Misingi na nguzo kuu za ndoa

 Nkwazi Mhango

Kama ilivyo nyumba, ndoa ina misingi yake. Kama ilivyo taasisi yoyote, ndoa ina nguzo hata miiko yake ambayo wanandoa wanapaswa kuizingatia na kuilinda.

Hapa, tutaongelea misingi mikuu ya ndoa ambayo tunaidadavua kama ifuatavyo; japo kwa uchache na ufupi ili kukuachia fursa na wakati muafaka kufanya utafiti binafsi na huru wewe mwenyewe.
 

Upendo wa kweli

Msingi mkuu wa kwanza wa ndoa ni upendo, maana bila upendo hakuna ndoa na kama ipo ni majuto na mateso, tena ya kudumu. Upendo ndiyo cheche inayoanzisha hitajio la kufunga ndoa. Hii haina maana kuwa hakuna misingi mingine muhimu. Ipo, ila upendo ndiyo msingi wa kwanza.
Kama ndoa ni dini, basi upendo ni imani. Maana bila imani hakuna dini.

Bila upendo wa kweli, hakuna mapenzi bali kutakana, kutumiana hata kuzidiana kete tu, maana mtaishi katika gereza. Tunadhani neno ndoa ni ndoana hutokana na uwepo wa ndoa zisizo na upendo wa kweli. Ndoa zenye upendo wa kweli ni kama pepo, hata ziwe na changamoto kiasi gani. Tutoe mfano mwingine. Kama ndoa ni mchuzi, basi upendo ni viungo. Kukiwapo upendo, msingi, nguzo na mambo mengine hufuata kirahisi.

Hivyo, wanaofunga ndoa, wahakikishe wanapendana kwa dhati na kwelikweli. Ndoa siyo lelemama wala jambo la muda kama urafiki na mahusiano mengine. Baada ya kufungwa ndoa, upendo na utayari hupimwa na changamoto za ndoa ambazo leo hatutazigusia. Tusisitize. Lazima kuwe na upendo wenye pembe kuu mbili, yaani udhati na ukweli.
 

Uaminifu wa dhati

Msingi wa pili wa ndoa ni uaminifu, hasa ikizingatiwa kuwa ndoa ina majaribu na mitihani mingi, iwe ya kijamii hata kiuchumi. Hivyo, wanaofunga ndoa, wahakikishe wanaaminiana na si kuaminiana tu, bali wahikikishe wanaaminika pia. Kwa nini uaminifu ni lazima na muhimu katika ndoa? Chukulia mfano inatokea hali ya kuyumba kiuchumi, ugonjwa, kesi, na mengine kama hayo.

Kama wahusika hawaaminiani juu ya kupendana, hakuna atakayejitoa au kumvumilia mwenzake. Hakuna mtihani mkubwa kama kuyumba kiafya au kiuchumi. Hebu fikiria mwenzako wakati mnaoana alikuwa nazo.

Mara ghafla unatokea mkwamo kiuchumi. Kwanza, waliowazunguka wataanza kujua kulingana na maisha yanavyobadilika. Hivyo, wapo watakaotaka kujua kunani. Hapa ndipo msingi mwingine wa usiri au kutunza siri za ndoa unapoingia na kufanya kazi au kukosekana na kuharibu kila kitu. Wahenga wanatuasa kuwa siri ya mtungi aijuaye kata. Na hapa tusisitize. Ni kata pekee apaswaye kuijua na kuitunza siri ya mtungi.

Katika mkwamo, siri za ndoa zinapovuja, wapishi watakuwa wengi na kuharibu mchuzi. Kimsingi, unapokosekana uaminifu ambao hutokana na kuenda sambamba na kutojiamini wala kuchukua tahadhari dhidi ya hatari dhidi ya ndoa, ndoa itayumba hata kusambaratika. Kama zilivyo taasisi zozote, lazima ziwe na kanuni; maadili, ithibati, miiko, uhuru, upekee, uaminifu, usiri na wivu.

Ndoa ikikosa au kupungua vitu hivi hugeuka tegemezi na hatarishi. Ndoa inayoendeshwa kwa utegemezi wa ushauri na matakwa ya wasiohusika si imara wala salama. Japo hatukani kuwepo kwa wanafamilia, jamii, wengine, si washirika katika ndoa. Ndoa si ushirika na haina wala haihitaji ushirika. Ndoa inapoanza kuendeshwa kwa mawazo, misukumo na ushauri wa marafiki mashoga, hata ndugu, ujue iko hatarini.

Ndoa ni ya wanandoa. Ndio wajuao misingi, miiko, siri, thamani na umuhimu wake. Ndoa si klabu. Ina misingi, sababu na siri zake. Ndoa ni kama serikali. Ndiyo maana huiingii bila kuapishwa, kuonywa, na kupewa majukumu. Hapa mantiki ni rahisi na wazi. Wanandoa ndio wanaojua sababu za kufunga ndoa. Ndio wanaojua thamani na umuhimu wake, pia waathirika wa kuvunjika au kushindwa kwa ndoa yao. Ndoa ni kama utajiri.

Inapotokea tajiri kufilisika, muathirika wa kwanza na mkuu ni yeye na siyo marafiki wala nguvu zao. Hivyo, tufahamu kuwa wanandoa ndiyo wajenzi hata wavunjaji wa ndoa. Kimsingi, adui wa kwanza wa ndoa ni wanandoa wenyewe, hasa pale wanapokiuka misingi yake.

Tusisitize. Ndoa ni kama jengo. Kama itajengwa kwenye misingi na ikaongezewa nguzo imara, itadumu. Kama itajengwa bila msingi au kwenye msingi na nguzo hafifu, itaporomoka itakapokumbana na changamoto, hata ziwe ndogo kiasi gani.