakabali wa lugha hii ambayo kwa sasa inadiriwa kuwa na wazungumzaji takribani milioni 500 duniani kote.

Kwa Tanzania yalikuwepo majukwaa mbalimbali yaliyotumika kuadhimisha siku hii iliyobebwa na kauli mbiu Kiswahili chetu, umoja wetu ambapo viongozi wa kitaifa, wanazuoni, wanataaluma na watanzania waliungana kuadhimisha siku hii.

Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) iliadhimisha siku hii kwa kufanya mjadala uliowakutanisha wanataaluma kujadili fursa na changamoto zinazoikabili lugha hii ambayo inakua kwa kasi ulimwenguni.


Kilio cha wasomi

Kilio cha wanazuoni ni kwamba kasi hiyo ya ukuaji wa Kiswahili haiendani na namna Watanzania wanavyochangamkia fursa za lugha hiyo ambayo kwa uhalisia inazungumza na watu wengi zaidi Tanzania kuliko nchi nyingine yoyote duniani.

Fursa hizo ni pamoja na kufundisha Kiswahili kwa wageni, kufundisha katika mataifa ambayo taasisi zake za elimu zinafundisha somo la Kiswahili au kozi mbalimbali za Kiswahili, uandaaji wa vitabu na matini mbalimbali za kufundishia na bidhaa nyingine zinazotokana na lugha hiyo adhimu.

Miongoni mwa walioonyesha wasiwasi katika hili ni Profesa Kitila Mkumbo kufuatia kile anachoeleza kuwa mataifa mengine ulimwenguni kuichangamkia lugha hii kitaaluma huku Tanzania ikiwa bado inasua sua katika hatua hiyo.

Kulingana na profesa huyo Kiswahili ni kati ya lugha tatu zenye nafasi kubwa duniani ikiwa sambamba ma Kiingereza na Kifaransa huku katika bara la Afrika ikiongoza kwenye orodha ya lugha zinazochangamkiwa zaidi.

“Kwa muda mrefu Tanzania tumekuwa tukikitumia Kiswahili kama lugha ya mawasiliano, miaka ya hivi karibuni ndio tumeanza kukichangamkia kama lugha ya kitaaluma. Niweke wazi kwamba kuna nchi ambayo yamechangamkia zaidi na tukizubaa zitatuacha mbali ndani ya muda mfupi,”.

“Nitolee mfano Kenya kwenye lugha ya Kiswahili kwa mawasiliano tumewazidi ila kuifanya taaluma wakenya wanakwenda kwa kasi kubwa, DRC na Rwanda nao wanachangamkia kweli kweli lugha hii kitaaluma,”.

Akichangia hoja hiyo Katibu Mtendaji mstaafu wa Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita)Dk Selemani Sewangi anasema kuna fursa nyingi katika lugha ya Kiswahili ambazo hazijachangamkiwa na watanzania na huenda zikawapa manufaa mataifa mengine.

Anasema lugha hiyo nayo inapaswa kwenda sambamba na kasi ya maendeleo ya teknolojia hivyo ni fursa kwa wadau wa Kiswahili kuihusianisha na bidhaa na huduma mbalimbali za teknolojia.

“Siku hizi watu wanasoma machapisho na makala kwenye mitandao, sasa je kuna makala za kutosha za Kiswahili ambazo mwanafunzi anaweza kuzipakua ukweli ni kwamba hazipo. Hakuna makala za kitaaluma kwa sababu lugha hii haijatumika kitaaluma, ingefanyika hivyo maprofesa wakawa wanaandika makala zao huko tungekuwa na vitu vingi vya kusoma.

Kuna fursa pia za kutandaa programu katika mifumo ya kompyuta, kuweka kompyuta katika lugha ya Kiswahili na mambo mengine ya aina hiyo ya tehama kwa kutumia lugha yetu adhimu kama ambavyo imefanyika kwa mataifa mengine kwa kuweka mambo haya kwa lugha zao,”

Dk Sewangi anasema wakati wa idara zetu za isimu, fasihi na kompyuta katika taasisi za elimu ya juu kuwaunganisha wanafunzi wake ili kuwa na muingiliano wa kompyuta na lugha ya Kiswahili.

“Tulipo kwa sasa tumeshaanza kuona uhusiano kati ya walimu au wanafunzi wa idara ya Kiswahili na Kompyuta. Kama wewe ni mwanafunzi wa Kiswahili unatakiwa pia uwe na uelewa mkubwa wa kompyuta kwa sababu siku hizi maarifa mengi yako kwenye teknolojia. Chuo Kikuu anzisheni idara ya isimu kompyuta kuna fursa kubwa upande huo,”.

Dk Sewangi pia anawahamasisha vijana wa Kitanzania kutumia simu kama maktaba za kutafutia maarifa na fursa nyingi zinazopatikana badala ya kuzigeuza kumbi kuwa kumbi za kusogoa na kujifunza maadili na tamaduni zisizo na tija.

Kwa upande wake, Mwalimu wa mstaafu wa Chuo cha Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa (TCDC) Yusta Maganga anasema ipo fursa ya kuwasaidia kuzungumza wanaojifunza lugha ya Kiswahili.

“Watu wengi hawafahamu kwamba vyuo vinavyofundisha Kiswahili duniani huwa wanawatafutia wanafunzi wao wazungumzaji wenza ili wawe wanawafanyia mazoezi ya kuzungumza lugha hiyo. Fursa hizi ni kuzitafuta huko mitandaoni unatuma maombi na wakiona una sifa wanazohitaji basi unaunganishwa na mwanafunzi kazi yako inakuwa kuzungumza naye kwa lugha ya Kiswahili kisha unalipwa, hivyo niwasisitize kuwa fursa zipo nyingi ni kuzitafuta na kuzichangamkia,”anasema Yusra.


Tahadhari

Suala la maadili linaelezwa vyema mwandishi mkongwe wa tamthiliya, Profesa Penina Mlama ambaye anasisitiza kuwa wakati kuna mjadala wa kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa bidhaa ni muhimu kuangalia ni katika mazingira gani na viwango gani biashara hiyo itafanyika.

Anasema katika kipindi hiki ambacho ubepari umechukua hatamu ni muhimu kujua wanaochukua dhamana ya kukitangaza au kukifanya Kiswahili kuwa bidhaa wana umahiri gani wa lugha hiyo ili dunia ipate kilicho bora.

“Hatuwezi kukataa kwamba sasa hivi tunaishi kwenye matabaka, labda tujiulize hawa vijana wanaosoma shule za mchepuo wa Kiingereza ni sanaa gani wanaziangalia. Wale wamshajijengea utamaduni wao kutokana na elimu wanayoipata, sasa tunaposema kuna fursa za kupeleka Kiswahili ughaibuni tujiulize tunapeleka Kiswahili gani?

“Lugha au sanaa yoyote haiishi hewani, inajikita katika misingi ya jamii na inajengwa hasa kiitikadi. Huko tulikotoka sanaa zilikuwa na uhusiano mkubwa na maendeleo ya nchi yetu. Huku tunakokwenda ni muhimu tunapozungumza kuhusu Kiswahili au sanaa zilizo katika Kiswahili kama zina fursa nje nafikiri ni muhimu tuangalie hizi sanaa au hii lugha yetu imejikita kwenye jamii ya aina gani,”

Mama huyu ambaye alijizolea umaarufu kupitia tamthiliya yake ya Nguzo mama anasema kwa sasa ni vyema vijana wakatumia fursa ya lugha ya Kiswahili na sanaa kuzungumzia changamoto zilizopo kwenye jamii na utatuzi wake.

“Jamii yetu ina matatizo mengi ikiwemo ukatili na unyanyasaji wa kijinsia hii ni fursa kwa vijana kutumia lugha, sanaa na ubunifu wao kujaribu kupambana na changamoto zinazoikabili taifa letu. Ni vyema tujenge mtazamo wa kuchanganua zaidi badala ya kuwa machawa uchochoro ambao vijana wengi wanaukimbilia kwa sasa kama njia ya mkato ya kupata maisha.”

Kwa upande wake mbobezi wa isimu Profesa Yohana Msanjila anaweka msisitizo wa lugha ya Kiswahili kutumika vyema ili kuimarisha mapatano na amani akikemea matumizi mabaya ya lugha yanayofanywa na kizazi cha sasa.

“Lugha tunayoitumia Kiswahili lazima ilete mapatano na amani, sasa hivi vijana wetu lugha zao ni za mkato hawawezi kutofautisha wanaongea na nani na kwa wakati gani. Tuwafundishe vijana wetu wajue wanaongea na nani, wapi wanaongea nini na watumie lugha ya staha,”alisema.