TUONGEE KIUME: Mwanamume fanya yote usisahau hili

Kondakta wa daladala Dar es Salaam huamka saa kumi alfajiri na kukutana na dereva wake sehemu wanapolaza gari lao.

Mpaka wakitoka hapo kuingia barabarani kuanza kazi huwa saa kumi na moja imeshafika. Wanaanza kupiga mzigo, kufanya kazi mwanzo mwisho, kama unavyofahamu, majukumu ya konda wa daladala ni kusimama siku nzima, kukimbiza gari muda wote na kupiga kelele kuita abiria bila mapumziko.

Mchana atapumzika kidogo kula kisha ataendelea na kazi hadi usiku. Kama ikiwa ni siku nzuri kibiashara basi kondakta wa daladala na dereva wake wanaweza kwenda kulaza gari saa 4 za usiku. Na kama ni siku ngumu, usishangae kuona wakiendelea kupiga mzigo mpaka saa 6 za usiku.

Kwa hiyo tuseme wakienda kulala saa sita za usiku; na siku inayofuata wakaamka saa 10 alfajiri watakuwa wamelala saa nne tu.

Ratiba hii unayoiona kwa kondakta wa daladala inafanana karibu na kila mtu anayeishi na kufanya kazi miji mikubwa kama Dar es Salaam.

Hata wanaofanya kazi ofisi za kupulizwa na viyoyozi iko hivi hivi. Saa 12 wanakuwa tayari wako barabarani wanasubiri usafiri wa kwenda ofisini na watafanya kazi na kurudi nyumbani usiku wa saa mbili au saa tatu. Kimsingi, ratiba ya kutafuta maisha inachosha sana, hasa kwenye miji mikubwa. Na ratiba hii ndiyo inanifanya nijiulize, je, ina maana sisi duniani tumekuja kuishi hivi kisha tufe tuondoke duniani?

Na hapa ndipo ninapotaka kuwakumbusha wanaume wote kuwa, iwe unaamini Mungu au huamini, lakini sitaki kuamini kwamba huyo unayemuamini alikuumba uje duniani kwa ajili ya kuamka alfajiri, kwenda ofisini kufanya kazi siku nzima, kisha kurudi nyumbani usiku, kuoga, kula kupanda kitandani kulala mapema ili kesho uweze kuamka alfajiri kwenda tena ofisini.

Na kwa sababu hiyo ningependa kuwakumbusha wanaume wenzangu kwamba, tuhakikishe tunatafuta namna ya kuipa pole miili yetu. Ukipata kajipesa kako, chomoa Sh50,000 zako hapo, nenda sehemu kafanye unachopenda kufanya. Kama kulewa lewa, kama kula kula.

Hizi habari za wahenga za fainali uzeeni zina umuhimu, lakini ukiziendekeza utafika uzeeni ukiwa na pesa pamoja na majuto ya kwamba hukuupa mwili pole.

Ndiyo ile unazeeka unaanza kufanya mambo ya ajabu kumbe ni kwa sababu mwili umeamua kujichukulia hatua.

Tunakumbushana tu, sijasema usiweke akiba, sijasema usiwe na mipango ya kesho. Nasema tafuta namna ya kuupa pole mwili wako. Na kwa wengine kuupa mwili pole inaweza kuwa kulala nyumbani tu, lakini wakashindwa hata kufanya hivyo kwa sababu wanajifanya wanapenda sana kazi. Mtu ni Jumamosi, Jumapili au siku yako yoyote ya kupumzika, lakini utamkuta mtu bado anafanya kazi tu.

Jamani, kazi haziishi, ukifa leo kampuni unayofanyia kazi haitakufa. Kila kitu kitaendelea kama kawaida kama vile haukuwahi kuwepo. Nakumbusha, sisemi tudharau kazi, nasema tuziheshimu, tuzifanye kwa bidii, tupate pesa, lakini tusisahu kuupa pole mwili.