Muhimu kuwa na ratiba ya vipimo vya magonjwa ya ngono

Muktasari:

  • Tunapozungumzia magonjwa ya zinaa jambo ambalo wengi huwajia akilini ni virusi vya Ukimwi, japokuwa kuna magonjwa mengine mengi ya zinaa ikiwemo kisonono, kaswende na magonjwa mengine mengi.

Magonjwa ya zinaa ni moja ya magonjwa ya kuambukiza yanayoenea kwa kasi kwa siku za karibuni ambapo kutotumia kinga wakati wa kushiriki tendo la ndoa na kuwa na washiriki wengi wa tendo la ndoa zimekuwa ni baadhi ya sababu kubwa zinazosababisha maambukizi ya magonjwa hayo. Tunapozungumzia magonjwa ya zinaa jambo ambalo wengi huwajia akilini ni virusi vya Ukimwi, japokuwa kuna magonjwa mengine mengi ya zinaa ikiwemo kisonono, kaswende na magonjwa mengine mengi.

Magonjwa ya zinaa yana madhara makubwa kuanzia kwenye mfumo wa uzazi na hata afya kwa ujumla kwani huchangia kusababisha ugumba na utasa na hata aina mbalimbali za magonjwa ya saratani bila kusahau matatizo mengine kama vile harufu mbaya kwenye via vya uzazi.

Lakini jiulize, je unajenga utamaduni wa kupata vipimo vya magojwa haya mara kwa mara? Kama daktari nakiri kuwa bado watu hawatilii maanani suala la kupata vipimo vya magonjwa ya zinaa.Hivyo nakushauri ni vyema ukaanza utaratibu huo kwani kadri unapowahi kugundua magonjwa ya zinaa mapema, ndipo unapokuwa kwenye nafasi nzuri ya kupona kutokana na kuwahi matibabu na kuzuia madhara mengine makubwa yatokanayo na magonjwa haya.

Lakini je unatakiwa kupata vipimo hivi mara ngapi hasa kwa mwaka? Kujua kama unahitaji kupata vipimo mara ngapi kwa mwaka inategemea unashiriki tendo la ngono mara ngapi na washirika wangapi tofauti na hasa kama hautumii kinga. Hivyo huu ni ushauri wangu kuwa na utaratibu wa kujiwekea ratiba ya kupata vipimo vya magonjwa ya zinaa.

Kuna kundi la watu ambao wao wanadumu na mshirika mmoja tu wa tendo la ndoa kwa muda mrefu. Na hii ndiyo inayoshauriwa kiafya na kimaadili pia. Kuwa na mshirika mmoja inakusaidia kukukinga na hatari ya kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa na kubwa zaidi ni ugonjwa Ukimwi. Lakini kuwa na mshirika mmoja haimaanishi kuwa haupaswi kuendelea kupata vipimo vya magonjwa ya zinaa.

Kuwa na mshirika mmoja haina maana kwamba hauwezi kuambukizwa magonjwa ya zinaa hapana! Maambukizi unaweza kuyapata ila tu hatari ya kupata maambukizi inakuwa ni ndogo. Hivyo kama una mshirika mmoja unashauriwa kupata vipimo hivi angalau mara moja kwa mwaka.

Kuna kundi la watu ambao wanakuwa na mshirika mmoja lakini wanashindwa kudumu na mshirika huyo mmoja yaani baada ya muda fulani mahusiano yao yanavunjika na hivyo kulazimika kutafuta mshirika mwingine.

Kundi hili pia halina tofauti sana na mtu anayekuwa na washirika wengi wa tendo la ndoa kwa muda mmoja. Kundi hili lipo kwenye hatari kubwa sana ya kupata maambukizi ya magonjwa ya zinaa kuliko kuliko kundi lingine lolote na hasa tukizingatia ukweli kuwa ni vigumu kumkosa mtu mwenye maambukizi kati ya idadi ya watu watatu hadi watano unaoshirikiana nao kimapezi.

Ndani ya idadi yi ni lazima utampata mshirika ambaye ana maambukizi ya magonjwa ya zinaa. Kundi hili linahitaji vipimo vya magonjwa ya zinaa kila baada ya miezi mitatu kutokana na hatari kubwa ya kupata maambukizi na kushiriki tendo la ndoa na idadi kubwa ya watu ndani ya muda mfupi. Lakini pia bila kuwasahau wale wote ambao hupendelea tabia ya kufanya ngono kupitia njia ya haja kubwa na mdomo. Hawa nao wapo hatarini sana.