Kutoka kona ya ‘stejini’ mpaka urubani

Mbali ya umaarufu, fedha na kipaji alichonacho, Ambwene Yesseyah ni mmoja kati ya wasanii wachache walioamua kurudi chuo kwa ajili ya kutimiza ndoto zake za kuwa rubani wa ndege katika maisha yake yote.
Muktasari:
- Anasema hatua hiyo ilikuwa ni ndoto yake kubwa aliyoitamani tangu akiwa mwanafunzi wa Sekondari ya Ufundi Ifunda. “Nadhani ndoto zangu ndiyo zitaanza kutimia, sikufikiria muziki ila kwa sababu ya changamoto bado sikukata tamaa,” anasema.
Maswali ni mengi yasiyokuwa na majibu miongoni mwa wasanii wengi katika harakati za mafanikio yao kimuziki yamekuwa yakiibuliwa kila kukicha.Hata hivyo miongoni mwa wasanii hao wamekuwa wakijaribu kujikita katika mbadala wa fursa wanazokutana nazo.
Asilimia kubwa ya wasanii waliofanikiwa kushika shilingi hapa nchini, wameshindwa kufikiria suala la kurudi darasani huku baadhi yao wakitoroka bila kumaliza hata elimu ya sekondari.
Hata hivyo mbali ya umaarufu, fedha na kipaji alichonacho, Ambwene Yesseyah ni mmoja kati ya wasanii wachache walioamua kurudi chuo kwa ajili ya kutimiza ndoto zake za kuwa rubani wa ndege katika maisha yake yote.
Anasema hatua hiyo ilikuwa ni ndoto yake kubwa aliyoitamani tangu akiwa mwanafunzi wa Sekondari ya Ufundi Ifunda. “Nadhani ndoto zangu ndiyo zitaanza kutimia, sikufikiria muziki ila kwa sababu ya changamoto bado sikukata tamaa,” anasema.
AY anasema kwa sasa anajiandaa kuanza masomo ya kozi ya urubani katika Chuo cha Mafunzo ya Urubani cha ‘Mosswood Aviation Academy’ kilichopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere(JNIA).
Hatua hiyo anasema haitakuwa na tafsiri ya kuachana na kazi ya muziki.“Nimeshalipia gharama zote, nimejaza fomu za kujiunga na Januari mwakani 2014 nitaanza kozi,” anasema AY.
Katika kozi hiyo AY anasema atahakikisha anasoma ngazi zote za leseni kabla ya kuanza kuruka hewani. “Lengo langu lazima litimie sitafikiria kuhusu gharama zinazohitajika,” anasema.
Alikotoka ni mbali
Utambulisho sahihi wa jina lake ni Ambwene Allen Yessayah aliyezaliwa mkoani Mtwara na kumaliza kidato cha nne katika Sekondari ya Ufundi, Ifunda iliyopo mkoani Iringa.
Ni mmoja kati ya wasanii wachache na ‘wabishi’ katika maisha akiwa na kumbukumbu ya kuwa mwimbaji wa kwanza kuimba staili za muziki aina ya Komesho, Rap na Hiphop hapa nchini.
Alianza kujitambulisha na nyimbo kadhaa ikiwamo Raha tu 1-2, Raha Kamili, Machoni kama watu, Binadamu na baadaye akaendelea kufanya vizuri katika anga za Afrika Mashariki, Kati, Afrika na sasa analazimisha kutambulika kidunia.
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa jamaa huyu alitokea katika kundi la East Coast Team lililokuwa likiongozwa na Gwamaka Kaihula maarufu kama King Crazy GK kutoka maskani yao Upanga, jijini Dar es Salaam.
Msanii pekee Tanzania
Mpaka sasa ni msanii anayeripotiwa kufahamika nje ya nchi kuliko wasanii wote nchini. AY amefanya kazi na wasanii mbalimbali akiwamo J Martis na P Square wa Nigeria, Chameleon na Ngoni (Uganda), Sean Kingston (Jamaica), Nameless, Aman na Jua kali (Kenya) pamoja na Lil Romeo wa USA.
Hapa anafafanua, “ Ninapokumbuka njia hizo huwa ninaamini kila kitu kinawezekana, sifa moja kubwa niliyonayo ni kuthubutu kufanya jambo ambalo linafikiriwa kutowezekana,” anasema.
Anasema juhudi za kufanikiwa katika muziki hazihusishwi na ‘Kolabo’ za wasanii wakubwa.” Mimi nilijitengeneza mapema na ndiyo sababu ya kuamini hivyo. Msaada wangu mkubwa zaidi kwa chipukizi ni mawazo, mbinu na uboreshaji wa kazi zao,” anasema AY.
Shoo tatu kali
Kuwa chini ya Meneja wake Mmarekani Hemdee tangu mwaka 2002, imekuwa ikitafsiriwa kuwa chanzo cha kukuza soko lake kimuziki. AY amefanya shoo nyingi za ndani na nje ya nchi lakini anathubutu kutaja shoo kali tatu miongoni mwa hizo.
Anasema shoo ya kwanza kufanya nje ya nchi alifanya akiwa nchini Uganda mwaka 2003, akiwa msanii wa kwanza kulipwa pesa nyingi katika shoo za nje.
“Nilipata Dola 2,000 (sawa na Sh3 milioni) nikiwa mimi na O ten, tulifanya shoo na wasanii wakubwa akiwamo Namless, Chameleon na Street bush,” anasema AY.
Anasema shoo yake kubwa na ya pili ilifanyika Durban nchini Afrika Kusini mnamo mwaka 2005, akiwa ameongozana na Lady JD.
Shoo hiyo iliyofahamika kama tuzo za Kola, alifanikiwa kukutana na wasanii wakubwa wa kimataifa akiwamo Miss Eliot, Shaggy na wengine kadhaa kutoka Mashariki ya mbali.
“Shoo ya tatu na kubwa ilikuwa ni Malaysia mwaka 2009, shoo ile niliipenda sana kwa sababu nilipokelewa vizuri,” anasema.
Aidha, anaongeza kuwa kitu muhimu alichokifurahia katika shoo hizo ni pamoja na kukuza jina lake katika mipaka ya nchi.“Ndiyo uliokuwa mwanya zaidi wa kupiga hatua ya kukuzaa muziki wangu,” anasema.
Nje ya muziki
Inawekezana idadi kubwa ya mashabiki wake hawatambui ukurasa wa pili katika maisha ya kila siku kwa msanii huyo, hususan katika shughuli za kijasiriamali.
AY anasema mbali na muziki pia ni mmoja kati ya wamiliki wa Kipindi cha Mkasi kinachorushwa katika televisheni ya East Africa.
“Katika umiliki wa kipindi hicho tupo watatu, mimi ambaye ni Core Director (Mkurugenzi Msaidizi), Salama (Mtangazaji) na Josh ambaye ni ‘Producer’ (mzalishaji),” anasema.
Mbali na hiyo AY ni mmiliki wa Kampuni ya Matangazo iitwayo ‘Unit Entertainment’. “Katika kampuni hiyo naendesha kazi mbalimbali za muziki ikiwamo za wasanii wakubwa tu kama vile Ommy Dimpoz na FA,” anasema.