Vijana kupenda kulelewa ni ugumu wa maisha au uvivu wa kufikiri?

Muktasari:
- Baadhi ya vijana wamethibitisha kuwa jambo hilo lipo na kwamba ugumu wa maisha na uvivu wa kufikiri au kutotaka kufanya kazi, umekuwa chachu ya kushamiri kwa vitendo hivi.
Dar es Salaam. Hakuna utafiti unaoonyesha hasa idadi ya wanaume wanaolelewa, lakini kuna ushahidi wa kimazingira katika jamii ambao unazidi kushika kasi.
Baadhi ya vijana wamethibitisha kuwa jambo hilo lipo na kwamba ugumu wa maisha na uvivu wa kufikiri au kutotaka kufanya kazi, umekuwa chachu ya kushamiri kwa vitendo hivi.
Baadhi ya vijana katika kijiwe eneo la Ilala Bungoni waliliambia gazeti hili kwa sharti la kutotaja majina yao wala kijiwe chao licha ya kuwa maarufu, kuwa ‘wanajibebisha’ na wakati mwingine wanapashana habari ili kila mmoja anufaike na mwanamke anayejilengesha.
Mmoja wa vijana hao aliyekuwa ameshika simu kali mbili na kifuani kwake akiwa amening’iniza cheni ya dhahabu, alisema hajawahi kufanya kazi ila ana ‘kibosile’ mmoja anamtatulia na kuwezeshwa kuishi vizuri mjini.
“Ninaishi vizuri, kama unavyoniona sijasoma sana lakini nafahamu jinsi ya kudili na kina mama wanaopenda vijana watanashati, ”anasema huku akikataa kutaja jina lake kwa madai ya kujiharibia kwa mademu wa makamu yake.
Dogo Boy (siyo jina lake halisi) mwenye umri wa miaka 29, anasema sababu kubwa ya kufanya hivyo ni ugumu wa maisha.
Anasema vijana wengi hawana kazi akiwamo yeye huku familia ikimtegemea. “Katika hali kama hiyo nipate mtu wa kunihudumia na kunipa mikwanja nimkatae nife? ”anahoji kijana huyu.
Boy anafafanua kuwa kina mama hao wanatambua thamani ya mtu na hujitoa kwa moyo kuhakikisha mpenzi wake anamtatulia matatizo ya kifedha madogo madogo. “Unaona gari hii, alinipa nilipokuwa nasheherekea siku yangu ya kuzaliwa nilipokuwa natimiza miaka 28, na alinifanyia hiyo sherehe, tangu nizaliwe wazazi wangu hawajawahi kunifanyia wala kunipa zawadi hata inayogharimu Sh100,000 kutokana na ugumu wa maisha nimepata wa kunitoa nikatae? ”anahoji Boy.
Kijana aliyejitambulisha kwa jina moja Kolumba anasema licha ya kuwa na maisha magumu, alipata msichana wa mtaani kwao, kabila la kwao pia na ni mrembo, lakini alichomfanyia hana hamu na hataki tena wasichana.
Anasema kwa kipato kidogo, aliongeza na fedha yake aliyolipwa kwenye kiwanda fulani baada ya kuachishwa kazi, akamfungulia biashara ili iwasogeze, lakini baadae aligundua kuwa binti huyo ana mpenzi mwingine.
“Nilimfuatilia, siku niliyomfahamu mpenzi wake sikuamini kwa sababu alikuwa ni mtu mzima kuliko mjomba wake aliyekuwa anaishi nae, ”anasema Kolumba.
Kolumba anasema kuanzia hapo alichofanya ni kubadili utaratibu wa maisha , akipata fedha hununua nguo nzuri, manukato na kutengeneza mwili wake kwa mazoezi ili awe na mvuto.
,“Huyu niliye nae sasa ni wa tatu, siku za mwanzo nilikuwa naona ajabu, lakini nimeshazoea na kuona ni kawaida, napata ninachokitaka mtaji wangu ni kujiweka freshi tu, ” anasema.
Mpenzi wa Kolumba ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake anasema ana kila kitu fedha, watoto, magari, nyumba kadhaa, lakini hapati anachohitaji kutoka kwa mumewe.
Anasema ukiondoa ubize wa mumewe unaowafanya wasiwe pamoja muda mwingi, lakini mumewe haoni umuhimu wa kushiriki nae baada ya kuwa na sista duu.
Anafafanua haiwezekani mwanaume akae na mkewe mwezi na zaidi bila kujuliana hali faragha.
Rajabu Hazron anasema ugumu wa maisha unachangia vijana kupenda ‘kulelewa’.
Anasema mbali ya ugumu wa maisha, uvivu wa kufikiri na kupenda mafanikio ya maisha kwa njia ya mkato matokeo yake ndiyo wanaangukia kwa hao wanawake wenye msongo wa mawazo na wajane. “Hali hii ikiendelea baada ya muda vijana wengi watakuwa na maradhi, kwa sababu wanachoangalia wao ni fedha tu, hajali afya zao, wanaendeshwa kila wanachoambiwa kufanya wanafanya,” anasema Hazron.
Andrew James anasema ugumu wa maisha ni kisingizio ukweli ni kwamba vijana wengi ni wavivu kufikiri.
“Vijana kama hawa wakikosa wanawake wa kuwalea ndiyo wanajiingiza katika mambo yasiyofaa kwenye jamii ikiwamo katika uhusiano wa jinsia moja kwa sababu wana tamaa na wanaona mwili wao ndiyo chanzo cha kuwaingizia kipato, ”anasema James.
Kutotaka kufanya kazi ni chachu ya kushamiri kwa vitendo hivi nchini, lakini vina athari kwani vinaweza kuwa chanzo cha kupata Ugonjwa wa Ukimwi, kufumaniwa na kudhuriwa au kuuawa.
Kwa taarifa zaidi nunua gazeti lako la Mwananchi au soma mtandaoni kupitia www.epaper.mcl.co.tz