UREMBO: Siri ya parachichi kwenye nywele

Mvuto wa nywele kwa mwanamke hutokea pale zinapobanwa au kuchanwa katika mitindo tofauti.

Nywele kama ilivyo kwa viungo vingine zinahitaji matunzo makubwa ili kuzifanya zionekane zenye mvuto na kupendeza wakati wote.

Zipo njia mbalimbali za kutunza nywele, lakini matumizi ya zana na vifaa vya asili vina uwezo mkubwa wa kujaza nywele na kuzirefusha kwa kiasi kikubwa.

Leo tutaangalia namna ya kujaza nywele kwa kutumia parachichi, yai na asali ambavyo vyote vinatengenezwa mchanganyiko ambao ni rutuba kwa nywele.


Namna ya kutengeneza

Chukua parachichi lililoiva, kata katika vipande vidogo vidogo, kisha vunja yai na uchote kiini uweke pamoja na vipande vya parachichi.

Mimina asali katika mchanganyiko wa parachichi na kiini kisha koroga mpaka vilainike na kuchanganyika kabisa kupata rojorojo.

Baada ya kupata mchanganyiko huo safisha nywele zako kwa maji ya uvuguvugu,kausha kwa taulo au kitambaa safi kisha paka mchanganyiko huo kwa kukata mistari na kuhakikisha nywele zote zimekolea.

Kaa na mchanganyiko huu kichwani kwa muda wa dakika 15 mpaka 20 kisha safisha tena kwa maji safi.

Fanya hivyo kwa muda wa wiki moja hadi mbili na utaweza kuona matokeo mazuri katika nywele zako.