Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

JUMA NATURE: Nyota wa muziki aliyejisomesha kwa kuokota, kuuza vyuma chakavu na vitumbua

Nature.

Muktasari:

  • Mara kadhaa alitembea kwa miguu kutoka Posta hadi Kimara kufuata shoo za muziki

Historia yoyote huwa na msingi wake. Uwe wa kitu au mtu, historia hujengeka kutokana na matukio iwe ya kusikitisha, kusisimua, kufariji hata kutia moyo.

Inaweza kuishia ikihuzunisha, kufurahisha hata kuonyesha ushujaa kutokana na mtiririko wa matukio kwa jambo au mtu husika anayelezea au kusimulia historia yake.

Ndivyo ilivyo pia kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya aliyejizolea umaarufu nchini hata nje ya mipaka ya Tanzania kutokana na umahiri wake katika muziki.

Hata hivyo, siyo kila mmoja anajua historia ya nguli huyo katika muziki huo, hata kumfanya apachikwe majina mengi na mashabiki wake.

Mara zote mashabiki hawakusita kufurika alipofanya uzinduzi wa albamu zake. Hiyo huwa ndiyo kile kinachoitwa na vijana kuwa ni habari ya mjini.

Hali hiyo husababisha ulinzi wa ziada kuhitajika ili kudhibiti msongamano wa mashabiki ambao usalama wao kuwa shakani kutokana na msongamano.

Katika mahojiano na mwandishi wa makala haya Nature anaanza kwa kueleza kuwa yeye ni mzaliwa wa jijini Dar es Saam katika Hospitali ya Ocean Road mwaka 1980 na kwamba jina lake halisi ni Juma Kassim Ally.

Anasema kwamba kabla ya kufikiria kuwa mwanamuziki alikuwa ni mchezaji mzuri wa soka katika timu za uswahilini  maarufu kwa jina la ‘Cha ndimu’.

Anaeleza kuwa pamoja na kucheza soka katika timu ndogo wakati huo akisoma Shule ya Msingi Kurasini, alikuwa akiwaza kuwa kipaji hicho cha soka ndiyo ‘kingemtoa’ na kumsaidia maishani.

Anabainisha kuwa alisoma shule ya msingi kwa shida na baada ya kumaliza hakuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari.

“Elimu ya ‘kibongo’ bila kuwa na mpango mbadala wa masomo ya ziada, ni vigumu kufaulu. Wenzangu waliokuwa na uwezo walisonga mbele mimi nikaishia hapo, “anasema Nature.

Anafafanua kuwa kutokana na familia yake kutokuwa na uwezo wa kumsomesha, binafsi alikuwa na moyo wa kusoma na  aliazimia kufanya analoweza ili ajiunge na sekondari mwaka unaofuata, baada kusota nyumbani kwa mwaka mmoja baada ya kumaliza elimu ya msingi.

“Nilikuwa nikiishi uswahilini, biashara ya kwanza wakati ule kwa watoto kama mimi, ilikuwa kuuza vyuma chakavu, hivyo nilikuwa kiguu na njia kutafuta malighafi hiyo na kuuza, lengo likiwa kutafuta ada,”anasema Nature.

Msanii huyo nyota anasema kwamba alikuwa akiongeza kipato chake kwa kazi nyingine ikiwamo kupasua mawe eneo la Kurasini, kusukuma mikokoteni ya maji na mizigo, pia kuokota mkaa na kusaidia wazazi kuuza vitumbua.

“Baada ya kukusanya fedha hizo nilipata fedha ya kianzio za kulipia shule binafsi iliyopo maeneo ya Temeke (hakupenda kuitaja),”anasema.

Anaeleza kuwa alisoma huku akifanya kazi hizo ili kujikimu katika mahitaji mbalimbali ya shule, ikiwamo kulipia mitihani ya kila wiki, kununulia madaftari, vitabu na vifaa vingine vya shule.

Nature anasema kuwa akiwa kidato cha tatu ndipo alipata hisia za kupenda muziki, ambapo walikuwa wakienda katika kumbi za starehe na kukutana na vijana waliokuwa wakiimba kutoka shule mbalimbali.

Anasimulia kuwa wakiwa shuleni, kulikuwa na mpango maalumu wa kupelekwa katika semina ili kujikinga na maradhi ya Ukimwi, matumizi ya pombe na dawa za kulevya.

Anafafanua kwamba walikuwa wakifanya uhamasishaji katika Ukumbi wa Amana Center uliopo Ilala na pamoja na Ukumbi wa Ruaha Galaxy uliopo Kimara. 

Anabainisha kwamba, hapo ndipo alianza kutunga mashairi akioanisha na kile walichokuwa wakifundishwa na kuimba peke yake akijikumbusha. “Hapo nilihisi kuna kitu kipo ndani yangu kuhusu muziki.”

Anasema hisia hizo ndizo zilimfanya awashawishi vijana wenzake watatu kuanzisha kikundi kilichokuwa likijulikana kwa jina la For Skills Gangstar (FSG), ambalo kiongozi wake alikuwa yeye akitumia jina la Nature Man. Anawataja wenzake hao kuwa ni Mark 2 B, Chriss na Dollo.

 “Kama kuna watu nilikuwa nawakwaza wakati huo basi ni wazazi wangu. Walikuwa wanatiwa ndimu na mjairani kuwa muziki ni uhuni, hivyo mimi nitapotea. Nyumbani moto ukawa ukiwaka kila niliporudi, hivyo nikiwa njiani kurudi nilipanga maneno mazuri ya kumliwaza mama. Yalimtuliza jazba kwa siku husika na kupata chakula, siku nyingine kilikuwa kinawaka, hata chakula nilinyimwa,”anasema Nature.

Anaeleza kuwa wakiwa na kundi hilo walipata changamoto nyingi ikiwamo kutembea kwa miguu kwa umbali mrefu kutafuta shoo za kuimba ili watambulike.

“Tuliwahi kutembea kutoka Posta hadi Kimara, mara ya kwanza tulisikia kuna shoo ya jamaa fulani, tukatoka Kurasini hadi Posta. Kumbe hatukusikia vizuri ilikuwa ni Kimara na tukalazimika kutembea hadi Kimara kwa miguu, “anasema.

Anasimulia kuwa mwaka 1999, waliingia studio iliyokuwa chini ya Mtayarishaji Endrico,  inayoitwa Sound Craftaz na kurekodi wimbo wa kwanza alioupa jina la ‘Jambo hili ni Batili’.

Anaeleza kuwa mashairi ya wimbo huo yalikuwa yakilenga kupiga vita matumizi ya dawa za kulevya ambayo kwa wakati huo yalikuwa yameshamiri.

Anabainisha kuwa wimbo huo ulifanikiwa kusikika katika kituo cha Redio  One, akieleza kuwa kabla ya kupeleka studio kwa kuwa yeye ni kiongozi alilazimika kurudi mtaani kuokota vyuma chakavu ili kupata fedha za kununulia kanda ya kurekodi wimbo huo na kuzisambaza studio.

Anafafanua kuwa iliwachukua mwezi mzima kutafuta Sh3,000  za kununulia kanda tupu.

“Sikujali kuwa mimi ni kiongozi kwa kuwa niliokuwa nao kwenye kundi hawakuwa na uzoefu wa kuokota vyuma chakavu kama mimi. Nililazimika kuokota kwa kazi mbili, ada na kununulia kanda,”anasema.

Kuibuka kwa Nature

“Mwaka 2000 ni wa historia kwangu kwani nilihitimu kidato cha nne kwa shida na kufanikiwa kuupeleka redioni wimbo wetu tuliorekodi,”anasema Nature.

Hata hivyo, anasema kuwa katikati ya mwaka 2000 kundi lao lilivunjika sababu ikiwa kila mmoja alitafuta njia yake kimaisha baada ya kumaliza shule.

Nature anasema kuwa hali hiyo haikumkatisha tamaa na kuendelea kutembea kwa miguu hadi Kimara kutafuta shoo za kuimba ili kujenga urafiki na wanamuziki wakubwa.

“Kipindi hicho nilidhalilishwa sana na makondakta wa daladala. Kuna wakati nilichoka na kuamua kuvaa nguo za shule, nikajidai  mwanafunzi huku nikionekana baba mzima. Nilishushwa njiani kwa kukosa nauli au kwa kushindwa kuelewana na konda,”anasema.

Anaeleza kuwa kama ilivyo maisha ya uswahilini, majirani na watu wanaomfahamu walimuona kama chizi na kumsema kwa maneno ya kejeli, wakimchukulia kuwa ni mwizi, mtukutu, mvuta bangi na mambo yanayofanana na hayo ingawa ukweli sikuwa na sifa hata moja kati ya hizo.

“Kutoka kimuziki kulikula akili yangu yote wakati huo. Hata nilipoambiwa kuna shoo Kibaha, bila kualikwa na kuhisi naweza kupata nafasi ya kuimba hata wimbo wangu mmoja, ningeenda bila kujali kama nina nauli au sina. Hakuna mtu hata mmoja wa familia yetu ambaye ningemwambia anipe nauli niende huko na kukubali, waliona ni uhuni na upuuzi, “anasema Nature.

Itaendelea wiki ijayo. Usikose kujua Nature ataeleza nini?