SAIKOLOJIA : Sababu za binadamu kutofautiana tabia

Muktasari:

  • Ili asiwafanye wanafunzi wachoke kwa mihadhara, alikuwa akitumia mbinu mbalimbali za kufundishia kama vile maigizo.

Mwanamke mmoja aliyesomea maendeleo ya jamii aliamua kuwafundisha wenzake katika kijiji chao kuhusu ujasiriamali na madhara ya unyanyasaji wa kijinsia.

Ili asiwafanye wanafunzi wachoke kwa mihadhara, alikuwa akitumia mbinu mbalimbali za kufundishia kama vile maigizo.

Hata hivyo, siku moja, mwanamke mmoja alilalamika kuwa yeye haridhiki na jinsi mwalimu wao anavyowafundisha. Alisema wao ni watu wazima lakini mwalimu wao anawafanya wajifunze kwa kuigiza kama watoto na wakati mwingine kuwaimbisha nyimbo na kuwachezesha ngoma za asili.

Baada ya muda alijitokeza mwanamke mwingine aliyempinga vikali yule wa kwanza. Yeye alisema mwalimu wao anawafundisha vizuri.

Kutokana na mtafaruku huu wanakikundi wakagawanyika katika makundi mawili. Moja likimuunga mkono yule mwanamke wa kwanza na jingine likimuunga mkono yule wa pili. Mapambano ya maneno na vijembe na mipasho akitawala katika kikundi hadi ikafika hatua ya kugombana hata wakakaribia kupigana. Mwalimu akajitahidi kurekebisha hali lakini akashindwa na kuamua kuwashirikisha viongozi, lakini haikusaidia kwani waligawanyika katika makundi matatu yaliyokuwa na mawazo tofauti. Hatimaye kikundi kikavunjika na huo ukawa ndiyo mwisho wa ndoto ya yule mwalimu ya kutaka kuleta maendeleo kwa wanawake wa kijiji chao.

Mambo haya hutokea

Katika makala hii tutajifunza sababu ambazo hufanya watu watofautiane katika hisia na tabia na hata katika vitendo. ?

Haiba inaweza kutafsiriwa kama tabia nafsi na mwenendo wa jinsi mtu anavyotenda mbele ya watu katika namna ambayo humfanya aonekane tofauti na watu wengine.

Ni dhahiri kuwa watu hutofautiana hata kama ni mapacha waliotokana na yai moja. Labda tu kama baada ya kuzaliwa watalelewa katika mazingira yasiyotofautiana hata kidogo na watendewe kila jambo katika mtindo usiotofautiana.

Tunamalizia kueleza maana ya haiba kwa kusisitiza kuwa haiba hutokana na vitu viwili, kwanza ni urithi ambao mtoto hurithi kutoka kwa wazazi waliyemzaa na pili ni mazingira ambayo anakulia ndani yake.

Tabia za kurithi

Kila mara huwa tunaona hali ya kufanana kati ya mtoto na wazazi. Viasiliasafu vya urithi huweza kuleta hali ya kufanana baina ya mzazi na mtoto katika vitu kama vile rangi ya macho, rangi ya ngozi na nywele, umbo na ukubwa wa kichwa na mara nyingi zaidi katika kimo. Katika urithi bado kuna swali ambalo linawatatanisha wataalamu ambalo ni kama mtoto anaweza kurithi akili kutoka kwa wazazi wake.

Labda kabla hatujalitafakari suala hili tujiulize akili ni nini? Ni uwezo wa kufikiri na kuwaza kinadharia na kuweka hizo fikara katika utendaji wenye viwango na ufanisi. Tafsiri hii ni moja kati ya nyingine kadhaa zilizozingatiwa katika tafiti zilizofanyiwa ili kubaini kama akili inaweza kurithiwa au hapana. Kwa kiasi fulani matokeo yameonyesha kuwa kwa kiwango kidogo akili inaweza kurithiwa kidogo lakini ukweli ni kuwa akili hukomaa kutokana na mazingira.

Walimu na viongozi wanakubaliana kuwa mazingira ni kitu chenye umuhimu wa pekee kabisa katika malezi ya mtoto na hata katika kukomaa kwa akili. Kwa kawaida kama akili itachangamshwa nyumbani kwa kujifunza kutoka kwa wazazi, kaka na dada na kupatiwa msaada katika kutambua baadhi ya masuala na matatizo ni dhahiri kuwa itakomaa.

Kwa miaka mingi wanasaikolojia wamekuwa wakifanya utafiti ili kubaini kipi ni muhimu zaidi katika kumjenga binadamu kama ni urithi au mazingira. Hata hivyo, mwisho waliamua kuacha kuendelea na utafiti huo kwani ilionekana kama kujiuliza kipi ni muhimu katika gari kama ni injini au petroli.

Binadamu hutofautiana vipi?

Tumekwisha fahamu kuwa kila mmoja wetu ana haiba ya kipekee kutokana na urithi na mazingira yanayotofautiana. Hata hivyo tukianza kulianganisha tofauti na sifa za kimaumbile moja baada ya nyingine tutagundua kuwa karibuni binadamu wote tuko sawa.

Katika nchi fulani kuna vipimo maalumu vya urefu vinavyohitajika kwa vijana kuingizwa jeshini. Wastani wa kimo kilichokubalika kilikuwa sentimeta 174.5. Katika vijana waliopimwa mwaka fulani asilimia 68 walikuwa na kimo cha kati ya sentimeta 168 na 182; asilimia 95 walikuwa na kimo cha takribani sentimeta 158 na 190. Ni asilimia 2 tu waliokuwa na kimo cha zaidi ya sentimeta 191. Hiki ni kielelezo halisi cha hali inavyoweza kuwa katika nchi yoyote.

Yaani haiwezekani watu wengi zaidi wakawa warefu au wafupi. Mtandao wa tofauti za urefu na watu unafuata mpindo unaitwa mzingopinda wa kawaida. Kanuni hii haishii tu katika vimo vya watu bali unafanana hata katika sifa mbalimbali kama vile ukarimu, ucheshi, uchoyo, akili, uongo na nyinginezo. Hususan, tulio wengi tuko kwenye wastani na wachache ndiyo walio kwenye upeo wa mwisho kwa upande wa hali ya juu au ya chini.

Tuhitimishe makala yetu kwa kusema, iwapo tutachukua sifa moja baada ya nyingine tutagundua kuwa tulio wengi tunafanana. Lakini tukitazama kwa mfumo mzima wa mwingiliano baina ya haiba zetu tutagundua kuwa kila mmoja wetu ana sifa zake za binafsi za pekee zinazomfanya awe yeye tofauti na mtu mwingine yoyote.