Ni mshono na umbo kitenge hakina baya
Unapozungumzia mitindo ambayo ipo kwa muda mrefu na itaendelea kuwepo huwezi kuacha kutaja kitenge. Vazi la kitenge kwa sasa linaweza kubeba utambulisho wa Afrika kwa kuwa karibu nchi nyingi za bara hilo kitenge kinapatikana.
Tofauti inaweza kuwa kwenye malighafi iliyotumika kukitengeneza, lakini kwa mwonekano bado kitaendelea kuwa kitenge kile kile.
Kwa maana hii ni kwamba, vazi hili litaendelea kuwepo kwa muda mrefu na kugusa watu wa rika zote bila kujali jinsia.
Licha ya kuwa wapo wanaume wanaovaa mavazi yaliyotengenezwa kwa vitenge, wanawake ndio hasa wanaolichangamkia vazi hili.
Tumeshatoka zile zama za kufikiri kitenge ni vazi la wazee na linavaliwa zaidi kanisani au katika maeneo ambayo yanakusanya watu wa heshima kama vile kwenye mikutano, semina, warsha au maofisini.
Hiyo inaweza kuwa ni kasumba iliyotawala mabinti wengi, lakini sasa imeanza kubadilika kwa kuwa imethibitika kitenge kinaweza kuwa maalumu kwa ajili yao endapo kitashonwa na kutengenezwa nguo ambayo itazingatia mazingira ya eneo husika.
Nguo ya kitenge kama ilivyo kwa mavazi mengine ambayo hupendelewa na wasichana inaweza kuvaliwa kwenye matembezi, ufukweni hata katika mizunguko ya hapa na pale ambayo wengi hupendelea kuvalia aina nyingine ya nguo.
Hapa ndiyo tunarudi kwenye hoja ya mshono na umbo, uzuri wa vazi la kitenge utaonekana pale litakaposhonwa vizuri kwa kuendana na mwili wa mvaaji.
Kwa kutumia fundi stadi kitenge kinaweza kubuniwa katika mtindo ambao utamfanya msichana ajione mwenye mvuto ndani ya vazi hilo kuliko hata suruali ambazo zimekuwa zikiwateka wengi.
Sio lazima kushona gauni au sketi ndefu kama wanawake watu wazima wanavyofanya, ukiwa kama msichana lazima kuwe na tofauti ya mavazi kati yako na mama mwenye umri wa miaka 35 na kuendelea.
Seleman Yusuf, fundi cherehani anayemiliki ofisi yake inayojulikana kama Ambiele Tailoring Mart iliyopo Mikocheni anasema licha ya kuwepo kwa aina nyingi ya mavazi bado kitenge kitabaki kuwa na thamani kubwa kwa mwanamke na msichana wa Tanzania.
Anasema uzuri wa vazi hili kwa mvaaji anaweza kushona mshono ambao anahisi utampendeza na kukufanya kuonekana mwenye mvuto, hususan kwa wasichana ambao hupendelea kushona magauni mafupi ili kwenda na wakati.
Anasema mtindo huu uko kawaida sana, hata ushonaji wake hauchukui muda mrefu kutokana na kutokuwa na mikato mingi, ingawa mikono hushonwa kadiri anavyohitaji mvaaji.
“Wapo ambao wanapenda ya mikono mifupi, wengine mikono ya kawaida na yapo pia ambayo hukatiwa kifuani, hivyo haya hayana mikono, lakini yote yanamfanya mvaaji kuvutia na kupendeza kwa kiasi kikubwa,” anasema.
Kwa mujibu wa Rosemary Mhagama, kadiri siku zinavyokwenda kunaibuka mitindo ya kushona ambayo inaweza kumshawishi msichana kujaribu kushona kitenge tofauti na miaka ya nyuma kidogo ambapo vali hilo lilikuwa likivaliwa eneo maalumu tu.
“Zamani kitenge kilikuwa kinaonekana sana kanisani, lakini siku hizi ukipata kitenge kizuri na fundi ambaye anaweza kushona vizuri unaweza kuonekana msichana umependeza kuliko hata aliyevaa skin jeans,” anasema Mhagama.