Kila mgonjwa anahitaji chakula tofauti

Muktasari:
Kabla ya kuanza kutayarisha chakula cha mgonjwa ni lazima kufahamu ugonjwa wake na kujua miiko ya mlo aliyopewa na daktari kuhusu ugonjwa wake. Kila mgonjwa anahitaji chakula cha aina yake kutokana na hamu aliyonayo au maagizo ya daktari.
Chakula ni muhimu kwa kila mtu lakini zaidi kwa mgonjwa kwa sababu kinahitajika kuimarisha kinga za mwili, kujenga na kuupa mwili nguvu na kuzisaidia dawa kufanya kazi vizuri ili mgonjwa apone haraka.
Kabla ya kuanza kutayarisha chakula cha mgonjwa ni lazima kufahamu ugonjwa wake na kujua miiko ya mlo aliyopewa na daktari kuhusu ugonjwa wake. Kila mgonjwa anahitaji chakula cha aina yake kutokana na hamu aliyonayo au maagizo ya daktari.
Wapo wagonjwa wanaozuiwa kuweka chumvi, sukari au mafuta kwenye vyakula vyao. Ni muhimu kufuata maagizo ya daktari bila ya kumhurumia mgonjwa kwani kuvunja maagizo hayo ni sawa na kufanya juhudi za makusudi ili kumwangamiza.
Kwa mgonjwa asiyejiweza kula chakula cha kawaida iwe ni kutokana na kuzidiwa au kwa maelekezo ya wataalamu wa afya, ni vizuri kumtayarishia kile kitakachoyeyushwa kwa urahisi. Wagonjwa wenye homa kali au homa za matumbo wanahitaji aina hii ya chakula.
Pia, chakula cha maji maji ni muhimu kwani mara nyingi mgonjwa hupoteza nguvu na maji kwa wingi. Uji mwepesi, mchuzi, juisi, maziwa na supu nyepesi iwe ya samaki au kuku wa kienyeji ni mifano ya vyakula muhimu kwa mgonjwa.
Vyakula vingine vyaweza kuwa viazi vilivyopondwa kisha kuchanganywa na maziwa, papai au matunda mengine laini, nyama ya kusaga, samaki wa kuchemsha, yai lililopikwa, ugali laini na mboga za majani ni mifano ya vyakula vinavyofaa kwa mgonjwa.
Vyakula hivi pia vinawafaa wagonjwa waliofanyiwa oparesheni au mama aliyejifungua kwa njia hiyo na wakati mwingine hata kwa njia ya kawaida ili haja kubwa isiwe ngumu itakayosababisha kutumia nguvu nyingi wakati wa kuitoa jambo linaloweza kufumua nyuzi zilizoshonwa baada ya upasuaji.
Chakula cha mgonjwa kinapaswa kiwe na aina zote za virutubisho vinavyohitajika mfano wanga, protini, mafuta hasa ya mimea, madini, vitamini, nyuzilishe na maji. Chakula cha mgonjwa kinapaswa kutayarishwa kwenye mazingira safi kuanzia kinapoandaliwa mpaka kinapofikishwa mezani ili kiliwe. Kinga za mwili za mgonjwa, mara nyingi, huwa dhaifu jambo linalohitaji umakini ili kutomuongezea vimelea vya magonjwa kupitia chakula. Endapo hakutakuwa na umakini wa kutosha, mgonjwa atapata maambukizi mengine, mapya.
Wakati wa kutayarisha chakula cha mgonjwa ni vizuri kuzingatia ladha nzuri ya kupendeza na yenye kuvutia macho. Mchanganyiko wa matunda au mboga za aina tofauti humvutia mgonjwa na kumuongezea hamu ya kula.
Vyombo vinavyotumika kuandaa chakula hicho ni muhimu kwa afya ya mgonjwa. Chakula ni lazima kipakuliwe kwenye vyombo safi na visivyokuwa na hitilafu yoyote vinafaa zaidi.
Vyombo vilivyokunjika vilivyopasuka havifai kwani vinaweza kuleta balaa lisilotarajiwa. Chakula kipakuliwe kidogo na mgonjwa ale hivyo. Akimaliza aongezewe kingine.
Kumpakulia mgonjwa chakula kingi kunaweza kusiwe busara kutokana na ulaji wa taratibu na uwezekano wa kupoa kabla hakijaliwa.
Maumivu ya ugonjwa yanatajwa kuwa sababu nyingine inayoweza kumfanya mgonjwa apoteze hamu ya kula.
Mgonjwa anahitaji kuhimizwa kula ingawa linaweza lisiwe jukumu zito kama chakula ni kizuri, safi na kimewekwa kwenye vyombo visafi.