Obby David Kukatishwa tamaa kumemuongezea nguvu

Muktasari:
- Mashairi ya wimbo huo yanayompa heshima mama kwa jukumu zito alilonalo hasa katika malezi, huwa inawafanya wengi wainuke kucheza wakati anapoimba kwenye matamasha mbalimbali.
Moja ya kazi zilizoachiwa hivi karibuni na kupenya maeneo mengi ni ‘Hakuna Kama Mama’ ya mwanamuziki anayechipukia kwa kasi ‘Obby David’ son BM mkazi wa jijini Dar es Salaam.
Mashairi ya wimbo huo yanayompa heshima mama kwa jukumu zito alilonalo hasa katika malezi, huwa inawafanya wengi wainuke kucheza wakati anapoimba kwenye matamasha mbalimbali.
Mwenyewe anasema malezi bora kutoka kwa mama yake ndiyo yaliyomfanya atunge wimbo huo.
“Huu ndio wimbo uliobeba albamu yangu mpya na ninamshukuru Mungu kwa sababu umepata kibali na kila ninapoimba, huwa naona utukufu wa Mungu,” alisema Obby.
Alisema tayari video ya albamu yake ya ‘Hakuna Kama Mama’ imeshakamilika na kwamba wakati wowote ataiachia mtaani.
Alitaja nyimbo nyingine zinazobebwa kwenye albamu hiyo kuwa ni Heri Wamchao Bwana, Yesu Ndiye Baba, Maisha Yangu, Amezaliwa Mwokozi, Kama Kuzunguka na Baba Unaweza.
Alisema changamoto kubwa anayopitia wakati anaanza kuimba ni kuvunjwa moyo na baadhi ya watu wake wa karibu kwamba, sio rahisi kwake kufanikiwa kiuimbaji japo anacho kipaji cha kuimba.
“Ilikuwa ninapoomba ushauri mtu ananikatisha tamaa sasa kama ningesikiliza nisingefikia hapa nilipo. Kwa hiyo niwaase wenzangu wapambane wasikubali kuishia njiani,” alisema.
Alisema changamoto nyingine ni kukosekana kwa meneja kwa ajili ya kusimamia kazi zake.
“Ni vigumu kufanya kazi bila meneja, nitashukuru kama nikimpata kwa sababu naamini uwezo wangu utaongezeka. Wanamuziki wenye uongozi wanafanya vizuri sana ikilinganishwa na sisi tusio na uongozi,” anasema.
Hata hivyo, anawasihi watangazaji kutoweka gharama kubwa wanapotaka kuwafanyia mahojiano au kupiga nyimbo za waimbaji kwa kuwa wengi, kazi zao zinaishia makabatini kwa kukosa fedha za kufanyia hivyo.
Akielezea safari yake kimuziki, Obby alisema mwaka 2013 alianza kuimba lakini wakati huo alifanya huduma hiyo chini ya kwaya na timu ya kusifu na kuabudu.
“Baadaye nikawa kiongozi wa kusifu na kuabudu na nimehudumu kwenye makongamano mengi makubwa Dar es Salaam na nje ya mkoa huu. Huko ndiko nilikopata nguvu ya kusimama na kuanza kuimba peke yangu,” anasema.
Anasema makambi ya vijana aliyokuwa akihudhuria na kuyaongoza kwenye huduma ya uimbaji yalimnoa na kumpa uwezo mkubwa wa kutunga nyimbo zake mwenyewe.
“Nyimbo zote zilizo kwenye hii albamu nimezitunga. Namshukuru Mungu kwa hatua hii kubwa,” anasema.
Mwanamuziki huyo anasema kwa kiwango alichofikia, yupo tayari kupokea mialiko ya huduma hiyo mahali popote nje na ndani ya nchi kwa sababu anaamini, kwa kuhudhuria makongamano hayo kazi zake zitaendelea kuwafikia wengi.
Anasema kitu pekee anachopendelea kwenye kazi yake ya muziki ni kuifikishia jamii ujumbe unaoweza kubadili maisha yao.
Akielezea mkakati wake, mwanamuziki huyo anasema ni kuendelea kumtumikia Mungu kwa viwango vya juu zaidi.