Elimu ya Tehama shuleni; Tujifunze kutoka nchi jirani

Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Mpunyule iliyopo Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi wakijifunza somo la Tehama. Baadhi ya nchi jirani ikiwamo Rwanda zimeshaanza ufundishaji wa vitendo kwa somo la kompyuta. Picha kwa hisani ya mtandao wa HakiElimu
Muktasari:
- Tayari Kenya na Rwanda zimeshaanza utekelezaji wa mpango wa kugawa kompyuta shuleni. Matumizi ya kompyuta shuleni, yanatajwa pia katika shule za Tanzania, lakini swali ni; je, tumejiandaa kwa matumizi yake kama ilivyo kwa wenzetu?
Moja ya nchi zinazotajwa kupiga hatua kwenye matumizi Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) shuleni katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ni Rwanda ambapo inakadiriwa kuwa nusu ya wanafunzi wanatumia kompyuta mpakato wakiwa shuleni.
Inakadiriwa kuwa, zaidi ya shule za msingi 1,200 nchini humo zina kompyuta na kwa uchache asilimia 10 ya shule za sekondari zimeunganishwa na mtandao wa intaneti.
Nchi ya Kenya nayo kwa sasa inaendesha kampeni ya kila mwanafunzi kupata kompyuta moja. Ni mpango unaotarajiwa kuzifaidisha shule zote nchini humo ifikapo Aprili mwaka huu.
Matumizi ya kompyuta hasa zilizounganishwa na mtandao wa intaneti katika sekta ya elimu, ni moja ya njia zinazotazamiwa kuboresha kwa kiasi kikubwa hali ya utoaji elimu.
Hii ni kutokana na ukweli kuwa, kwa kutumia intaneti mwanafunzi anaweza kupata maarifa makubwa, hasa katika nchi kama yetu ambayo ina uhaba mkubwa wa walimu.
Hali ikoje Tanzania?
Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ntambi Bunyazu anasema kuwa Serikali ina mikakati mbalimbali ya kuhakikisha elimu inatolewa kwa njia ya Tehama.
Anasema kuwa, kwa kuanza imeanza kutoa mafunzo kwenye vyuo vyote vya ualimu, ili kuwawezesha walimu tarajali kuwa na elimu ya teknolojia hiyo itakayowawezesha kufundisha kwa urahisi shuleni.
“Wanafunzi wanaosomea ualimu kwenye vyuo vyote vya Serikali, wanafundishwa namna ya kutumia Tehama kufundisha, hiyo ni moja ya njia za kuhakikisha wanaweza kutoa elimu kwa njia hiyo,” anasema.
Anaeleza kuwa mbali na walimu waliopo vyuoni, pia walimu waliopo shuleni hasa wale wa masomo ya Sayansi, Hisabati na Kiingereza wanafundishwa kwa awamu namna ya kutumia teknolojia hiyo kuwafundisha wanafunzi wao.
Anasema kuwa, wameanza na walimu hao, kwa sababu ya umuhimu wa masomo hayo katika maendeleo ya nchi.
Vifaa vya Tehama shuleni
Bunyazu anasema, mbali ya kutoa mafunzo kwa walimu, tayari Serikali imeanza kusambaza baadhi ya vifaa vya Tehama shuleni kama vile kompyuta.
Hata hivyo, anasema kwa sababu ya kuwepo kwa uhaba mkubwa wa walimu, Serikali inajipanga pia kutumia njia ya redio kufundishia wanafunzi shuleni.
“Zamani wakati sisi tunasoma tulikuwa tunawekewa redio darasani halafu mtaalamu labda wa Kiswahili anafundisha, nchi nzima ilikuwa inamsikiliza. Njia hii inapunguza hata tatizo la walimu, asema na kuongeza kuwa njia hii inaweza kutumika kwa sasa endapo walimu watahamasishwa kuitumia.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Hassan Mshinda anasema kuwa suala la utoaji elimu kwa kutumia Tehama linawezekana nchini.
“Kuna mipango mbalimbali iliyopo ya kutoa elimu kupitia Tehama shuleni, miradi hii inatekelezwa kwa awamu,” anasema na kuongeza kuwa changamoto zilizopo zinaweza kutafutiwa ufumbuzi ili hatimaye ndoto ya kutumia Tehama shuleni itimie.
Wasemavyo wadau
Makamu wa Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Honoratha Chitanda anasema kuwa utoaji wa elimu kupitia Tehama unawezekana, kama Serikali itaamua kwanza kujenga miundombinu yake shuleni.
“Kufundisha kwa Tehama kunawezekana tukiamua kuboresha miundombinu ya shule zetu, shule nyingi hazina kompyuta na umeme. Lazima turekebishe kwanza miundombinu,” anaeleza.
Chitanda anasema tatizo la kutokuwepo kwa miundombinu linavikabili pia vyuo vya ualimu. Ana wasiwasi kuwa hata walimu wenyewe wanaweza kukosa mafunzo bora ya Tehama, hivyo kukwaza juhudi za kutumia Tehama kufundishia shuleni.
“Hata ukienda kwenye hivyo vyuo vya ualimu unakuta wanafunzi 800 kompyuta 20, watajifunziaje kwenye mazingira kama hayo?” anafafanua.
Akiamini kuwa Tehama ni moja ya njia bora kwa wanafunzi kujifunza maarifa mbalimbali, Chitanda anasema:
“Ni vyema sasa tukaanza kujenga maabara za kompyuta badala ya hizi za sayansi ambazo kila shule imeambiwa ijenge moja. Walimu pia wafundishwe ili wapate uzoefu, mafunzo kazini ni muhimu sana.
“Wapewe mafunzo na vifaa, kwa sababu mkongo wa Taifa upo karibu kila mahali, wanafunzi wanapenda sana kutumia kompyuta ila lazima tukubali kuwa kwa sasa bado tuna safari ndefu, kwa sababu hakuna vifaa na walimu bado hawajaandaliwa ya kutosha.”
Naye Mhadhiri Mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Ruth Meena anasema kuwa tatizo linalorudisha nyuma maendeleo ya elimu nchini, kutokufanya mambo kwa kufuata vipaumbele.
Anashangaa kuwa wakati Kenya ikijipanga kusambaza kompyuta shuleni, Tanzania bado inahangaika na uhaba wa madawati.
“Hapa hapa kwetu inawezekana, suala ni kupanga tu vipaumbele vyetu, tupunguze matumizi ya anasa ambayo hayatusaidii na tuwekeze kwenye elimu.
Tukipunguza magari ya kifahari na matumizi yasiyo ya lazima, miundombinu kama umeme wa jua itaenda shuleni na miundombinu mingine itaboreshwa, na hapo tutaaza kutoa elimu yetu kwa njia tunayotaka,” anasema.