Kutongoza kila mwanamke kunavyopromosha vijana

Anakuja mwanamke mnayefahamiana na kukwambia ana kazi fulani na anatafuta mtu wa kuifanya. Kwa bahati mbaya wewe huwezi kuifanya kazi hiyo kwa sababu zozote zile, labda muda unakubana, huna ujuzi wa kuifanya na kadhalika.

Lakini kuna mtu unamfahamu na unaamini ukimpatia hii kazi ataiweza, unamuunganisha na aliyekupa kazi na kuwaacha waendelee na mazungumzo ukitemegemea watayamaliza wenyewe.

Kweli, wanayamaliza! Wanayamaliza kwa kushindwa kufanya kazi huku sababu ikiwa ni mtu wako alishindwa kuzuia tamaa zake za kiume, akamtongoza mwanamke aliyempa kazi a.k.a bosi.

Mwanamke akaona huyu mtu ana hitilafu za kitaaluma, huwezi kuanza kutongozana na mtu unayetaka kufanya naye kazi mapema au haraka haraka namna hiyo, katikati ya kazi na huo ndiyo ukweli.

Vijana wanashindwa kujizuia na vitu vidogo. Kila mwanamke wanayemtamani wanadhani anaweza kutongozwa muda wowote bila kujali mazingira na wakati na hii ni moja ya sababu zilizowanyima fursa vijana wengi.

Sio dhambi kutongoza, ni sahihi kabisa kutongoza mtu ambaye umemuona na kumpenda, lakini hii tabia ya kutongoza kila mwanamke, wakati wowote, mahali popote inasababisha unapoteza watu ambao pengine walistahili kubaki kuwa marafiki zako tu ili mfanikishe mambo mengine ya kimaisha, ili mfanye biashara pamoja na madili mengine.

Tatizo kubwa ambalo tunalo vijana wa sasa ni haraka, hatuzingatii muda na eneo kabisa. Kuna methali ya mtaani inasema, ‘kumchinja kobe kwataka timing’ ikimaanisha unapotaka kufanya jambo gumu au ambalo limekaa kimtegomtego, zingatia muda unaotaka kulifanya jambo hilo.

Kama kweli unampenda mtu, inaweza kuwa rahisi zaidi ikiwa ukaanza kufanya kazi yake kwanza, kisha kazi ikiisha ukajaribu kumtafuta na kumueleza shida zako zingine. Lakini kumtongoza mtu katitkati ya kumpa mtego na wasiwasi juu ya maadili yako kwenye masuala ya kitaaluma.

Na kuna watu wanauliza kwani hamuwezi kufanya kazi mkiwa wapenzi? Jibu ni inawezekana lakini kuna sababu kubwa ya ofisi kuweka sera zinazohusisha mahusiano kazini. Sera kama wapenzi hamuwezi kufanya kazi katika kitengo kimoja, au wapenzi hamuwezi kufanya kazi huku mmoja akiripoti kwa mwenzake, yote hii ni kwa sababu inahatarisha afya ya kazi, sio kwenu tu, hata kwa wafanyakazi wenzenu.

Kwa mfano wewe ni mkuu wa kitengo na una uhusiano rasmi ya kimapenzi na mmoja wa wafanyakazi unawaongoza. Inapotokea unahitajika kutoa uamuzi kumuhusu mara zote wafanyakazi wengine hudhani umefanya uamuzi hayo ukisukumwa na mapenzi yenu hata kama haikuwa hivyo.

Kwahiyo tunapoanza kuwatongoza watu tuliukutanishwa nao kwa ajili ya kazi, tena bila kuzingatia ‘timing’ tunajiweka kwenye hatihati ya kuzikosa hizi fursa kwa sababu kama mwanamke ana sera kali yanapokuja masuala ya kazi maana yake ni atakukataa na ujue ndiyo umepoteza na mchongo aliokuwa anataka kukupa. Kwa sababu kwa akili yake ataona una mapungufu makubwa ya maadili kitaaluma, ya kuanza kuingiza mapenzi kwenye kazi tena mapema hata kabla hamjafahamiana vizuri.

Sasa kwanini ucheze bahati nasibu maisha yako kwa kiasi kikubwa namna hiyo? Kuna haja gani? Huyo mwanamke ana kipi ambacho unadhani ukikikosa utakuwa umepoteza almasi ya mwadui, au ana nini ambacho unadhani kinalingana na kuhatarisha nafasi yako ya kujiongezea kipato kwa kufanya naye kazi tu? Ana nini? Kama hakuna sababu kubwa, hakuna haja ya kutongoza wanawake ovyo kwenye maeneo ya kazi.