Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Huu hapa mbadala wa matumizi ya nguvu katika malezi

Muktasari:

  • Ikiwa tunataka tusichape watoto, upo umuhimu mkubwa wa wazazi, hususani mama kupatikana, kuelewa hisia za mtoto, na yeye mwenyewe kuonekana kweli ana uso wenye matumaini.

Dodoma. Utafiti uliofanyika miaka ya 1970 na mshunuzi nguli, Mary Ainsworth ulionesha kuwa msingi mkubwa wa changamoto nyingi za kitabia kwa watoto,  ni kilio cha kukosa upendo, ambao ni hitaji kuu la kila mwanadamu.
Kupendwa, ni ile hali ya mtoto kujisikia kukubalika, kuonekana, kuthaminika na kueleweka na mzazi wake.

Kimsingi, hata mjadala wa ‘tuchape au tusichape’ mzizi wake mkubwa ni uelewa wa jambo hili muhimu. Kwamba mtoto asiyeamini anapendwa hawezi kuwa na adabu kama nitakavyoeleza.

Mary Ainsworth, baada ya kuwachunguza watoto kwa maelfu, aligundua wangeweza kuwagawanya kwenye makundi makuu manne kama ifuatavyo.


Mtoto mtulivu

Huyu ni mtoto anayejisikia huru kucheza bila kumsumbua mama yake. Uso wake una furaha na matumaini na mara kwa mara, kwenye utafiti wa Ainsworth, alijaribu kumshirikisha mama michezo yake.

Mama anapoondoka haoneshi wasiwasi. Ingawa hapendi mama aondoke, hata hivyo, kubaki na mgeni si tatizo kubwa kwake. Utulivu huu ni ushahidi wa imani alinayo kwa mama na mgeni.

Jambo la msingi hapa ni kuwa kwa karibu kila mtoto mtulivu Mary Ainsworth  aligundua mama alikuwa na tabia ya kupatikana kwa mtoto kimwili na kihisia na hakuonekana kuwa mtu mwenye huzuni na ishara za maisha yenye simanzi.

Mtoto wa kundi hili, huwa na mtazamo chanya na watu, hagombani na watu  na anajali hisia za mtu mwingine. Kwenye migogoro, hatumii nguvu. Unapomkosea, anajali hisia zako, mwepesi kusamehe na anapokosea hapati shida kuomba msamaha.

Huyu kwa hakika si mtoto unayehitaji kumchapa wala kutumia mabavu kuwasiliana naye.


Mtoto kiburi

Mtoto huyu haoneshi uchangamfu anapokuwa na mama na wala hafanyi jitihada za kufurahia ukaribu. Hata mama anapoondoka hajali.

Mama anaporudi, mtoto kiburi haonekani kuwa na haja ya kumfuata na anaweza kuendelea na michezo yake kama vile hajamwona.

Je, kuna uhusiano wowote na malezi? Kabisa. Kiburi hiki cha mtoto kinahusishwa na mama asiyejali hisia za mtoto hata pale mtoto anapokuwa na hitaji kubwa la kueleweka, kusikika na kuthaminika.

Tabia hii ya kutojali hisia za mtoto inachangia tatizo la mtoto kutosumbuka kupambania ukaribu na mama.

Je, unadhani fimbo inaweza kuwa suluhu unapokuwa na mtoto wa kundi hili? Hata kidogo. Unapomchapa unaendelea kuongeza umbali wa kihisia na mtoto, na kwa hakika, huwezi kukitoa kiburi chake kwa mabavu.

Tukifanya kosa la kuendelea kushughulika na tabia zake za kiburi kwa mabavu, kimsingi tunakuwa tumeimarisha zaidi tatizo na ukubwani anaweza kugeuka kuwa mtu asiyejali hisia za watu wengine na akaingia kwenye matatizo.


Mtoto muoga

Huyu ni mtoto ‘anayemganda’ mama na muda wote anaweza kutaka abebwe. Uso wake hujaa wasiwasi kwa hofu ya kubaki mwenyewe.

Kuondoka kwa mama huleta kizaazaa na kumnyamazisha mama anapomwacha si kazi nyepesi. Kimsingi, hana imani na usalama wake mbali na mama na hisia za kutafuta huruma humtawala.

Mama anaporudi chumbani, mtoto huyu angeweza kulia mithili ya mtu anayesema, ‘Kwa nini ulinionea kwa kuacha mwenyewe?’ Huyu ni mtoto asiyejiamini, asiyeamini watu na tabia zake, kwa kiasi kikubwa hutegemea wengine wanataka nini.

Mama wa mtoto huyu, kitabia anajali hisia za mtoto,  anajua kupenda, lakini hatabiriki. Mtoto anapokosa uhakika ni wakati gani hasa atapata upendo wa mama yake, huleta hali ya wasiwasi unaoathiri imani yake kwa mama.

Je, unadhani fimbo inaweza kuwa suluhu unapokuwa na mtoto wa kundi hili? Hata kidogo. Badala ya kumchapa anapoonesha tabia za usumbufu, kubwa unalohitaji ni upatikanaji wako, huna sababu ya kumchapa.


Mtoto mkorofi

Huyu ni mtoto asiyeelewa mbadala wa nguvu na mabavu. Katika utafiti wa Mary Ainsworth, huyu ni mtoto ambaye angeweza kucheza kwa kumpiga piga mama na midoli yake.

Kuondoka kwa mama hakumsumbui kama ilivyokuwa kwa mtoto jeuri lakini anaonekana kumchangamkia mgeni kuliko mama yake, kumaanisha ni mwepesi kuamini watu asiowajua kuliko familia yake.

Ukatili unaonekana kwa mtoto, ni matokeo ya kulelewa na mama mkali kupindukia, asiyeelewa hisia zake, asiyetabirika anataka nini na mkatili.

Katika mazingira yetu, huyu anaweza kuwa mama mwenye matusi, mbabe, anayetumia mabavu kuadabisha na huenda anaweza kumwacha mtoto alie bila msaada.

Fimbo haiwezi kuwa ufumbuzi wa mtoto wa kundi hili asilani. Kadri unavyomchapa ndivyo unavyoimarisha ukatili, ubabe, ugomvi, unaoweza kuumiza watu wengine.


Tunachojifunza

Kama tulivyoonesha, uhusiano wa karibu na mtoto ndio msingi hasa wa kuepuka bakora na matumizi ya mabavu. Uhusiano huu, kwa kiasi kikubwa, unamtegemea mama.

Ikiwa tunataka kugeuza meza tusichape, upo umuhimu mkubwa wa wazazi, hususani mama kupatikana, kuelewa hisia za mtoto, na yeye mwenyewe kuonekana kweli ana uso wenye matumaini.